TAAMULI HURU: Viongozi wetu wawajibike kwa makosa yao
Kitu chenye thamani kubwa duniani kuliko vyote ni uhai. Uhai wa binadamu unapokatishwa kwa umwagaji damu, hiyo ni hatia. Damu hiyo itaendelea kuwaumiza na kuwatafuna wahusika wa tukio hilo kwa kupitia kitu kinachoitwa karma.
Damu ya kiongozi huyu wa Chadema, aliyeuawa kikatili na mwili wake kutupwa Ununio, siyo tu itawagharimu waliokatisha maisha yake, bali na wengine wote wenye wajibu wa kuzuia kilichotokea, lakini hawakuzuia kwa uzembe.
Kufuatia Watanzania wengi kuwa ni waumini wa dini kuu mbili, Ukristo na Uislamu, hivyo sio wengi wanajua kitu kinachoitwa karma ni nini, kwa sababu karma ni neno la lugha ya kihindi (Hindu) na linafundishwa kwenye dini ya Hinduism na Buddhism, mimi nilijifunza kuhusu karma wakati nikiishi jiji la New Delhi nchini India.
Huu ni wito kwa viongozi wetu, unapokosea hata kwa kujikwaa tu ulimi, tujenge tabia ya kuwajibika kwa makosa yetu, au kwa uzembe wetu kwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti, kabla ya kutokea majanga au maafa.
Karma ni kanuni ya binadamu kulipwa kwa kadiri ya mawazo yake, maneno yake na matendo yake, ukiwaza mema, ukasema mema, ukatenda mema, unalipwa mema. Ukiwaza uovu, ukasema uovu, ukatenda uovu, unalipwa uovu. Kwa kawaida malipo ya karma ni hapa hapa duniani na adhabu kubwa kuliko zote ya karma ni kifo cha mateso makubwa kufidia uovu wako.
Ukimtendea mtu jambo baya, hilo jambo likimuumiza, akiumia moyo, kama hukumtendea haki, wewe uliyetenda, litakufika jambo baya ambalo litakuumiza kufidia maumivu uliyomsababishia mwenzio.
Karma kwenye uongozi
Kwenye uongozi wa umma, jambo zuri na la furaha ni mtu kuteuliwa kwenye nafasi ya wadhifa wa uongozi, iwe ni kwa kuchaguliwa au kuteuliwa na kinacholeta raha ya kweli, siyo malipo ya mshahara mnono na marupurupu, bali ni ule utumishi wa umma wa kuwatumikia watu.
Ukijiuzulu mwenyewe, hata ukiumia vipi, hakuna adhabu ya karma kwa aliyekuteua, lakini ukitumbuliwa, ukiumia, kama hukutumbuliwa kwa haki, unambebesha mzigo wa karma aliyekuteua bila wewe kujijua na bila yeye kujua.
Wito kwa viongozi wote wa umma, ukiharibu, usisubiri kutumbuliwa na kumbebesha mzigo wa karma mkuu wa nchi, wajibikeni kwa kujiuzulu ili kumuepushia mizigo ya karma za uzembe wenu zisizomhusu, maana hizi karma, zinadunduliza, zikifika za kutosha kustahili adhabu.
Kwa kadiri siku zinavyokwenda, wale watu wa Nyerere wanazidi kupungua, katika kizazi cha sasa, waliokuwa wanaujua utawala wa Mwalimu Nyerere ni wachache, wengi ni kizazi kipya cha utawala wa Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli, hivyo inawezekana kabisa, wengi wasielewe kuwa enzi za Nyerere, viongozi wetu walipofanya makosa ya wazi, sio tu waliomba msamaha, bali msamaha huo uliandamana na barua ya kuwajibika.
Kwa viongozi wetu wa sasa, pale wanapofanya makosa ya wazi kabisa au makosa ya kujikwaa kisiasa, tuwaache waombe msamaha na maisha yaendelee kama kawaida au tujenge utamaduni wa viongozi wetu wanapofanya makosa, hata kupishana tu kauli na mkuu wa nchi, kuwajibika kwa makosa yao?
Uwajibikaji wa Mwinyi
Mfano mzuri wa ombi la msamaha likiandamana na uwajibikaji ni kujiuzulu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Hassan Mwinyi kufuatia vifo vya mahabusu wakiwa mikononi mwa polisi, vilivyotokea mwaka 1976 mkoani Mwanza na Shinyanga ambapo mwaka 1977, Waziri Mwinyi aliandika barua kwa Rais Nyerere ya kuomba msamaha na kuwajibika.
Kwenye kadhia hiyo, haikuishia kwa Mwinyi pekee kujiuzulu, bali Rashidi Kawawa aliondolewa kwenye nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Taifa, Peter Siyovelwa alijiuzulu.
Pia, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Emelio Mzena alistaafishwa, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Samuel Pundugu alistaafishwa, Kamisha Mkuu wa Magereza alistaafishwa. Kisha moto huo ukahamia Mwanza, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Peter Kisumo alimwaga unga. RPC, RSO, OCD na DSO wa Mwanza, walistaafishwa kwa manufaa ya umma.
Wakati huo, sio tu unastaafishwa na kuamua kuishi popote, bali unastaafishwa na kufuatwa usiku usiku kusafirishwa kurudishwa kijijini kwenu kwa Landrover 109 za enzi hizo na kukabidhiwa kwa serikali ya kijiji, huruhusiwi kutoka nje ya kijiji bila ruhusa.
Huu uwajibikaji wa enzi za Mwalimu umepotelea wapi? Mahabusu wangapi siku hizi wanakufa mikononi mwa polisi na hakuna uchunguzi wowote wala hatua zozote zinazochukuliwa na hakuna mtu yeyote anayewajibika?
Hitimisho
Ni lini uwajibikaji kwa viongozi wa umma utarejeshwa kwa kiwango cha uwajibikaji wa enzi za Mwalimu? Yaani kiwango cha uadilifu wa mke wa Kaisari? Kiongozi wa umma ni hadi afanye kosa kubwa kiasi gani au uzembe wa kiasi gani chini yake ndipo awajibike?
Viongozi wetu watambue kwamba cheo ni dhamana, ikitokea ukatuhumiwa tu, tuhuma za wazi, hata bila uthibitisho, ama kanusha au wajibika, msiwatwishe wengine mzigo wa karma kama mlivyomponza yule mwingine na karma ikafanya mambo yake.
Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan asilifumbie macho jambo hili, awe mkali kama viongozi waliomtangulia. Mwinyi aliwahi kuwajibika na maofisa wa serikali walishitakiwa kwa uzembe, nini kinachokwamisha uwajibikaji wa kiwango kile?
Rais Samia asikubali kabisa kutiwa madoa ya damu na watendaji wazembe walio chini yake, asibebeshwe mizigo yao. Awe mkali kwenye hili, kila mtu aubebe mzigo wake mwenyewe. Mungu Ibariki Tanzania.