Tutafute maisha tukijali usafi pia
Katika kona mbalimbali za nchi yetu, wananchi tumekuwa tukiamka kila alfajiri tukiwa na matumaini ya kutafuta riziki.
Ni hali inayoonyesha juhudi zetu kubwa za kujitafutia maisha halali kwa njia ya kazi na juhudi zetu.
Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo, kuna jambo moja ambalo linaonekana kuachwa nyuma na wengi wetu, nalo ni usafi wa mazingira.
Katika maeneo mengi ya mijini na hata vijijini, biashara ndogondogo zimekuwa njia muhimu ya maisha ya wengi.
Wamo mama ntilie wakipika chakula barabarani, vijana wakisukuma mikokoteni ya matunda, wachuuzi wa samaki, wauzaji wa mahindi ya kuchoma, karanga, mayai ya kuchemsha, vitumbua, mishikaki na bidhaa nyingine lukuki.
Biashara hizi ni halali na zina mchango mkubwa kwenye uchumi wa mtu mmoja mmoja na hata wa Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, jambo la kusikitisha ni kwamba, sehemu nyingi ambazo biashara hizi zinafanyika zimekosa kabisa viwango vya msingi vya usafi. Taka hutupwa ovyo, maji machafu hutiririka bila mpangilio, vyombo vya kupikia na kuhifadhia chakula havina usafi wa kutosha, na mara nyingine chakula kinauzwa sehemu zinazopakana na mifereji ya maji machafu.
Mama ntilie ni mifano hai ya wananchi wanaojitahidi kupambana na hali ya maisha kwa njia ya kujiajiri.
Wanakaa na sufuria zao barabarani, chini ya mti au pembeni mwa jengo, wakipika wali, maharage, ugali, mboga na kuuza kwa watu waendesha bodaboda, wafanyakazi na wapita njia.
Lakini tunapoangalia mazingira ya biashara hizo, tunagundua kuna changamoto kubwa ya usafi. Kuna mama ntilie anayepika karibu na dampo la taka, au mwingine anayesafisha vyombo kwa kutumia maji yasiyo safi wala salama.
Wapo wanaokosa sehemu za kutupia taka, au hata vyombo vya kuhifadhia chakula kuwa visafi. Hali hii siyo tu inahatarisha afya ya mteja, bali pia ya mfanyabiashara mwenyewe.
Wauzaji wa matunda, nao wamekuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa wakazi wa miji. Lakini ukweli ni kuwa, wengi wao hawazingatii usafi wa mazingira wala wa matunda wanayouza. Tunashuhudia matunda yakipangwa juu ya meza zilizochakaa, baadhi yakiwa wazi bila kufunikwa, na wakati mwingine yakiwa karibu kabisa na vumbi.
Wengine wanakata matunda kwa kutumia visu visivyo safi, na kuvihifadhi katika vyombo visivyo salama kiafya.
Ni dhahiri kuwa mteja anayenunua matunda haya anajiweka kwenye hatari ya kupata maradhi kama kuhara, kipindupindu na magonjwa mengine ya tumbo.
Wakati mwingine, haya madhara hayaonekani haraka, lakini kwa muda mrefu yanamwathiri mtu kiafya.
Wapo wanaoamini kuwa suala la usafi ni kazi ya halmashauri za miji au serikali pekee. Lakini huo ni mtazamo wa kupotosha. Usafi ni jukumu la kila mmoja.
Hali ya usafi wa mazingira inaanzia pale mtu anapoamua kutotupa taka ovyo, kuhakikisha eneo lake la biashara ni safi, na kutumia vyombo sahihi vya kuhifadhia taka na maji.
Mfanyabiashara mdogo anayeuza barabarani anapaswa kuwa mfano wa uzalendo kwa kuhakikisha kuwa bidhaa zake na eneo lake ni safi.
Viongozi wa mitaa, maofisa afya na halmashauri wanayo nafasi ya kusaidia kwa kutoa elimu na kusimamia sheria ndogondogo zinazohusiana na usafi wa mazingira.
Lakini kama wananchi hawatakuwa tayari kubadilika, juhudi hizo zitakuwa bure. Usafi uanze na mtu binafsi kabla haujawekwa kwa shuruti.
Ni muhimu kuelewa kuwa hatutakiwi kuchagua kati ya kutafuta maisha na kuwa wasafi. Tunaweza kufanya vyote viwili kwa pamoja. Mfanyabiashara wa barabarani anaweza kuweka meza yake juu ya mfuko wa plastiki, ili kuzuia vumbi, anaweza kutumia dumu la majisafi kwa ajili ya kusafisha vyombo vyake, na anaweza kuwa na chombo maalum cha kuhifadhi taka.
Kama taifa, hatuwezi kuendelea ikiwa tunawekeza nguvu kubwa kwenye kazi na kutupilia mbali afya. Kila mjasiriamali mdogo anapaswa kutambua kuwa mteja ana haki ya kupata huduma safi, salama na isiyo na madhara kiafya.
Maendeleo hayawezi kuja kwa uchafu. Uchumi wa mtu mmoja mmoja unaweza kukua kwa biashara ndogo ndogo, lakini ukaharibika kutokana na gharama za matibabu za magonjwa yanayosababishwa na uchafu.
Ni wakati wa kila mmoja wetu kutambua kuwa usafi si jambo la ziada, ni hitaji la msingi. Tutafute maisha, tujikimu, tufanye biashara, lakini tusisahau jambo hili kuwa usafi ni afya, na afya ni maisha.
Tuchague maisha bora kwa kazi safi. Tujitume, lakini tukumbuke usafi.