Ni kufa na kupona Simba vs Ahly

Muktasari:

  • Uwanja wa Benjamin Mkapa leo utawaka moto wakati mabingwa wa soka wa Afrika, Al Ahly watakapokuwa wageni wa Simba, ambao kwa sasa wako moto baada ya kushinda mechi yake ya kwanza ugenini dhidi ya timu ngumu ya AS Vita.

Dar es Salaam. Uwanja wa Benjamin Mkapa leo utawaka moto wakati mabingwa wa soka wa Afrika, Al Ahly watakapokuwa wageni wa Simba, ambao kwa sasa wako moto baada ya kushinda mechi yake ya kwanza ugenini dhidi ya timu ngumu ya AS Vita.
Simba wameipa mechi hiyo jina la "Total War:Point of No Return (vita kamili, nyuma mwiko)" kuonyesha umuhimu wa ushindi leo baada ya kampeni ya kwanza ya "War in Dar" kushuhudia vigogo hao wa soka nchini wakiisambaratisha Platnum ya Zimbabwe kwa mabao 4-0 na kugeuza ushindi wa kwanza wa bao 1-0 jijini Harare na hivyo kufuzu kucheza hatua ya makundi.
Huku kila timu ikiwa na pointi tatu mkononi, mchezo wa leo wa raundi ya pili ya Kundi A unatarajiwa kuwa wa "kufa na kupona" kama vyombo vya habari vya Misri vinavyouelezea.
"Timu ya Tanzania itakuwa mwenyeji wa vigogo wa Cairo kwenye Uwanja wa Taifa katika mechi ya kufa na kupona kwa pande zote. Timu zote zinawania kuendeleza mwanzo mzuri katika hatua ya makundi ya mashindano hayo makubwa," imeandika tovuti ya Ahramonline.com ya Misri.
"Ikicheza ugenini, mpango wa Ahly hautakuwa rahisi, hasa baada ya kuwaona wenyeji wao wakiwashinda wapinzani wagumu Vita ya Congo DR kwa bao 1-0 ugenini katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi wiki iliyopita."
Ugumu wa mechi ya leo pia umeonyeshwa na kocha raia wa Afrika Kusini anayeifundisha klabu hiyo, Pitso Mosimane, ambaye jana alionyesha ufahamu mkubwa wa mchezo wa Simba na baadhi ya wachezaji wake kama Luis Miquisson, Cloutus Chama na Meddie Kagere, lakini akasema mpango wao mwaka huu ni kujihakikishia mapema tiketi ya kusonga mbele tofauti na mwaka jana.
"Safari hii tunaangalia hatua ya makundi kwa mtazamo tofauti kwa kuwa tunataka kujihakikishia kufuzu mapema, tofauti na msimu uliopita wakati tulipoona timu ikifuzu katika mechi ya mwisho baada ya kuizidi Al-Hilal ya Sudan," alisema Mosimane katika mkutano na waandishi wa habari jana Jumatatu jijini Dar es Salaam.
“Tumejikita katika kuujua mchezo wa Simba na hatuangalia yaliyopita.
"Simba ni timu nzuri, lakini tumekuja hapa kushinda tu na tunaamini kuwa tunakutana na mpinzani mgumu na ambaye ana umaarufu mkubwa nyumbani.
"Niliisoma Simba, ina wachezaji wazuri. Itakuwa mechi kubwa dhidi ya timu ngumu ambayo imepangwa vizuri, lakini tunataka matokeo mazuri kuhakikisha tunafuzu mapema."
Mosimane alisema anamjua vizuri Miquisson kwa kuwa ndiye aliyemchukua kutoka Msumbiji, na kwamba Chama, ambaye alimtaja kwa namba yake ya mgongozi (7) ni kiungo mzuri, huku akisema Kagere, ambaye pia alimtaja kwa namba ya mgongoni (14), ni mchezaji mzoefu anayefunga magoli.
Alisema ameiona Simba kuwa ni timu inayofurahia kucheza na inacheza kwa ajili ya mashabiki wake, akisema timu kama hiyo ikipamba moto ni vigumu kuizuia.
Mosimane pia alisema klabu yake, ambayo imeshatwaa ubingwa wa Afrika mara tisa, haina mpango maalum wa kukabiliana na hali ya hewa, lakini akasema mabadiliko yoyote ya kiufundi yatakayofanyika, yatakuwa ni kwa ajili ya kuishinda Simba tu.
Ahly, klabu yenye mafanikio kuliko zote duniani, leo itamkosa beki wake wa kushoto, Ali Maaloul, winga Taher Mohamed Taher, na mshambuliaji Salah Mohsen ambao ni majeruhi.
Lakini beki anayejulikana kuwa na ufanisi mkubwa, Ayman Ashraf ameruhusiwa na madaktari kucheza mechi ya leo iwapo atapangwa baada ya kupona majeraha ya misuli, wakati mshambuliaji Marwan Mohsen anaweza kupangwa baada ya kurejea mazoezini.
"Ahly imeathiriwa vibaya na mechi ngumu za Klabu Bingwa ya Dunia, na hiyo ndiyo sababu kubwa ya majeraha ya hivi karibuni, kwa kuwa tulicheza mechi tatu ndani ya siku tisa tu. Tutanufaika na uzoefu tulioupata wakati wa michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia," alisema Mosimane, ambaye aliiongoza klabu hiyo kushika nafasi ya tatu.
Ahly, kama zilivyo timu nyingine za Arabuni, ni timu yenye wachezaji wajanja hasa wanapopokonya mpira kwa kuwa hubadili upepo haraka na kulifikia lango la wapinzani katika muda mfupi, hali ambayo huyumbisha ngome ya wapinzani.
Wanaposhambulia, wachezaji wasio na mpira ni wajanja katika kutafuta nafasi, hali ambayo huchanganya wachezaji wa timu pinzani, na ni wazuri kufunga kwa mipira ya krosi na adhabu.
Kwa wenyeji, Simba inatarajiwa kuendeleza ubabe wake dhidi ya timu za Misri zinapocheza nyumbani. Ilishawahi kuishinda Ahly na Zamalek na hivi sasa iko katika ari kubwa ya kuwazima vigogo hao wa Afrika.
Kocha Didier Gomes Da Rosa ameonyesha kuwa na uhakika kwa wachezaji wake kuonyesha kiwango cha juu dhidi ya mabingwa hao watetezi.
"Nimewaambia wachezaji wangu kuburudisha wakati wakicheza na Ahly na kufanya kila wawezalo katika mechi," alisema Da Rosa alipohojiwa na kituo cha televisheni cha ON Sport TV Jumamosi.
"Nategemea kuwa idadi kubwa ya mashabiki itakuwa jukwaani, kwa kuwa itakuwa mechi kubwa."
Simba imejiimarisha katika safu ya kiungo na ushambuliaji baada ya kufuzu kucheza hatua ya makundi, ikimuongeza Perfect Chikwenda katika ushambulaiji na Thadeo Lwanga ambaye ameonyesha uwezo mkubwa wa kusoma mchezo na kutawala kiungo, huku Bernard Morrison akifufua makali yake baada ya kukaa nje kwa muda.