Barker abeba tena tuzo Ligi Kuu, beki Singida BS achomoza
Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker. Picha na ,Simba
Muktasari:
- Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker leo Jumatano, Aprili 8, 2026 amtengazwa kuwa Kocha Bora wa mwezi Machi wa Ligi Kuu ya NBC.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Barker amekuwa mshindi kwa kuwapiku Pedro Goncalves wa Yanga na David Ouma wa Singida Black Stars.
Katika mwezi huo, Barker aliiongoza Simba kupata ushindi katika mechi mbili na kutoka sare mbili na kuifanya timu yake ipande kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
Hiyo ni mara ya pili mfululizo kwa Barker kushinda tuzo ya Kocha Bora wa mwezi kwani ndiye alikuwa mshindi wa tuzo hiyo kwa mwezi Februari.
Kwa upande wa wachezaji, aliyeibuka mshindi ni beki wa Singida Black Stars, Ibrahim Imoro.
Imoro katika mwezi huo amefunga mabao matatu katika mechi tano za Singida Black Stars huku akionyesha kiwango bora na amewapiku Anicet Oura wa Simba na Lamine Jarjou anayecheza naye Singida Black Stars.
Meneja wa Uwanja wa Airtel Singida, Omar Malule yeye amefanikiwa kuwa mshindi wa tuzo ya Meneja Bora wa Uwanja.
Katika Ligi ya Championship, Omari Mponda wa Mbuni amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Machi huko Kocha Bora akiwa ni Zuberi Katwila wa Geita Gold.