Wanawake, fursa bado ipo msiipoteze
Muktasari:
MJADALA wa kupata Katiba Mpya ulipoanza wengi wetu tulitarajia kujitokeza madai ya wanawake, kinyume chake wanawake wamegawanyika kwa misingi ya itikadi ya vyama, wameweka kando ajenda yao katika kupigania haki na maslahiyao.
MJADALA wa kupata Katiba Mpya ulipoanza wengi wetu tulitarajia kujitokeza madai ya wanawake, kinyume chake wanawake wamegawanyika kwa misingi ya itikadi ya vyama, wameweka kando ajenda yao katika kupigania haki na maslahiyao.
Tumeona namna walivyokubali kutumika kisiasa kwa ajili ya kufurahisha makundi maslahi, ingawa wapo baadhi yao waliosimama kidete kutetea, kupigania na wakati mwingine hata kutofautiana na viongozi wao katika vyama vya siasa au katika asasi za kiraia.
Historia ya mapambano ya wanawake inakwenda mbali zaidi, wakati wa kutafuta uhuru ni wanawake waliojitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya vyama vya ukombozi, wengine wakasimama kwenye majukwaa kupaza sauti za ukombozi.
Bado Dunia inawakumbuka wanawake shupavu, hodari na jasiri akina Winnie Mandela, Margareth Thatche, Benazir Butho, Hillary Clinton, Bibi Titi Mohamed, Dk Ruth Meena, Getrude Mongela, Anna Abdallah, Leila Sheikh, Barbara Mikulowski, Hanan Ashrawi, Bibi Indira Gandi, Asha Bakari, Margareth Sanger, Amina Salum Ali, Naila Majid Jidawi, Marry Robinson, Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf na wengineo.
Wanawake hawa kila moja na haiba yake, uwezo na historia yake katika mapambano ya kutafuta haki na maslahi ya wanawake bado wanabaki kuwa kielelezo cha ushupavu ambao ulipaswa kuonekana kwenye mchakato wa maoni ya Katiba kwa upande wa wanawake ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakieleza malalamiko yako kuhusu mambo ya kisiasa, kijamii, kiuchumi kuwa wameachwa nyuma chini ya hoja ya mfumo dume.
Mtakubaliana nami kwamba kila kwenye mashaka, matatizo, vita, maafa,ukatili, uonevu, ghasia, ni wanawake na watoto ndio wanakumbwa na mashaka hayo, hata wakati ambapo maoni ya Katiba yamepamba moto ni wanawake waliokuwa waathirika zaidi wa misimamo isiyokuwa ya kidemokrasia ya baadhi ya vyama vya siasa kuwaelekeza wanachama na wafuasi wao kutoa maoni ambayo yanatakiwa na chama husika.
Pamoja na ukweli kwamba wapo baadhi ya wanaume waliokubali kuburuzwa, lakini sehemu kubwa ni wanawake. Bila ya shaka, watakuwa wamejifunza na watajirekebisha kupitia mabaraza ya Katiba.
Katiba yetu ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina vifungu ambavyo vinawahakikishia wanawake haki zao kwenye ulingo wa siasa, lakini licha ya hilo na mafanikio mengine ambayo yamepatikana bado wanawake wanahitaji kujipanga, kuwa na mkakati wa pamoja katika kutetea maslahi yao kupitia Katiba Mpya, fursa hii ikitoweka kwa maana ya muda wake kupita, haitapatikana kirahis.
Wanawake wanawajibu wa kukumbuka madhila wanayopata, wasikubali kufanya wema wa mshumaa unateketea unaangazia wengine. Madai ya usawa katika jamii yanayotolewa na wanawake nayachukulia kama ni mapambano ambayo siku zote hakuna mapambano yasiyokuwa na mafanikio ijapokuwa hakuna mapambano yasiyokuwa na wasaliti, tumeupata ushahidi wa kinyamwezi kwenye mchakato wa utoaji wa maoni kwa upande wa wanawake.
Wale waliokuwa na nguvu na vyeo vya kisiasa baadhi yao wameyumba, wamekubali kuyumbishwa na upepo wa wanaume wachache, bila shaka hili ni funzo kwa jamii nzima ya wanawake wanaharakati. Tukiwa kwenye matayarisho ya mabaraza ya Katiba ni wakati muafaka wanawake kujitathmini wao wenyewe, je, wamefikia au watafikia pale walipotaka kwenda au wajiulize ni wapi hasa wanakwenda au wanajipeleka wenyewe?
Je, wanataka kufikia pale mcheza tennis maarufu aliyesumbua sana akili za viongozi wa mchezo huo kwamba ashindane na wanawake au wanaume? Huyo ni "Rennee Rich" ambaye kimaumbile ya misuli na haiba alikuwa mwanaume, lakini baadaye aliweza kubadilisha jinsia na hata jina na akawa mwanamke.
