UCHAMBUZI: Hakimiliki ya Ardhi ni mtaji wa kufuta umasikini
Muktasari:
- Shamba ni miongoni mwa rasilimali ambazo wananchi wengi wanaweza kuipata, kuitumia na kunufaika nayo kwa maendeleo binafsi kwani uchumi wa Tanzania unategemea zaidi kilimo. Lakini, wananchi wengi hawana hati za maeneo wanayoyamiliki au kuyatumia kwa namna moja au nyingine.
Kukosa sifa za kukopesheka ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili Watanzania wengi katika harakati za kupambana na umasikini.
Wengi hushindwa kukopa kutokana na kutokuwa na dhamana dhidi ya mikopo wanayoihitaji ambacho ni kigezo muhimu kabla benki au taasisi ya fedha haijatoa fedha.
Dhamana ambayo mara nyingi huwa ni mali isiyohamishika kama vile kiwanja, shamba au nyumba ndiyo inayohitajika kabla mkopo husika haujatolewa. Kuthibitisha umiliki wa ardhi yaani kiwanja, nyumba au shamba unahitaji kuwa na hati.
Endapo utakuwa na hati unacho kigezo muhimu sana cha mtaji kutoka kwenye taasisi za fedha. Kuipata hati ya eneo lako unahitaji kulipanga, kulipima na kulilipia katika mamlaka inayohusika na umilikishaji wa ardhi.
Hati hutolewa na kamishna wa ardhi ambaye huteuliwa na Rais. Huwa anapatikana katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akiratibu matumizi ya ardhi yote nchini kwa niaba ya Rais mwenye dhamana nayo kwa niaba ya Watanzania.
Kamishna wa ardhi hutoa hati kwa mkataba wa miaka 33 au 66 na 99. Upo umiliki wa aina mbili wa ardhi unaotambulika nchini ukiwamo ule wa hati za Serikali na hati za kimila.
Kuna sifa za kumiliki ardhi nchini. Mtu yeyote ambaye ni Mtanzania, awe mwanamme au mwanamke anaruhusiwa kumiliki ardhi. Kikundi cha raia wa Tanzania walio katika umoja wa kisheria, wabia au washirika wanaweza kumiliki ardhi.
Ifahamike kuwa mtu ambaye si raia wa Tanzania au kikundi cha watu ambao wengi si Watanzania hawana haki ya moja kwa moja ya kumiliki ardhi nchini na kupewa hakimiliki isipokuwa endapo watapewa kama wawekezaji kwa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji ya 1997.
Upo utaratibu wa kuomba hati ya ardhi. Maombi ya kumiliki hufanywa kwa maeneo yaliyopo kwenye miji, manispaa au majiji. Katika sehemu zote zilizotajwa, utaratibu unaanza kwa kujaza fomu maalumu na kuipeleka kwa kamishna wa ardhi.
Iwapo kamishna ataridhia maombi hayo basi atatoa hati ya ahadi (offer) kwa maandishi inayoeleza masharti ambayo mwombaji anapaswa kuyatimiza.
Mwombaji akiyakubali masharti ya hati aliyoomba atapaswa kuilipia na kuendelea kufanya hivyo kwa eneo analolimiliki kwa siku zijazo. Kila kipande cha ardhi kilichopimwa kinapaswa kulipiwa kodi ya ardhi.
Gharama za hati zinazotambulika ni pamoja na malipo ya awali (premium charge) ambazo ni fedha inayotozwa na Serikali katika ardhi iliyopimwa na kuidhinishwa na mkurungenzi wa upimaji na ramani kutokana na thamani iliyoongezeka kwenye ardhi husika.
Ongezeko hilo la thamani ni kama vile kuwepo kwa miundombinu, ardhi kutumika kama mtaji, kurekodiwa katika nyaraka za kiofisi kwa umiliki halali wa mhusika, kuwepo maisha bora kutokana na mpangilio wa kitaalamu wa viwanja na mahitaji muhimu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya 1999, Waziri wa Ardhi ana mamlaka ya kutoza malipo ya awali pindi mmiliki anapopewa hati ya kumiliki ardhi husika. Malipo haya huwezesha upatikanaji wa huduma muhimu za jamii.
Vigezo vinavyozingatiwa kwenye malipo haya ya awali ni kujulikana kwa matumizi ya eneo husika, thamani ya ardhi kwa mujibu wa mauzo, upangishaji, mnada, zabuni na miamala yoyote iliyofanyika kisheria na uendelezaji uliofanywa. Kigezo kingine ni kuwepo kwa bei ya soko la ardhi iliyokadiriwa na mthamini aliyefuzu katika taaluma ya uthamini.
Kupata kiasi cha malipo haya, mambo matatu huzingatiwa nayo ni bei ya ardhi husika iliyoidhinishwa na mthamini mkuu, ukubwa wa kiwanja au shamba na tozo iliyoidhinishwa na waziri wa ardhi.
Kukamilika kwa utaratibu huu kunampa mwananchi haki ya kumiliki hati ya eneo lake. Hati hii, unaweza kuitumia kufanya muamala wa aina yoyote uliopo kisheria hivyo kukuwezesha kupambana na umasikini.
Ardhi yenye hati inakupa fursa ya kuingia ubia na wawekezaji wa kimataifa wanaotaka kuanzisha miradi yao nchini. Wapo watu wengi walionufaika kwa aina hii ya mikataba.
Kwa sasa, takwimu zinaonyesha Watanzania wenye hati ni asilimia tatu pekee ingawa kilimo kinaajiri zaidi ya asilimia 70. Ukiangalia kwa makini utagundua wengi wanashindwa kukuza mtaji kwa kumiliki ardhi isiyo na hati. Usiwe mmoja kati yao kuanzia sasa.
Mwandishi ni mtaalamu wa mipango miji. Anapatikana kwa namba 0714 068 303