BMT, TFF watakiwa mahakamani kesho kesi ya uchaguzi
Muktasari:
- Wadau wa Soka nchini wamefungua kesi Mahakama Kuu dhidi ya TFF na wenzake; wakipinga uchaguzi wake unaotarajiwa kufanyika Jumamosi ijayo na wamewataka wafike mahakamani kesho kwa ajili ya kesi hiyo.
Dar es Salaam. Vuguvugu la kupinga uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), limeanza kukolea baada ya wadau mbalimbali kuanza kupishana katika korido za Mahakama pamoja na mambo mengine kwa lengo la kuzuia uchaguzi huo.
Uchaguzi Mkuu wa TFF ambao umekuwa ukilalamikiwa na wadau mbalimbali wa mpira wa miguu, umepangwa kufanyika jijini Tanga, Jumamosi, Agosti 16, 2025.
Hata hivyo baadhi ya wadau wa soka nchini wamefungua mashauri ya maombi Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam katika harakati za kupinga uchaguzi huo.
Miongoni mwa mashauri hayo ni shauri namba namba 19873/2025, lililofunguliwa na mawakili wanne, Aloyce Komba na wenzake watatu, Jeremiah Mtobesya, Deusdedit Luteja na Denice Tumaini.
Wadaiwa katika kesi hiyo ni Baraza la Taifa la Michezo (BMT) lenye dhamana ya usimamizi wa michezo yote nchini, ambalo ndilo mdaiwa wa kwanza; TFF yenyewe (mdaiwa wa pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mdaiwa wa tatu.
Shauri hilo limepangwa kusikilizwa na Jaji Mfawidhi, Salma Maghimbi na mahakama tayari imetoa wito ikiwataka wadaawa kufika mahakamani hapo kesho Alhamis Agosti 14, 2025.
Kwa mujibu wa hati za wito wa mahakama kwenda kwa wadaiwa, ambazo Mwananchi limeziona, wadaiwa wametakiwa kufika mahakamani hapo bila kukosa na kuwasilisha nyaraka zao zote wanazotarajia kuzitumia katika utetezi wao.
“Tambua kuwa kesi tajwa hapo juu, imepangwa kwa ajili ya kutajwa Agosti 14, 2025, saa 3:00 Asubuhi, mbele ya Mheshimiwa Jaji Maghimbi”, zinasomeka hati hizo za wito na kuongeza:
“Unatakiwa kufika katika mahakama hii bila kukosa na unapaswa kuwasilisha siku hiyo nyaraka zako zote unazokusudia kuzitumia katika kesi yako.”
Katika shauri hilo lililofunguliwa chini ya hati ya dharura, wadai wanaiomba mahakama iridhie wafungue shauri la mapitio ya mahakama ili itoe amri kuilazimisha BMT kutekeleza wajibu wake wa kisheria katika kuisimamia TFF pamoja na mambo mengine, MBT iielekeze TFF kufuta uchaguzi huo na kuanza upya.
Hata hivyo wakati wakisubiri uamuzi wa maombi yao hayo ya kibali, wanaiomba mahakama hiyo iridhie kutoa amri ya zuio la muda dhidi ya TFF kutokuendelea na mchakato wa uchaguzi huo.
Zuio hilo linahusisha kuitisha mkutano wa uchaguzi Agosti 16, 2025 au tarehe nyingine yoyote baada ya hiyo mpaka madai waliyoyaibua dhidi ya BMT yatakapofanyiwa kazi.