Kaburu: Ebu subirini muone

Aliyewahi kuwa makamu mwenyekiti wa klabu ya Simba, Geodfrey Nyange 'Kaburu'.

WAMEFYEKWA. Ndivyo ilivyo baada ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba, juzi Jumapili kutoa orodha ya majina 14 ya wagombea waliopitishwa katika mchujo wa kwanza wa usajili, huku vigogo Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Idd Kajuna wakifyekwa.

Kaburu, makamu wa rais wa klabu hiyo enzi za Evans Aveva aliomba nafasi ya uenyekiti, lakini jina lake halikurudi kama Kajuna aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa utawala wa Aveva, aliyefyekwa katika nafasi ua ujumbe kwa madai ya kutokidhi vigezo.

Kamati ya uchaguzi imeeleza baadhi ya sababu ya majina ya wagombea wengine kushindwa kurudi, kujiondoa katika mchakato wa uchaguzi, fomu kutojazwa kikamilifu, usahihi na haiba na kutangaza majina 14 ya waliopenya akiwamo watatu wa nafasi ya uenyekiti na 11 ya ujumbe.

Waliopenya kwenye mchujo huo, Moses Kaluwa na Murtaza Mangungu anayetetea kiti wote waliomba nafasi ya uenyekiti, huku wanaoomba ujumbe wa bodi ya wakurugenzi wakiwa ni 12 wakiwamo Seif Muba, Seleman Harubu, Iddi Kitete, Issa Masoud na Abubakar Zebo.

Wengine ni Abdallah Mgomba, Elisony Mweladzi, Rashid Mashaka, Rodney Chiduo, Aziz Mohamed, Asha Baraka na Pendo Mapugilo, huku kamati ikitoa nafasi kwa mwanachama kuweka pingamizi la maandishi akiambatanisha na vielelezo, ushahidi wa kuunga mkono pingamizi lake.


msikie Kaburu

Mwanaspoti lilimtafuta Kaburu kutaka kujua maoni yake baada ya jina kutorudi naye alisema ameona orodha ya majina, lakini anatafakari kwanza na kushauriana na watu wake wa karibu kama akate rufaa au apotezee.

“Nitaenda kukaa na washauri wangu kujadiliana kama ambavyo ilikuwa hapo awali wakati nakwenda kuchukua fomu nikiamini ninakidhi vigezo vya kamati ilivyovihitaji,” alisema Kaburu na kuongeza;

“Baada ya kushauriana kwa kina na washauri wangu hapo nitakuja na maamuzi kama nitakwenda kukata rufaa au nitaacha tu waliopita kwenye mchakato waendelee.”

Uchaguzi Mkuu wa Simba utafanyika Januari 29 na baadhi ya wajumbe pamoja na Mangungu watatakiwa kutetea nafasi zao.