Ya kuzingatia tukiuaga mwezi wa Ramadhani

Wakati tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu tukielekea kumaliza salama faradhi ya swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, hatuna budi kuyazingatia mambo matatu muhimu yanayozikamilisha swaumu zetu ipasavyo na kupata fadhila zake nayo ni: Zakaatul-Fitri, Eidil Fitri na Swaumu ya Sitta Shawaali. Makala yetu inakusudia kuyadadavua mambo matatu hayo, In-Shaa-Allaah! 

1. Zakaatul-Fitri

Zaka hii maarufu huitwa Zakaatul-Fitri (Zaka ya Kufuturu) kutokana na kumalizika kwa funga ya Ramadhani kwa ajili ya kutakasa funga ya Muislamu kutokana na kutoa maneno machafu na ya upuuzi alipokuwa katika ibada ya funga, kwa kulisha masikini chakula, ili nao wapate chakula kizuri siku ya Eid na ndiyo maana hutolewa kabla ya kuswali swala ya Eidil-Fitr, kama ilivyokuja katika hadithi ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani)  kutoka Ibn Abbas (Allaah Amridhiye) kwamba: “Mtume wa Allaah (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amefaradhisha Zakaatul-Fitri kuwa ni takaso kwa mwenye kufunga kutokana na maneno ya upuuzi na machafu na kulisha masikini. Atakayeitoa kabla ya swala (ya Eid) basi hiyo ni zaka iliyokubaliwa na atakayeitoa baada ya swala basi hiyo ni miongoni mwa swadaka” (Abuu Daawuwd kwa isnaad iliyo nzuri).

Utoaji wa Zakatul Fitri ulioelezwa ndiyo kusudio la kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kama tunavyosoma katika Quran Tukufu, Sura ya 87 (Surat Al-A-alaa), Aya ya 14 na 15 kuwa: "Hakika amefaulu ambaye amejitakasa.Na akakumbuka jina la Mola wake Mlezi na akaswali."

Wakati wa kutoa Zakatrul Fitri ni kuanzia Magharibi ya siku ya mwisho ya Ramadhani hadi asubuhi kabla ya swala ya Eidil-Fitr. Inaweza pia kutolewa kabla ya muda huo kwa siku mbili tatu. Mtoto atakayezaliwa siku hiyo kabla ya kuzama kwa jua imewajibika kumtolea Zakaatul-Fitri.

Hadithi kutoka kwa Ibn Umar (Allaah Amridhiye) inaeleza anayewajibika kutoa Zakatul Fitri na aina ya kitu cha kutoa kuwa: "Mtume wa Allaah (Allaah Amrehemu na ampe Amani) ameifanya Zakaatul-Fitri ni faradhi (lazima) kwa mtumwa na aliye huru, mwanamume na mwanamke, mdogo na mkubwa miongoni mwa Waislamu kwa kutoa pishi moja (kilo mbili na nusu) ya tende kavu au pishi moja (kilo mbili na nusu) ya shayiri, na akaamrisha kwamba itolewe kabla ya watu kwenda kuswali (Swalaatul-Eid)" (hadithi hii inapatikana katika kitabu cha Hadithi za Mtume Muhammad -Allaah Amrehemu na Ampe Amani kiitwacho Sahih Al-Bukhary). 

Kimsingi ni kuwa kinachotolewa ni chakula kinachotumika na watu wa eneo husika kama tunavyoona katika hadithi kutoka kwa Abuu Saidil-Khudriy (Allaah Amridhiye) akisema: "Tulikuwa tukitoa zama za Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) pishi moja ya chakula, au pishi ya shayiri au pishi ya tende au pishi ya zabibu au pishi ya aqit" (mtindi mkavu – chakula walichokuwa wakikitumika zama hizo) (hadithi hii inapatikana katika vitabu vya Hadithi za Mtume Muhammad -Allaah Amrehemu na Ampe Amani viitwavyo Sahih Al-Bukhary na Sahih Muslim).

2. Eid Al-Fitri

Eidil Fitri ni sikukuu maarufu yenye maana ya sikukuu ya kufuturu na imeitwa hivyo  kutokana na Waislamu kumaliza swaumu ya Ramadhani na mojawapo ya sikukuu za Waislamu ambapo haifai kwa mtu kufunga siku hiyo, bali ni siku ya kula, kunywa, kufurahi na kusherehekea kwa namna inayoruhusiwa na Sharia ya Dini ya Uislamu.

Ni sunna siku ya Eid kuoga kabla ya kutoka kwenda kuswali, kujipamba na kuvaa nguo nzuri na manukato mazuri. Ni Sunna pia kula tende kabla ya kutoka kwenda kuswali na aliyekosa tende anaweza kula chochote kile kilicho halali.

Ni sunna pia kuleta Takbira kwa kusema: Allaahu Akbar Allaahu Akbar, Laa Ilaaha Illa Allaah, Wa-Allaahu Akbar Allaahu Akbar wa Lillaahil Hamd.

Ni vyema Siku ya Eid kupongezana kwa ajili ya kudhihirisha mapenzi na undugu na hususan kwa maneno waliyokuwa wakiambiana maswahaba wanapokutana siku ya Eid, nayo ni: 'Tuqubbila Minnaa wa Minka’ au ‘Taqabbala Allaahu Minnaa wa Minkum’ (Allaah Atutakabaliye).

3. Funga ya Sitta Shawwaal

Hii ni swaumu inayofuatia moja kwa moja baada ya mwezi wa Ramadhani na anaweza mtu kuanza siku ya pili baada ya Eidil-Fitri.  

Kufunga siku sita ndani ya mwezi Shawwaal (Mfungo Mosi) ni sunnah yenye fadhila kuu, kwani thawabu zake ni sawa na thawabu za kufunga mwaka mzima kwa dalili kauli ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kuwa: “Atakayefunga Ramadhani, kisha akafuatiliza na siku sita za mwezi wa Shawwaal itakuwa kama ni funga ya mwaka.” (hadithi hii inapatikana katika kitabu cha Hadithi za Mtume Muhammad -Allaah Amrehemu na Ampe Amani -  kiitwacho Sahih Muslim).

Wanazuoni wa Kiislamu  wameelezea sababu ya mtu kulipwa thawabu za mwaka mzima kwa atakayefunga Ramadhani na siku sita hizo za Shawwaal kwamba: Jambo zuri hulipwa ujira mara kumi, kwa hiyo mtu akifunga siku 30 za Ramadhani atapata ujira mara kumi; nazo zitakuwa 300, ukijumlisha na siku sita za Shawwaal ambazo zikilipwa mara kumi, huwa 60 hivyo kupata 360, mtu atapata hesabu ya mwaka mzima.

Kwa mantiki hii, kuna umuhimu na ubora mkubwa wa kuifunga swaumu hii ya Sitta Shawaal.

Tunamuomba Allaah Mtukufu atukubalie ibada zetu na atuwekee sawa upungufu wetu na yeye ni muweza wa hayo. 

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).

Simu: 0713603050/075460305