Umaskini na kukosa ajira kunavyoathiri afya ya akili
Kukosa ajira limekuwa janga kwa vijana wa Kitanzania na hii huathiri afya ya akili ya wengi wao, suala la kutoweza kujikimu kimaisha humfanya mtu kudhoofika.
Kipindi mtu anahitimu masomo yake, siku hiyo huambatana na furaha kubwa, maana kama mambo yakienda kama anavyotarajia basi ataweza kutimiza na kuishi maisha ya ndoto yake.
Ndoto hii ikiwa ni kuajiriwa na kuanzisha familia au kuajiriwa na kujenga, zote hizi ni baadhi ya matarajio yaliyomjaa mhitimu.
Lakini nini hutokea pale ndoto hizi zisipotimia? Huku anayepaswa kukuajiri anakwambia jiajiri maana ajira hamna? Nini kinatokea kwa wengi pale wanapojikuta bado wako nyumbani kwa wazazi na hawawezi kujikimu kwa lolote?
Nini kinatokea kwa mtu anayejikuta kwenye janga la umaskini? Hizi ni baadhi ya athari za kukosa ajira na umaskini katika afya ya akili.
Msongo wa mawazo (stress). Watu wanaokosa ajira au kuishi katika hali ya umaskini hukumbana na hali ngumu ya kiuchumi inayosababisha msongo wa mawazo.
Wasiwasi juu ya jinsi ya kukidhi mahitaji ya msingi kama chakula, malazi na mavazi huongezeka na hali inapoendelea kwa mda mrefu inaweza kusababisha madhara makubwa, kama msongo wa mawazo.
Sonona (depression). Sonona ni neno la kisayansi ambalo kwa tafsiri ya kawaida ndiyo tunaita sonona. Huu ni ugonjwa wa akili ambao mtu anaupata baada ya kupitia matatizo fulani na kumuacha kwenye huzuni au kusononeka kwa muda mrefu.
Lakini watu wengi bado hawajui kama hali hiyo ni ugonjwa kama yalivyo maradhi mengine.
Kukosa ajira na kuwa katika hali ya umaskini mara nyingi husababisha watu kujiona hawana thamani au kushindwa. Hii inaweza kusababisha sonona, hali ambayo mtu anajisikia huzuni kali, kukosa matumaini na kutoona sababu ya kuendelea mbele.
Kukosa kujiamini, kukosa kazi na kipato husababisha mtu kukosa kujiamini. Hii ni kwa sababu mtu hujihisi kutoweza kutimiza wajibu wake kifamilia au kijamii.
Hali hii humfanya mtu ajitenge na jamii, hali inayoweza kuongeza matatizo ya afya ya akili.
Matatizo ya kula na kukosa usingizi (insomnia). Wasiwasi na huzuni kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, husababisha matatizo kama kukosa usingizi na mabadiliko katika jinsi mtu anavyokula, kama vile kupoteza hamu ya chakula au kula kupita kiasi.
Hali hizi zikiendelea huweza kusababisha madhara ya kiafya. Matatizo ya mahusiano, umaskini na ukosefu wa kazi huathiri mahusiano ya kifamilia na kijamii.
Migogoro inaweza kuongezeka na hii huchangia matatizo ya afya ya akili, hasa kwa sababu ya kukosa msaada wa kijamii.
Kuongezeka kwa ulevi na matumizi mabaya ya dawa za kulevya. Watu wanaokabiliwa na ukosefu wa ajira na umaskini wako kwenye hatari kubwa ya kujihusisha na ulevi au matumizi mabaya ya dawa za kulevya kama njia ya kukabiliana na msongo wa mawazo.
Hii inaweza kusababisha utegemezi na matatizo mengine ya afya ya akili na mwili. Kuongezeka kwa mawazo ya kujidhuru au kujitoa uhai.
Katika hali mbaya zaidi umaskini na ukosefu wa ajira vinaweza kumfanya mtu kufikiria kujidhuru na hata kujitoa uhai.
Hii hutokana na kujisikia kutoona thamani ya maisha na kukosa matumaini ya kuboresha hali ya maisha.
Ukijikuta katika hali yoyote kati ya hizi, ni muhimu kutafuta msaada kutoka kwa wataalamu wa afya ya akili kama vile wanasaikolojia, washauri au madaktari. Ni muhimu kuimarisha mahusiano ya kijamii na kuwa karibu na marafiki na familia wanaotoa msaada wa kisaikolojia.
Kushiriki katika vikundi vya usaidizi (group therapy) vikundi hivi husaidia watu kueleza hisia zao na kupata mbinu za kukabiliana na hali ngumu.
Kujiunga na programu za maendeleo kama vile elimu na mafunzo zinaweza kuongeza ujuzi na kuongeza nafasi za kupata ajira.
Pia kujihusisha na masuala ya imani na sala husaidia kufanya mambo yasonge mbele na kukutia moyo.
Kwa jumla, umaskini na kukosa ajira vinaweza kuwa na athari kubwa kwenye afya ya akili, lakini kwa msaada wa kisaikolojia na jamii, inawezekana kukabiliana na hali hii na kuboresha hali ya kiakili na kiuchumi.