Cape Verde yaendelea kushangaza Kombe la Dunia
Muktasari:
Uruguay inashika nafasi ya pili huku Cape Verde ikiwa ya tatu zikiwa na pointi mbili kila moja baada ya michezo miwili ya Kundi H, na zote mbili bado zina nafasi ya kufuzu hatua ya mtoano ya timu 32 bora.
Kampeni ya kwanza ya Cape Verde katika Fainali za Kombe la Dunia imeendelea kuvutia baada ya kulazimisha sare ya kusisimua dhidi ya mabingwa mara mbili, Uruguay, mjini Miami.
Baada ya kuwashangaza mashabiki kwa sare ya 0-0 dhidi ya Hispania katika mchezo wao wa ufunguzi, Cape Verde ilipata bao la kuongoza dhidi ya Uruguay kupitia mpira wa adhabu wa mbali uliopigwa na Kevin Pina katika dakika ya 21, mpira ambao ulipenya katikati ya ukuta wa wachezaji.
Kuongoza kwao kulibadilisha mwenendo wa mchezo kwani Cape Verde ilicheza kwa kushambulia zaidi na kuacha mianya nyuma katika safu yao ya ulinzi.
Baadhi ya wachezaji wa Cape Verde wakishangilia baada ya kusawazisha bao dhidi ya Uruguay. Picha na Mtandao
Uruguay ilitumia vizuri nafasi hiyo ya wazi, huku Maxi Araujo akijirusha na kufunga kwa kichwa bao la kusawazisha baada ya beki Sidny Lopes Cabral kuugusa mpira na kuuelekeza langoni kwao.
Agustin Canobbio, ambaye hakuwa katika kikosi cha kwanza cha Uruguay kilichotoka sare ya 1-1 dhidi ya Saudi Arabia, alithibitisha kwa nini alijumuishwa kwenye kikosi safari hii kwa kufunga bao la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kupokea pasi ya Araujo akiwa karibu na lango.
Usambazaji duni wa mpira wa Cape Verde mbele ya presha kubwa ya Uruguay uliwafanya washindwe mara nyingi kujenga mashambulizi kutokea nyuma, ingawa waliendelea kutafuta nafasi za kufunga.
Hata hivyo, Cape Verde ilifanikiwa kusawazisha matokeo kutokana na kosa la umakini kutoka kwa safu ya ulinzi ya Uruguay.
Mathias Olivera alijaribu kuupiga mpira kuvuka eneo lake la hatari lakini hakumuona Helio Varela aliyekuwa akisubiri. Varela aliudhibiti mpira, akampita kipa na kisha kuutumbukiza nyavuni.
Uruguay ilikaribia kupata bao la ushindi, lakini bao la Federico Valverde lilikataliwa kutokana na kuotea baada ya kuusukuma mpira wavuni akiwa karibu na lango.
Timu zote mbili zilipata nafasi nyingine za kufunga katika dakika za nyongeza, lakini hakuna iliyofanikiwa kupata bao la ushindi.
Uruguay, iliyopo nafasi ya pili, huku Cape Verde ikiwa ya tatu, sasa zina alama mbili kila moja baada ya michezo miwili katika Kundi H, na zote mbili bado zina nafasi ya kufuzu hatua ya mtoano ya timu 32 bora.