Arsenal, Chelsea mechi ya uamuzi
Muktasari:
- Timu hizo zimekutapa mara 64 katika EPL ambapo Arsenal imepata ushindi mara 26 huku Chelsea ikiibuka mbabe mara 20 na zimetoka sare katika michezo 18.
London, England. Chelsea inaikaribisha Arsenal leo katika Uwanja wa Stamford Bridge kuanzia saa 1:30 usiku, kwenye mchezo ulioshika ramani ya timu zote mbili katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) msimu huu.
Kabla ya mechi za jana, Chelsea na Arsenal kila moja ilikuwa imeachwa na kinara Manchester City kwa pointi saba hivyo itakayopoteza leo, itaanza kujiweka katika mazingira magumu ya kutwaa ubingwa kwani inaweza kujikuta ikitanguliwa kwa pointi 10 na Man City iliyocheza jana na Brighton.
Zinakutana huku zikiwa na mwenendo usiovutia katika mechi za hivi karibuni za EPL, ambapo Chelsea katika mechi tano zilizopita, imepata ushindi mara mbili, ikitoka sare mbili na kupoteza moja wakati huo Arsenal ikiwa imepata ushindi katika mechi mbili, imelazimishwa sare mara moja na imepoteza michezo miwili.
Utamu uko hapa
Chelsea imekuwa na unyonge dhidi ya Arsenal kwani haijapata ushindi katika mechi tano mfululizo zilizopita za Ligi Kuu ya England baina yao ambapo imepoteza mechi nne na kutoka sare katika mchezo mmoja.
Katika mechi hizo sita zilizopita za EPL zilizokutanisha timu hizo, Arsenal imefunga mabao 15 ikiwa ni wastani wa mabao matatu kwa mechi wakati huo Chelsea ikiwa imefunga mabao matano ikiwa ni wastani wa bao moja kwa mechi.
Mara ya mwisho kwa Chelsea kupata ushindi mbele ya Arsenal kwenye Ligi Kuu England ilikuwa ni Agosti 22, 2021 na hivyo hadi leo hii, zimetimia siku 1177 kwa timu hiyo kutoonja ushindi dhidi ya Arsenal.
Hata ukiondoa matokeo ya mechi hizo tano zilizopita baina yao, Arsenal bado inaonekana kuwa mbabe kwa kuibuka na ushindi mara nyingi katika mechi zake inazokutanaga na Chelsea kwenye ligi ya England.
Timu hizo zimekutapa mara 64 katika EPL ambapo Arsenal imepata ushindi mara 26 huku Chelsea ikiibuka mbabe mara 20 na zimetoka sare katika michezo 18.
Refa mnoko kushika kipyenga
Refa Michael Oliver ndiye amepangwa kuchezesha mechi hiyo ya leo ambapo atasaidiwa na Stuart Burt, James Mainwaring na refa wa mezani ni Andy Madley na katika tekonolojia ya usaidizi wa video kwa marefa (VAR) watakuwepo Paul Tierney. Assistant VAR: Richard West.
Ni mwamuzi ambaye anasifika kwa kumwaga kadi kwa wachezaji wanaofanya faulo na kuonyesha utovu wa nidhamu na kuthibitisha hilo, katika mechi tisa za mashindano tofauti ambazo amechezesha hivi karibuni, ametoa idadi ya kadi 52 ikiwa ni wastani wa kadi 5.8 kwa mchezo na katika kadi hizo 52, kadi nyekundu ni mbii na kadi za njano ni 50.
Arsenal inaonekana kuwa na bahati na refa Oliver katika mechi za EPL alizoichezesha timu hiyo katika miaka ya hivi karibuni kulinganisha na Chelsea.
Katika mechi tano zilizopita za Ligi ambazo Oliver ameichezesha Arsenal, timu hiyo imepata ushindi mara nne na kutoka sare moja huku Chelsea katika mechi tano zilizopita za EPL ziliamriwa na refa huyo, imepata ushindi mara tatu na kupoteza mechi moja.
Nisterlooy kuachia kijiti
Katika Uwanja wa Old Trafford, Manchester United baada ya kucheza mechi mbili mfululizo za EPL bila kupata ushindi, itaikaribisha Leicester City kwenye mechi itakayoanza saa 11:00 jioni.
Mchezo huo utakuwa ni wa mwisho kwa Ruud Van Nisterlooy ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya meneja wa timu hiyo kwani baada ya hapo atampisha Ruben Amorim kuwa mrithi wa kudumu wa Erik Ten Hag.
Kwingineko, Nottingham Forest itaikaribisha Newcastle United na Tottenham Hotspur itacheza na Ipswich ambapo michezo hiyo yote itaanza saa 11:00 jioni.