Ya Engonga yaweza kutokea kwenye familia yako
Juma lililopita karibu habari kubwa mitandaoni ilimhusu Bartazary Engonga, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Upelelezi wa Fedha Equatorial Guinea.
Umaarufu wa Engonga umekuja kufuatia kashfa iliyomkumba kigogo huyo wa Serikali baada ya kukutwa na video 400 ambazo zinamuonesha akishiriki ngono na wanawake mbalimbali.
Kilichoibua msisimko kwa watu wengi kufuatilia sakata hilo lililoibua mjadala barani Afrika, ni namna alivyofanikiwa kuwashawishi wake wa vigogo wenzie na kushiriki nao ngono huku akiwarekodi.
Kesi ya Engonga imekuwa kubwa zaidi kutokana na video hizo kumuonesha kuwa kuna wakati alifanya vitendo hivyo ofisini kwake, hii ina maana kwamba alitumia ofisi ya umma kufanya mambo ya hovyo.
Hazikuwa video nzuri hata kidogo, lakini kwa aliyepata fursa ya kuziona hakika atakubaliana na mimi kwamba kuna vitu havipo sawa, hivyo wakati tunaendelea kushabikia hilo lililotokea kwa Engonga, kuna maswali tunapaswa kujiuliza.
Miongoni mwa maswali ninayojiuliza, kwa nini alifanya vile, kwa nini alijirekodi, kwanini inaonekana hata wanawake aliokuwa nao walikuwa wanatambua kuwa wanarekodiwa na kwa nini alitunza video hizo kwenye simu yake.
Hadi sasa sijapata majibu ya maswali yangu na hakuna mwenye majibu sahihi zaidi ya yeye mwenyewe au wanawake wanaoonekana kwenye video hizo.
Ninachokiona hapa kuna changamoto kwenye malezi, eneo hili ndilo tunapaswa kuweka nguvu ili siku moja tusije kuwa na akina Engonga kwenye familia zetu.
Nasema malezi kwa sababu kwa umri wa mwanamume huyu unaokadiriwa kuwa zaidi ya miaka 50, kufanya vitendo vya aina hii ni wazi kwamba hana msingi mzuri katika malezi na makuzi yake, ndiyo maana alidiriki kufanya hayo aliyoyafanya.
Hapa naona lipo la kujifunza, hasa kwa wazazi, unamlea mtoto wako kwa namna gani, unamuwekea misingi gani itakayomfanya kwanza ajipende, ajithamini na atambue thamani yake.
Kwa kilichofanywa na mwanamume yule, ni wazi kwamba hata yeye mwenyewe hajithamini na wala hajali kuhusu utu wa wengine. Pia ni muhimu kuwalea watoto katika misingi ya kiimani, mtoto akiwa na hofu ya Mungu kuna vitu hawezi kufanya.
Hata akikutana na mazingira yanayomsukuma kufanya kitu cha hovyo, hofu ya Mungu iliyo ndani yake itamfanya asifanye na ndiyo maana nasisitiza ni muhimu watoto wakashibishwa mafunzo ya kiimani.
Wapo wanaosema ni changamoto ya afya ya akili au masuala ya ushirikina yanaweza kuchochea vitendo vya aina hii, sipangani na mitazamo hiyo, lakini narudi pale pale, tukiweka msingi mzuri kwenye malezi kuna mengi tunaweza kuyaepusha kwa vizazi vyetu.
Sasa wewe mama au baba wakati unaangalia na kupongeza au kusikitishwa na kilichofanywa na Engonga, hakikisha unasimama vyema kwenye nafasi yako ya malezi ili kuiepusha jamii kuwa na watu wengi wenye vitendo vya hovyo.
Na hili halipo upande wa wanaume pekee, lawama zinaenda pia kwa wale wanawake ambao wanaonekana wakifanya ngono na mwanamume huyo, kati yao wakiwemo wake za watu. Mwanamke aliyelelewa vyema hawezi kushawishika kirahisi kufanya mambo ambayo hayataishia kuchafua taswira yake, bali mume wake na familia yake kwa jumla.
Wito wangu katika hili turudi kwenye msingi wa malezi ambayo yanamtengeneza mtoto kuwa mtu mwenye maadili na kutegemewa kwenye jamii, awe mwenye heshima, ajali utu wa wengine na kubwa na muhimu zaidi ni hofu ya Mungu.
Elizabeth ni mhariri wa Jarida la Familia, anapatikana kwa [email protected]