TAHARIRI: Jamii isifumbie macho ukatili wa 'waliotumwa na afande'
Katika gazeti letu la jana tuliandika habari ikilinukuu Jeshi la Polisi nchini, likieleza kuanzisha uchunguzi wa tukio la kikatili la kubakwa na kulawitiwa kwa msichana mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam kulikofanywa na wanaume watano.
Hii ni baada ya kusambaa kwa picha ya video katika mitandao ya kijamii zikiwaonyesha wanaume hao wakimlawiti na kumbaka msichana huyo kwa zamu, kitendo ambacho hakikubaliki kwa jamii iliyostaarabika na hakipaswi kufumbiwa macho.
Katika video hizo, wanaume hao wanajirekodi pasipo hofu yoyote na kufurahia kitendo hicho wakimtuhumu msichana huyo kutembea na mume wa mtu na baada ya kumaliza unyama wao huo, walimtaka amuombe radhi mwenye mume.
Kwanza tunalipongeza Jeshi la Polisi, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake na wenye mahitaji Maalum, Dk Dorothy Gwajima na Watanzania kwa namna walivyojitokeza haraka kulaani tukio hilo la kikatili lisilovumilika.
Ni lazima Jeshi la Polisi lihakikishe linawasaka wote kuanzia aliyetoa maagizo ya kufanyika kwa tukio hilo na waliotekeleza tukio, ili kwanza umma uwajue na kisha wafikishwe katika vyombo vya sheria bila kujali nafasi, kazi au wadhifa wao.
Lakini wakati Jeshi la Polisi likishughulika na wahalifu hao, tunaiomba jamii kwanza isiendelee kusambaza video hizo lakini pili ni kuiomba jamii itoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili watu hao wakamatwe.
Tunafahamu kifungu cha 131A cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, kinasema mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kubaka kwa kikundi, atahukumiwa kifungo cha maisha jela.
Ni kwa msingi huo, tunatoa rai kwa vyombo vya uchunguzi kuwasaka kwa udi na uvumba waliopanga na kutekeleza tukio hilo na kuwafungulia mashitaka, ili watakapotiwa hatiani iwe fundisho.
Kitendo hicho kwa namna yoyote ile hakiwezi kuhalalishwa na sababu yoyote ile iwe ya utamaduni au vyovyote kama ambavyo waliotekeleza unyama huo walitaka kutuma ujumbe kuwa ni kosa kwa mtu kutembea na mke au mume wa mtu.
Tunasema hivyo kwa sababu Tanzania inaongozwa kwa misingi ya utawala bora unaoheshimu utawala wa sheria na kwa mujibu wa Ibara ya 107A ya Katiba ya Tanzania, Mahakama ndicho chombo cha utoaji haki hapa nchini.
Kwa hiyo, kwa vyovyote vile kama kuna mwanamke mwingine alimtuhumu msichana huyo kutembea na mumewe, alipaswa afungue kesi ya madai kortini na kudai fidia, lakini si kujichukulia sheria mkononi ambalo ni kosa la jinai.
Lakini wakati tukisubiri kuona matokeo ya uchunguzi, tunaona ni vyema kwa Serikali na asasi za kiraia zinazotetea haki za binadamu, zione umuhimu wa kumtafutia msichana huyo wataalamu wa saikolojia ili kuweza kumtibu.
Tunasema hivyo kwa sababu kitendo cha kumbaka na kumlawiti msichana huyo kwa zamu tena akirekodiwa na video kusambazwa katika mitandao ya kijamii, kitakuwa kimemsababishia athari kubwa za kiakili na kisaikolojia maishani.