Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TAHARIRI: Athari uhaba wa dola zitafutiwe suluhisho

Uhaba wa Dola ya Marekani ni changamoto kubwa kwa nchi nyingi, hususan zenye utegemezi mkubwa wa bidhaa kutoka nje, Tanzania ni miongoni mwazo.

Dola hiyo inahusika kwa asilimia zaidi ya 80 katika miamala ya kimataifa, kwetu sisi inapokuwa adimu ni vigumu kuagiza bidhaa muhimu.

Uhaba wa Dola za Marekani pia unaathiri thamani ya sarafu yetu na kusababisha gharama kubwa za uagizaji bidhaa, jambo linalochangia kwenye mfumuko wa bei.

Kwa mujibu wa Ripoti Ya Benki Kuu ya Tanzania ya mapitio ya uchumi ya kila mwezi, uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi ulipungua hadi Dola za Marekani 16.027 bilioni (Sh43.51 trilioni) kwa mwaka ulioishia Juni 2024, kutoka Dola za Marekani 16.980.4 bilioni (Sh46.10 trilioni) za mwaka uliotangulia.

Wakati uagizaji ukiwa hivyo, katika kipindi hicho usafirishaji bidhaa kwenda nje ya nchi ulikuwa Dola za Marekani 14.68 bilioni (Sh39.85 trilioni) pekee, hali inayoonyesha nakisi (upungufu) ya zaidi ya Dola 1.34 bilioni (Sh3.63 trilioni ya biashara), hivyo kuwepo umuhimu wa kuzalisha zaidi bidhaa za kuuza nje na za kutumia ndani ili kupunguza zaidi uagizaji.

Miongoni mwa bidhaa ambazo Tanzania inaagiza kwa kiasi kikubwa ni bidhaa za mashine na za viwandani, plastiki, bidhaa za chuma, mbolea, vipuri, mafuta ya kupikia na mafuta ya petroli, magari na sukari.

Pia inaagiza baadhi ya vyakula, dawa za binadamu na za kuua wadudu, sabuni, bidhaa za nguo na karatasi.

Kuendelea na wingi wa bidhaa hizi kutoka nje ni sababu tosha kwamba matumizi yetu ya dola yataendelea kuwa makubwa na hivyo kuna jambo lazima lifanyike.

Hali hii katika kipindi ambacho dola imeadimika, inasababisha kuongezeka kwa gharama za maisha, kushuka kwa thamani ya shilingi yetu, mfumuko wa bei na hatari ya kudorora kwa uchumi.

Pamoja na hatua nyingine ambazo Serikali inazichukua, eneo la kuongeza nguvu ni katika uzalishaji wa ndani wa bidhaa ambazo kwa kawaida hununuliwa zaidi nje ya nchi kwa ajili ya viwanda na matumizi binafsi.

Ikiwa nchi inaweza kuzalisha bidhaa zinazohitajika ndani, inamaanisha kuwa itahitaji kutumia dola chache au kutotumia kabisa kuagiza bidhaa hizo kutoka nje.

Kwa mfano, kuwekeza katika uzalishaji wa chuma ndani ya nchi kunaweza kupunguza uagizaji wa chuma kutoka nje, hivyo kupunguza matumizi ya dola.

Pia, ni muhimu kuongeza kasi ya matumizi ya gesi kwenye magari ili kupunguza matumizi ya dola kwenye uagizaji mafuta, bidhaa ambayo inaongoza kwa kutafuna dola nyingi, ikifuatiwa na chuma.

Serikali iendelee kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kwenye maeneo ya kimkakati, kama kwenye uzalishaji wa sukari, mafuta ya kula, nguo, plastiki na kilimo kwa ajili ya chakula na kuuza nje, ili kupunguza matumizi ya fedha za kigeni na kuimarisha uchumi kwa kuongeza uzalishaji na ajira.

Pato la ndani litakapoongezeka, kuna uwezekano wa sarafu ya ndani kuwa imara zaidi ya ilivyo na kuchangia ongezeko la mapato ya Serikali kupitia kodi.

Vilevile, uzalishaji wa ndani unachochea ubunifu na uvumbuzi, kwani wazalishaji wa ndani watahitaji kubuni njia bora za uzalishaji ili kushindana na bidhaa za kimataifa. Hatua hii pia inachangia kusambaza ujuzi kwa wazawa, kuongeza ubora wa bidhaa za ndani na za soko la nje, na hivyo kuweka uwezekano wa kupata fedha za kigeni.