11 wapenya mchujo wa mwisho Uchaguzi Mkuu TFF
Muktasari:
- Kwa mujibu wa kalenda ya Uchaguzi Mkuu wa TFF, muda wa kampeni ni kuanzia Agosti 9, 2025 hadi Agosti 15, 2025.
Wagombea 11 wamepita katika kiunzi cha mwisho cha Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kesho wataanza rasmi kampeni za kuomba ridhaa.
Katika orodha ya majina iliyochapishwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF leo, Ijumaa Agosti 8, 2025, Mgombea wa nafasi ya Urais ni mmoja na nafasi za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni 10.
Mgombea pekee wa nafasi ya Urais ni Wallace Karia lakini ushindani unaonekana utakuwa katika kanda tatu ambazo zina wagombea zaidi ya mmoja wa nafasi za Ujumbe wa Kamati za Utendaji.
Wagombea waliopitishwa kwa kanda namba moja ni Lameck Nyambaya na Hosseah Lugano na kanda namba tatu ina wagombea watatu ambao ni James Mhagama, Evance Mgeusa na Cyprian Kuyava.
Kanda namba tano ina wagombea wawili ambao ni Vedastus Lufano na Salum Kulunge. Kanda tatu zina wagombea wa nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambao hawana washindani.
Kanda hizo ni kanda namba mbili ambayo mgombea pekee ni Khalid Mohamed na kanda namba nne ambayo mgombea aliyepitishwa ni Mohamed Aden. Kanda namba sita nayo ina mgombea mmoja tu ambaye ni Issa Bukuku.
Wagombea hao kesho wataanza kampeni ambazo zimepangwa kumalizika Agosti 15, 2025 na Uchaguzi Mkuu utafanyika Agosti 16, 2025 jijini Tanga.