Tuwatumie wasanii kupanda miti

“Tutaangalia tufanye nini sasa ili mazingira yetu yajayo yawe bora zaidi, ni namna gani tuishi, hatua gani tuchukue kuhakikisha kila mmoja anatoa mchango katika hili”.

“Tutaangalia pia tutumie mbinu na ubunifu gani kuja na njia ambazo ni rafiki kwa mazingira.

Pia tutaangalia ushirikishwaji wa makundi ambayo yanaachwa nyuma,” Hizi ni nukuu za Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu alipokuwa akizungumza kwenye jukwaa la fikra lililoandaliwa na kampuni hiyo kuhusu mapambano ya mabadiliko ya tabianchi.

Jukwaa hilo la fikra mwaka 2023 liliandaliwa mahsusi kujadili nini kinafuata kwa Tanzania baada ya mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (COP 27).

Maono haya ya Machumu pamoja na timu nzima ya MCL, lengo lake hasa ni kuhakikisha Tanzania inakuwa salama na kila Mtanzania anafahamu mashara yatokanayo na mabadiliko hayo ya tabiachi.

Kama alivyosema ni vema kuangalia ushirikishwaji wa makundi yanayoachwa nyuma. Kama ambavyo MCL wanajipanga kuhakikisha kunakuwa na elimu na mapambano ya moja kwa moja ya mabadiliko ya tabiachi, kuna baadhi ya taasisi pia zimeliona hilo na kuunganisha nguvu, ubunifu kuhakikisha hili janga haliiachii nchi athari kubwa.

Bunfu hizo ni pamoja na kutumia kila nyenzo iliyopo an yenye ushawishi kushiriki kutoa elimu , kupanda miti na kufanya vitu vingine vya namna hiyo, ilimradi kufikisha ujumbe wa kulinda na kutunza mazingira.

Wasanii wa kada mbalimbali wa Tanzania pia hawako nyuma katika hilo, kwani watajumuika na kupanda miti katika jiji la Dodoma Machi mwaka huu.

Shughuli hiyo ni sehemu ya mradi mkubwa wa upandaji miti unaoratibiwa na Taasisi ya LP Media kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Akizungumza juu ya mradi huo, Ofisa Miradi wa Taasisi ya Sanaa ya LP Media inayoendesha mradi huo, Abdallah Kambangwa alisema wasanii wapatao mia moja wa kada mbalimbali watapanda miti kwa ajili ya kukijanisha ardhi inayotishiwa na ukame, ili kuhami kizazi kilichopo na kijacho dhidi ya tishio la jangwa na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa sasa ni janga la dunia.

Mradi huo unaanzia Dodoma kwa sababu ni miongoni mwa mikoa ya kanda ya kati yenye ukame na uhitaji mkubwa wa misitu.

Kwa asili mikoa ya kanda hiyo imeathiriwa na hali ya jangwa ikiwa na msimu mdogo wa mvua na vipindi virefu vya jua na upepo mkali.

Zaidi ya Dodoma, mikoa mingine iliyomo kwenye janga hilo ni Singida, Shinyanga, Simiyu, Manyara, Tabora, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro na Kagera.

Tangu Serikali ilipotangaza kuhamia Dodoma, idadi ya watu imekuwa ikiongezeka siku hadi siku kutokana na wahamiaji na ongezeko la asili kama ilivyoainishwa katika sensa ya mwaka 2022).

Ongezeko hilo linakwenda sambamba na ongezeko la shughuli za kibinadamu na za kimaendeleo zikiwemo usafirishaji, ujenzi wa viwanda, miundombinu, majengo makubwa na ongezeko la hitaji la nishati ikiwemo mkaa.

Vyote hivyo kwa pamoja vinatajwa kuchangia uharibifu wa mazingira.

Tofauti na upandaji miti mwingine, mradi huu unaoitwa Green Dom utaratibu upandaji na utunzaji wa miti.

Ambapo miti iliyopandwa itahudumiwa na kuhakikishwa maendeleo yake kwa awamu hadi itakapokua.

Azma yao kubwa ni kuikijanisha sehemu husika na kuondoa kabisa hali ya jangwa ili kuweka usawa wa mahitaji ya kimazaingira kwa viumbe hai, pamoja na kuisaidia Serikali kutekeleza mkataba wa kimataifa wa kurudisha misitu iliyoharibiwa.

Msanii wa filamu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya LP Media, Madebe Lidai alisema taasisi yake itaanza kutekeleza mradi huo kwa kutoa elimu ya upandaji miti, uhifadhi wa misitu, ufugaji nyuki na uzalishaji wa nishati mbadala kwa semina ya siku mbili kwa wasanii na wanamichezo hao, kisha shughuli ya utoaji elimu hiyo kwa wananchi katika maeneo ya wazi.

Elimu itatolewa kwa njia ya filamu na uhamasishaji utakaofanywa na wasanii na wanamichezo waliopata mafunzo.

Mara baada ya mafunzo shughuli ya upandaji miti katika maeneo yaliyoainishwa itatekelezwa kwa kushirikiana wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, wananchi, wadau wa mazingira na Serikali kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji hadi Taifa.

Miongoni mwa mambo aliyosisitiza Lidai ni kuwaomba wafadhili wajitokeze kwa wingi ili kuuwezesha mradi ufanye kazi iliyokusudiwa kwa kiwango cha juu.

Mabadiliko ya tabiachi yakitokea popote nchini athari zake zinaweza kuigusa nchi nzima, hivyo kama wadau wanavyosisitiza wananchi wote wana wajibu wa kushiriki katika mapambano haya.