Je, haionekani kuwa kupoteza fursa ya utoaji maoni kwenye Tume ya Katiba kulikofanywa na wanawake waliojiegemeza na kujitia kwapani kwa wanasiasa na hata baadhi ya wanaharakati kumewapotezea muda na pengine wamepanda jahazi lililopoteza mwelekeo wakipelekwa katika bahari kuu yenye papa na nyangumi?
Wanawake wanasiasa waliojitokeza kusema hadharani mawazo yao bila woga ni Naibu Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Thuwaiba Edington Kisasi, yeye alisema ni muumini wa Muungano, ingawa hakusema wa muundo gani.
Baada ya hapo, akaorodhesha kero tele za Muungano ambazo haridhiki nazo. Na yeye akamalizia kuwa anataka mafuta na gesi asilia, forodha, ushuru na kodi ya mapato, bandari, elimu ya juu na takwimu na leseni za viwanda yaondolewe kwenye Muungano.
Maoni haya ni sawa na yale yaliyowahi kutolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Amani (CCM), Fatma Mbarouk Said wakati walipokutana na Tume ya Katiba kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Fatma alipendekeza mamlaka kamili ya Zanzibar kitaifa na kimataifa. Mwakilishi mwingine wa viti maalumu (CCM), Asha Bakar Makame yeye hakuficha hisia zake katika kila anachokiamini.
Hawakuwa wanasiasa viongozi kwa upande wa Zanzibar tu bali hata huko Tanzania Bara, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya alitaka muundo wa Muungano ubadilishwe na kuwa wa Serikali tatu, badala ya uliopo sasa aliosema una kasoro nyingi.
Moja ya kasoro hiyo ni Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuruhusiwa kuingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , huku wabunge wa Bara wakiwa hawana uwakilishi katika Baraza la Wawakilishi.
“Mwenyekiti, tuwe na Serikali tatu katika Muungano, vinginevyo kila mmoja abaki na chake," alisema Mbunge Ester Bulaya katika maoni yake kwa Tume ya Jaji Warioba.
Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo naye alitaka muundo wa muungano uwe wa Serikali tatu pamoja na kuruhusiwa kwa mgombea binafsi katika nafasi mbalimbali. Alisema kuwa mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wasitokane na wabunge kwa sababu hawataweza kufanya kazi kwa ufanisi na ni mgongano wa kimasilahi.
Licha ya udhaifu waliouonesha wakati wa awamu ya kwanza ya ukusanyaji maoni, ni imani yangu kuwa wanawake wataungana pamoja katika awamu ya mabaraza ya Katiba na kutoa mawazo ambayo yanatokana na wao wenyewe na sio yale ya kupewa na wanasiasa.
Hivyo kwa vigezo kadhaa wa kadhaa mjadala juu ya mabadiliko ya mfumo wa muundo Muungano ndio kiini cha mawazo ya waliowengi kule Zanzibar na kwa msingi huu hapana budi makundi maalumu Zanzibar waitumie fursa hii kwa ujasiri mkubwa, umakini na zaidi ya yote kuweka mbele maslahi ya Zanzibar na sio maslahi binafsi ya makundi au kiitikadi.
Ni wazi wapo wataosukuma ajenda zao katika mjadala huu kwa maslahi yao binafsi hasa ya kisiasa hata kuweza kupotosha mambo, waiangamize hoja ya wanamageuzi ili itoweke kabisa ili wao wafaidike na maslahi binafsi tena ya muda mfupi bila kujali mustakbali wa vizazi vijavyo.
Mara zote ajizi ni nyumba ya njaa, tusifanye ajizi kwenye mambo ya nchi kama ambavyo tulivyowaona mashabiki wa uhafidhina wa kale walivyojaribu kufanya katika utetezi wa hoja dhaifu ya kisingizio cha Sultan, kukiuka amri ya chama wakati kumbe wenyewe rohoni wanagugumia kwa uzalendo wa Kizanzibari.
Bila shaka makundi maalumu yataitumia vema fursa hii kwa maslahi ya Zanzibar badala ya kuichezea maana ipo siku wataitamani fursa kama hii, lakini muda utakuwa umewapita kwani kila jambo na wakati wake.
Msanii Mrisho Mpoto katika wimbo wake wa heri kujenga daraja kuliko ukuta, anasema "Mjomba tazama kule ile ni shule, na yule anayegawa visheti ni mwalimu na wengine watauza kesho, wamepeana zamu ya kuyanusuru maisha yao japo haipo kwenye mtalaa wa shule, tukiona inasaidia tuipitishe wala siwachongei mkiwafukuza wafukuzeni wote sehemu ya ubeti wa wimbo wa Mjomba Mrisho Mpoto.