Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Si lazima kila mtu apitie kwenye maumivu yako

Muktasari:

Tutaendeleaje kama nchi kama wengine hawaoni umuhimu wa kuongeza idadi ya watu watakaochangia maendeleo hayo? Huo ni uchawi au uchoyo? Kwa faida ya nani? Hakika ni kwa hasara ya wote. Hasara kwa huyo anayegoma kuwafundisha wengine, hasara kwa hao waliotakiwa kufundishwa na hasara kwa nchi kwa jumla. Sijui kama wale wanaofanya upuuzi huu wanazitambua hasara hizo.

Nakumbuka miaka ya nyuma, kuna mtu alinipa usemi unaokera kidogo kwa Mwafrika kwani unaudhalilisha Uafrika. Alisema kwamba kama mzungu akipanda mlima kwa taabu sana akishafika kileleni anatafuta namna ya kupunguza machungu hayo ili watakaofuata wasipate shida aliyoipata. Hivyo kama mlima unateleza basi atatengeneza ngazi. Lakini eti kwa Mwafrika ni tofauti, yeye atahakikisha mlima huo ameweka utelezi kabisa ili watu wengine wasipate unafuu wa kuupanda; yaani hatataka watu wengine wapate urahisi wakati yeye alipata shida katika kuupanda. Sizipendi kabisa fikra hizo kwani ukweli zinaudhalilisha Uafrika. Lakini nikifikiria matukio yanayotokea kwa jamii ninayoishi mimi najiuliza kama kweli hali hiyo siyo uhalisia unaoelezea matukio hayo.

Zaidi ya matukio hayo ya kutaka watu wengine wasipate starehe kama mtu alipata shida upo pia ugonjwa mwingine nao ni kuua mambo yote ambayo mtu anakuta yalishatekelezwa na wale waliomtangulia. Jumapili hii tuyatafakari matukio hayo na namna yanavyoathiri maendeleo yetu katika nyanja mbalimbaili.

Utamkuta mtu anajua shughuli fulani labda kukausha matunda na mboga, soko lipo halafu akashindwa kukidhi mahitaji ya soko kwa kuwa labda hana mtaji lakini mtu huyo asitake kabisa watu wengine kujifunza teknolojia hiyo. Akili za haraka haraka zinaniambia kwamba mtu huyo alipaswa kuwafundisha wengine ili wachangie katika upatikanaji wa kiasi kinachotakiwa. Lakini kwa kuwa mtu hataki wengine wapate faida ya kujua haraka haraka hatawafundisha. Ukiuliza kisa utajibiwa kwamba yeye alianzia chini sana akikausha kwa teknolojia duni sana hivyo anaona na wengine wapitie katika hatua hizo hizo. Hebu fikiria mtu ameshindwa kukidhi mahitaji ya soko lakini anaona kuliko kuwafundisha watu ili mahitaji ya soko yakamilishwe ni afadhali soko libaki na manung’uniko hivyo hivyo. Huu nao ni uchawi wa aina yake. Tutaendeleaje kama nchi kama wengine hawaoni umuhimu wa kuongeza idadi ya watu watakaochangia maendeleo hayo? Huo ni uchawi au uchoyo? Kwa faida ya nani? Hakika ni kwa hasara ya wote. Hasara kwa huyo anayegoma kuwafundisha wengine, hasara kwa hao waliotakiwa kufundishwa na hasara kwa nchi kwa jumla. Sijui kama wale wanaofanya upuuzi huu wanazitambua hasara hizo. Wenzetu wanaokwenda mbele wanajivunia nchi yao kuwa na uwezo wa kuzalisha kitu fulani kwa wingi na watahakikisha kwamba nafasi hiyo ya nchi yao haibomolewi sasa iweje sisi tuone taabu nchi yetu wenyewe kwenda mbele kwa kuwawezesha watu wengi zaidi? Kwa nini watu tuwe na roho ya kutu hivi?

