Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI: Huu ndiyo umuhimu wa kingatiba ya matende, mabusha

Unajua kwamba mtu anapoonekana na dalili ya kuwa na busha au matende huwa ameishi na vimelea vya ugonjwa huo kwa zaidi ya miaka sita?

Usihisi kuwa unapoumwa na mbu aenezaye magonjwa hayo utapata dalili mapema kama ilivyo kwa ugonjwa wa malaria, la hasha.

Mabusha ni hali ya kujaa maji kwenye mfuko wa korodani. Hali hii hutokea kunapokuwa na mkusanyiko wa maji kati ya tabaka mbili za utando unaozunguka korodani.

Inakadiriwa kuwa karibu asilimia moja ya wanaume wote duniani huathiriwa na tatizo hili.

Kwa hapa nchini, tatizo hili ni limeenea katika maeneo ya mwambao wa pwani hali inayohusishwa na imani tofauti, huku baadhi wakiona mtu kuwa na busha ni aina fulani ya ufahari.

Mojawapo ya dhana iliyozoeleka miongoni mwa watu wa mwambao ni kwamba, mabusha yana uhusiano mkubwa na unywaji wa maji ya madafu.

Lakini, tatizo hili limekuwa likichukuliwa na baadhi ya watu kuwa ni hali ya kudhalilisha ingawa kwa wengine huonekana ni hali ya kuwa ‘mzee wa heshima’ au ‘umwinyi.’

Ifahamike kuwa, tatizo la mabusha halitokei kwa wanaume watu wazima tu, bali hata watoto.

Kwa kawaida mabusha hayana maumivu na wala hayaleti madhara, isipokuwa kama yatapata uambukizi kwa sababu nyingine yeyote ile.

Hali hiyo inasababisha wengi wa waathirika, hasa wa mwambao, kuwa wagumu kutafuta ufumbuzi wa tiba.

Ni vyema kama mtu ana uvimbe wowote kwenye korodani zake, kutafuta msaada wa kitabibu ili kuweza kuondoa uwezekano wa kuwepo kwa magonjwa mengine ya sehemu za siri kama vile saratani ya korodani ambayo wengi hawaitambui.

Wakati Wizara ya Afya ikiwa imejikita kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili kwa miaka kadhaa sasa kupitia mradi wa magonjwa ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele, Mkoa wa Dar es Salaam umetajwa kuongoza kwa maambukizi ya magonjwa hayo kwa asilimia 12 ikilinganishwa na mikoa mingine iliyo chini ya asilimia moja.

Hiyo inaonyesha ni namna gani mkoa huo ulivyo na maambukizi ya hali ya juu na hivyo kuonyesha ni kwa namna gani walio na vimelea kuongezeka zaidi licha ya kuwa kwa sasa hawana dalili.

Ugawaji wa kingatiba za matende na mabusha kwenye mikoa korofi ulianza kutolewa Desemba 15 hadi 20, lakini waliojitokeza kwa ajili ya kumeza dawa hizo ni wachache, ukilinganisha na ukubwa wa tatizo. Hali hiyo inaashiria kuwa wapo wenye vimelea vya ugonjwa huo na hawajaweza kumeza dawa. Awali mpango uliangalia wilaya 185 nchi nzima lakini baadaye iligundulika wilaya 60 hazikuwa na maambukizi.

Katika halmashauri 121 zilizokuwa na maambukizi, baada ya ugawaji kingatiba wilaya 93 zimefanikiwa kutokomeza magonjwa haya na maambukizi kwa sasa yapo chini ya asilimia moja.

Wizara ilitenga kingatiba kwa wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam pekee kuwafikishia kingatiba kupitia hospitali, vituo vya afya, Serikali za mitaa na kwenye kambi maalumu, ambayo ni dozi ya kila mwaka pindi inapotangazwa lakini waliojitokeza ni wachache.

Bila kujitokeza na kupata tiba kwa wakati ni dhahiri kuwa utokomezaji wa vimelea vya ugonjwa huu katika wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine ya ukanda wa Pwani hautakwisha.

Ikumbukwe kuwa sababu za kutokea kwa mabusha hutofautiana kati ya watoto wa kiume na wanaume watu wazima haya ni ya kuyazingatia ili kubaini mapema.

Magonjwa yasiyopewa kipaumbele ni pamoja na matende na mabusha, usubi, trakoma, kichocho, minyoo ya tumbo, homa ya malale, kichaa cha mbwa, tauni, tegu na mengineyo.

Maambukizi ya magonjwa hayo yanatokana na kuenezwa na wadudu kama vile mbu, nzi na konokono kwa hapa nchini udhibiti wa magonjwa hayo unaelekezwa kwenye kinga, tiba, usafi binafsi wa mazingira na udhibiti wa wadudu waenezao magonjwa hayo.

Athari za magonjwa haya yasipotibiwa mapema ni pamoja na saratani ya kibofu cha mkojo na ini, upofu, utumbo kujifunga na dalili za kifafa.

Ikumbukwe kuwa magonjwa haya pia husababisha ulemavu wa kudumu hali inayopunguza uwezo wa wanajamii kushiriki shughuli za maendeleo ya kiuchumi.

Magonjwa haya huathiri pia watoto, hivyo kupunguza mahudhurio yao shuleni. Ni vyema kwa kila mwanajamii kuhakikisha anameza dawa za kingatiba kama inavyoelekezwa na wataalamu wakati wa kampeni husika, kwani dawa hizi aina ya Mectizan, Albendazole, Praziquantel na Zithromax, zimethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) kuwa ni salama na hazina madhara yoyote.

Herieth Makweta ni mwanandishi wa Mwananchi, anapatikana kwa baruapepe; [email protected]