Viongozi wanaokiuka maadili wawajibishwe

Muktasari:

  • Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya viongozi wa umma wamebainika kutumia si tu misuli na ubabe dhidi ya wananchi, bali hata vitisho na lugha ya matusi dhidi ya wananchi.

Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya viongozi wa umma wamebainika kutumia si tu misuli na ubabe dhidi ya wananchi, bali hata vitisho na lugha ya matusi dhidi ya wananchi.

Kwa mtazamo wa kawaida, vitendo hivyo vya viongozi, wakiwamo wakuu wa wilaya ni dalili za kulegalega kwa maadili ya viongozi wa umma nchini.

Imekuwa ni jambo la kawaida kuwaona viongozi wa umma wakionyesha ubabe na hata kumwaga matusi ya nguoni hadharani dhidi ya wananchi kinyume na maadili ya kazi na utu wa Mtanzania.

Japo baadhi ya viongozi waliohusika kwenye matukio hayo wamejitokeza na kuomba radhi na wengine wanasisitiza walichofanya ili kionekane kama kilikuwa sahihi, bado kauli na vitendo vyao havikubaliki ndani ya jamii kimaadili.

Hatutaki kuhukumu, lakini tabia za aina hii – kama kutukana wananchi, kuwapiga, kuwashambulia katika biashara zao na majumbani inaonekana kuwa ni mazoea kwa baadhi ya viongozi wa umma na inabidi ufanyike utaratibu wa kuikomesha.

Kama walivyoeleza baadhi ya wachambuzi, nasi tunakubaliana na mtazamo kwamba tabia na mazoea mabaya ya uongozi wa umma kukiuka maadili inachangiwa na wahusika kutokemewa na hivyo kuonekana kama vile wametumwa kufanya hivyo.

Hatujaona kiongozi wa ngazi ya juu akikemea vitendo vya namna hiyo au pengine hata kuchukua hatua. Au hata pale hatua zinapochukuliwa inakuwa kimyakimya kiasi kwamba inakuwa vigumu hatua hizo kusaidia viongozi na watendaji wengine kujifunza.

Mambo haya kwa hakika si tu yanashusha hadhi na haiba ya viongozi na Serikali pekee, bali pia yanaondoa sura ya utawala bora.

Ajabu ni kwamba vitendo vya namna hiyo vinafanyika huku watendaji wote wakiwa wanaapa na kusaini maadili ya utumishi wa umma ambayo yanakataza masuala ya namna hiyo.

Isiwe kama fasheni kwa viongozi baada ya kuapishwa wawe wanasaini kiapo cha maadili na kuendelea kutenda kinyume chake, bali ifike hatua Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma inayosimamia kiapo hicho isiishie tu kuangalia mali walizojaza viongozi, bali iangalie hata mienendo yao ya kila siku katika nafasi zao za utumishi au uongozi.

Kwa sababu baadhi ya viongozi wanaofanya vitendo hivyo ni makada au wanatokana na chama tawala na jumuiya zake, tunadhani CCM inao wajibu wa kusimamia na kudhibiti tabia na mienendo yao.

Kwa wale viongozi wa nafasi za kuteuliwa, ni muhimu mamlaka zao za uteuzi ziwe zinachukua hatua mara moja pale makosa ya ubabe, vitisho na matusi yanapofanyika ili kutoa funzo kwa wengine.

Vyombo vya dola vinavyosimamia utii wa sheria navyo vinapaswa kuchukua hatua stahiki, hasa pale makosa yanayofanyika wanapokuwa na sura ya jinai.

Mfano kutoa matusi hadharani ni kosa la jinai linalotakiwa kushughulikiwa na vyombo vya dola bila kujali nafasi, ushawishi wala cheo cha mkosaji, lakini matukio ya namna hiyo hata yakiripotiwa, si rahisi yakafunguliwa jalada wala kesi kufunguliwa.

Tulifarijika hivi karibuni baada ya kusikia kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba atakuwa na kipimo cha mabega na hatawavumilia viongozi au watendaji wanaotunisha mabega yao badala ya kuwa watumishi wa umma.

Kauli hiyo ya Rais ishuke kwa wengine walio chini yake, nao wawasimamie wanaowaongoza ili masuala ya ubabe na kutunishiana mabega yageuke kuwa historia.