Bravos yaitishia Simba, hesabu za Yanga ziko hivi
Muktasari:
- Bravos imecheza mechi mbili kwenye uwanja wake wa nyumbani ambapo imekusanya pointi sita hali inayopelekea mchezo baina yao na Simba kuwa mgumu.
Dar es Salaam. Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kimataifa Simba na Yanga tayari wamewasili kwenye mataifa wanayoenda kucheza mechi zao za Mashindano ya CAF, Yanga ikiwa Maurtania ikiwafuata Al Hilal wakati Simba ikiwa Angola ikiwafuata Bravos.
Simba itacheza kesho Jumapili, Januari 12, 2025 dhidi ya Bravos kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika huku ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kupata matokeo katika mchezo wa kwanza uliopigwa kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ambapo iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Jean Ahoua kwa mkwaju wa penati.
Ugumu wa mechi upo hapa
Bravos bado inaamini ina nafasi ya kusonga mbele iwapo itashinda mechi dhidi ya Simba kwani itafikisha pointi tisa sawa na Simba huku ikisubiri matokeo ya mechi za mwisho ambapo itakuwa ugenini Tunisia dhidi ya CS Sfaxien ambayo imeonekana nyepesi kwenye kundi wakati Simba watakuwa na kibarua kigumu nyumbani dhidi ya CS Constantine ya Algeria.
Matokeo ya Bravos kwenye uwanja wao wa nyumbani yanaweza kufanya mchezo ukawa mgumu kwani katika mechi mbili walizocheza wameshinda zote na kukusanya pointi sita wakati katika mechi za Ligi Kuu ya Angola ‘Girabola’ imecheza mechi 15 imeshinda mechi nne, imepata sare mechi nane na imepoteza mechi tatu ikiwa inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 20.
Tatizo la Bravos lipo hapa
Bravos mpaka sasa imeonekana kuwa hatari kwenye mechi zake za nyumbani ambazo imeshinda zote lakini imekuwa ikiruhusu nyavu zake kutikiswa katika mechi zote nne ilizocheza nyumbani na ugenini ikiwa imeruhusu mabao nane ambapo manne imefungwa nyumbani na manne ugenini wakati kwenye Ligi Kuu imefungwa mabao 14 huku yenyewe ikifunga 12.
Kwa upande wa Simba imekuwa bora katika safu ya ulinzi pamoja na ushambuliaji ikiwa imeruhusu mabao matatu katika michuano ya Shirikisho huku ikifunga mabao matano katika michezo minne wakati kwenye Ligi Kuu imecheza michezo 15 ikiwa imeshinda mechi 13, imepata sare mechi moja na kupoteza mechi moja ambapo inaongoza Ligi ikiwa na pointi 40 ikiruhusu mabao matano huku ikifunga mabao 31.
Iwapo Simba itatumia vizuri nafasi itakazo tengeneza inaweza kupata matokeo mazuri yatakayoifanya kufuzu robo fainali moja kwa moja pasipo kusubili mechi ya mwisho. Wachezaji kama Jean Ahoua na Kibu Denis wameonekana kuwa tishio katika mashindano haya wakiwa na mabao mawili kila mmoja wakati Jó Paciência ndiye anaonekana kuwa hatari kwa upande wa Bravos akiwa na mabao mawili.
Hesabu za Yanga zipo hivi
Katika mchezo wa leo Yanga inahitaji matokeo ya ushindi ili kuendelea kubaki na matumaini ya kwenda robo fainali.
Iwapo Yanga itapata ushindi dhidi ya Al Hilal itafikisha pointi saba huku ikisalia nafasi ya pili kulingana na matokeo ya jana ya MC Alger baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya TP Mazembe imefikisha pointi nane.
Yanga itasubili mechi ya mwisho itakapokuwa kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya MC Alger. Katika mechi hiyo Yanga itahitaji matokeo ya ushindi ambayo yataifanya kufikisha pointi 10 zitakazoiweka katika nafasi ya pili huku MC Alger ikibaki na pointi nane.
Kabla ya mechi ya mwisho dhidi ya MC Alger, Yanga inatakiwa kushinda mechi ya leo dhidi ya Al Hilal ambayo tayari imeshafuzu kwenda robo fainali huku ikiwa na kibarua cha kuvunja mwiko wa kutopata matokeo mazuri ikikutana na timu hiyo ambapo katika mechi tatu za mwisho walizokutana Yanga imepoteza mechi mbili na kupata sare mechi moja.
Yanga inawategemea nyota wake kama Stephan Aziz Ki mwenye bao moja alilofunga dhidi ya Mazembe, na Clement Mzize ambaye alifunga mabao mawili wakati Al Hilal ikiwategemea Adama Coulibaly, Jean Claude Girumugisha na Mohamed Abdelrahman amabao wamekuwa wakitamba ndani ya kikosi hicho huku kila mmoja akiwa na bao moja.