UCHAMBUZI: Coastal Union ni mfano bora wa kuigwa Ligi Kuu

Coastal Union ni miongoni mwa timu ambazo zimefanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Hadi wakati ligi hiyo iliposimamishwa, timu hiyo ya mkoani Tanga ipo katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 46 ilizokusanya katika jumla ya mechi 28 ilizocheza.

Imeibuka na ushindi mara 13 ikitoka sare mara saba na kupoteza michezo nane huku ikifunga jumla ya mabao 27 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 19.

Ndiyo timu inayoshika nafasi ya pili kwa kuruhusu idadi ndogo ya mabao nyuma ya Simba kwani vinara hao wa ligi wamefungwa jumla ya mabao 15 wakati Yanga na Azam FC kila moja ikifungwa mabao 20.

Ukiondoa matokeo na nafasi yake kwenye msimamo wa ligi, pia Coastal Union imeibua vijana ambao wamekuwa na kiwango bora na kupelekea kuwindwa na timu mbalimbali zinazoshiriki ligi hasa zile kubwa za Yanga, Simba na Azam.

Mfano wa wachezaji hao ni kipa Soud Abdallah ‘Dondola’, mabeki Bakari Mwamnyeto, Hassan Kibailo na Abdallah Ame, viungo Ayoub Semtawa na Mtenje Albano pamoja na washambuliaji Ayoub Lyanga, Hija Ugando pamoja na Issah Abushehe.

Haishangazi kuona Mwamnyeto akiwa tegemeo pia katika kikosi cha timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ ambako ameweza kuwa na nafasi ya kudumu kutokana na kiwango bora alichoonyesha ndani ya muda mfupi lakini pia hata Lyanga naye amekuwa akiitwa mara kwa mara ingawa amekuwa hana namba.

Ubora wa wachezaji hao na kiwango kizuri ambacho Coastal Union wanaonyesha msimu huu ni matokeo ya muunganiko mzuri walionao kitimu ambao kwa kiasi kikubwa umechagizwa na juhudi za benchi lao la ufundi linaloongozwa na nyota wa zamani wa timu hiyo, Juma Mgunda.

Ni timu ambayo inahitaji pongezi za kipekee msimu huu kwa sababu inaundwa na kundi kubwa la wachezaji vijana ambao kwa wastani, umri wao ni chini ya miaka 24 na wengi wao hawajawa na uzoefu wa kutosha wa ligi.

Hayo yanaikuta Coastal Union ambayo haina nguvu kubwa ya kiuchumi na imekuwa ikijiendesha kwa bajeti kiduchu kuanzia gharama za mishahara na posho, usajili na hata huduma nyingine muhimu kwa wachezaji kama malazi, matibabu na usafiri.

Lakini pamoja na changamoto hizo, Coastal imeweza kupambana na kujiweka katika kundi la timu za daraja la juu katika ligi hiyo msimu huu jambo ambalo ni nadra kuliona kwa timu nyingine ambazo zina bajeti kiduchu.

Inapaswa kuwa mfano bora wa kujifunza kwa timu nyingine ambazo zinapaswa kuepuka kisingizio cha ukata kama sababu ya kuwa wasindikizaji kwenye ligi.

Kinachoifanya Coastal ifanikiwe ni matokeo ya juhudi na utayari wa pamoja wa wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wa timu hiyo ambao wengi wao ni wakazi wa Tanga.

Wachezaji pamoja na bajeti ndogo ya klabu, wanapambana kuisaidia ifanye vizuri wakiamini itakuwa fursa muhimu kwao kujiweka sokoni mara baada ya msimu kumalizika ili wapate malisho ya kijani mahali kwingine.

Ni vigumu kwa timu kumsajili mchezaji ambaye hachezi, hivyo akili yao kwa kiasi kikubwa wameielekeza uwanjani wakiamini hapo ndipo panapoweza kukomboa maisha yao wakiitazama Coastal kama daraja tu la kuvukia katika kutimiza malengo yao.

Lakini pia timu inapofanya vizuri, ndipo wanajua itavutia idadi kubwa ya mashabiki kujitokeza katika mechi zake za nyumbani jambo litakalofanya klabu iingize fedha ambazo zitawezesha kulipa mishahara na stahiki nyingine za wachezaji.

Benchi la ufundi nalo kwa nafasi yake linawaandaa na kuwajenga wachezaji wake kiufundi hadi wameweza kuwa na ubora wa kushindana katika ligi lakini pia linatoa mchango mwingine wa kuwajenga kisaikolojia nyota wake, hali inayowafanya wawe wavumilivu na wenye kiu ya mafanikio katika hali ngumu wanayopitia.

Kwa upande wa uongozi, nao umeonekana kuwa imara na kutoa sapoti kwa timu jambo ambalo limekuwa likiongeza morali na hamasa ya wachezaji ambayo huchangia wapate matokeo mazuri.

Idadi kubwa ya viongozi wa Coastal wamekuwa wakiambatana na timu yao kila inapokuwa na mchezo, iwe uwanja wa nyumbani au ugenini, tofauti na ilivyo kwa timu nyingine.