Utakuta ndani ya ofisi mtu mzima mwenye cheo chake anaweka utaratibu mbovu unaozuia vijana kupata vyeo, kisa yeye alikipata cheo chake kwa taabu sana sasa iweje wengine wapate vyeo kirahisi rahisi tu? Huu ni upuuzi wa aina yake. Tutapata wapi viongozi wa kuchukua nafasi za wanaostaafu au kuacha kazi katika taasisi mbalimbali ? Mtu anatakiwa ajifunze namna ya kuongoza toka akiwa kijana akianzia kushika uongozi wa chini halafu anapanda kufikia ngazi ya huyo asiyetaka kuwafundisha wengine. Sasa watajifunzaje kama mtu anawawekea ‘kauzibe’ ili wasipande eti kwa kuwa yeye alisota kufikia nafasi hiyo? Tabia hii inahuzunisha lakini ndiyo hali halisi kwa watu wengine. Wapo wengi wa aina hiyo.

Tuna wahadhiri wenye mawazo ya kuwanyima wanafunzi maksi wanazostahili kuzipata eti kwa sababu wao walisotea sana masomo yao. Wapo wabunifu wanaokufa na ubunifu wao kwa sababu tu wameshindwa kuutoa huo ubunifu kwa watu wengine hata kwa malipo. Wapo wale wanaoacha kazi halafu wakachana nyaraka zote walizoziandaa ambazo zingeweza kurahisisha utendaji wa kazi wa mtu anayekuja kuchukua nafasi hiyo. Kilichopo kichwani mwake! “Naye akatengeneze ya kwake ya kufanyia kazi”. Utakuta sasa badala ya taasisi kwenda mbele kwa mtu kuanzia pale alipoishia mwenzake, inabaki palepale kwa kuwa watu wanatumia muda mwingi kutengeneza mambo ambayo yalishatengenezwa na watu wengine lakini kwa sababu zisizokuwa na msingi hawataki kuendeleza mazuri yote yaliyoachwa. Kwa mtindo huu tutaishia hapa tulipo.

Sasa umezuka mtindo wa ajabu zaidi nao ni ule ambao sasa kibao kinageuka. Mtu anatengeneza mambo ambayo watu wanaofuata wangepata pa kuanzia lakini kwa sababu mbalimbali wanavuruga kila wanachokikuta. Hivi kweli mtu anafika katika ofisi na kukuta wafanyakazi lakini kwa utashi wake akamwondoa tu mtu ofisini na kutamka kwamba atakaa nyumbani lakini atalipwa mshahara. Kwa kosa gani? La kibinafsi. Huo ni wendawazimu na kutojua kuendesha ofisi. Kwa kuwa mtu hatoi mshahara mfukoni mwake anaona ni sawa kabisa kulipa watu wawili kwa nafasi hiyo hiyo. Tutaendeleaje kama watu wanawafuatia watu badala ya tabia. Mtu atataka kubalisha mkao wa watu ofisini, kile wanachokalia, utendaji wa kazi n.k. Siyo kwamba utaratibu, watu au samani alizozikuta zina matatizo hapana ila tu anataka kuona kwamba yule aliyeondoka ameondoka na mipango na ubunifu na utendaji wake wote. Hakika huu nao ni ugonjwa unaorudisha maendeleo ya taasisi nyuma. Hii habari ya kuajiri upya, kununua samani upya, kutengeneza mifumo ya utendaji upya kama haina tija kwa maendeleo ya taasisi husika ni ya nini. Mabadiliko hayo yote ni kwa faida ya nani? Kama kila atakayeingia ataanza na kuvunjavunja yale yote yaliyowekwa na mtu aliyetangulia basi tutaendelea kuwa katika ngazi za chini za maendeleo.

Kutowaachia wengine ujuzi wako au kile unachokijua au kuharibu kile ambacho aliyekutangulia alikitengeneza ni dalali za roho mbaya. Roho mbaya haisaidii katika ukuaji wa taifa. Roho mbaya ni jambo binafsi lakini athari yake ni kwa jamii kwa sababu inarudisha kasi ya maendeleo ya jamii na nchi kwa jumla. Hakika tusipoiache itabidi tukubaliane na usemi huo wa kutudharau kwamba tunataka kila mtu apitie kwenye machungu tuliyopitia. Hii inarudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Jumapili Njema.