Chama afanya yake tena Jeshini
Muktasari:
- Hii ni mechi ya pili mfululizo kwa Chama kufunga bao katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ambapo alifanya hivyo pia katika mechi iliyopita dhidi ya Yanga.
Dar es Salaam. Simba imeendelea kujiimarisha katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya leo Jumatano, Mei 6, 2026 kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania Kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Simba ilianza kwa presha ya juu, ikitengeneza mashambulizi ya mapema kupitia Clatous Chama, Ellie Mpanzu na Libasse Guaye.
Hata hivyo, JKT Tanzania ilionekana imara kiulinzi, ikiongozwa vyema na Karim Mfaume na Laurian Makame kabla ya kupata majeraha waliziba mianya muhimu hasa katika maeneo ya pembeni ambako Simba ilijaribu kupenyeza mara kwa mara.
Licha ya Simba kujaribu mbinu mbalimbali za kushambulia, JKT iliendelea kuwa makini na kuondoa hatari zote karibu na lango lao.
Hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika, hakuna timu iliyopata bao. Simba ilikuwa na mashuti matano, mawili yakilenga lango na kupata kona nne, huku JKT ikiwa haijapiga shuti lililolenga goli.
Dakika ya 45+2 ilishuhudia JKT ikilazimika kufanya mabadiliko baada ya Makame kuumia, nafasi yake ikichukuliwa na Edson Katanga.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi kutoka kwa Simba, iliyoongeza mashambulizi na kuweka presha kubwa langoni mwa wapinzani wao.
Jitihada hizo zilizaa matunda dakika ya 52, ambapo Ellie Mpanzu alitoa pasi safi iliyomkuta Clatous Chama, naye akamalizia kwa utulivu na kuipa Simba bao pekee katika mchezo.
Bao hilo lilikuwa mwendelezo wa ubora wa Mpanzu na Chama, ikumbukwe wawili walihusika katika bao la pili la Simba wikendi iliyopita katika sare ya 2-2 dhidi ya Yanga kwenye dabi ya Kariakoo. Kwa Chama, hilo lilikuwa bao lake la tano msimu huu.
Baada ya kupata uongozi, Simba ilifanya mabadiliko ya kiufundi kwa kumtoa Libasse Guaye na kumuingiza Seleman Mwalimu kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji.
Baadaye, Alassane Kante alichukua nafasi ya Loemba ili kuimarisha kiungo na kudhibiti mchezo.
JKT Tanzania walijaribu kuongeza kasi kusaka bao la kusawazisha lakini Simba ilionyesha nidhamu katika kulinda na kudhibiti kila hatari.
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 45 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara nyuma ya Yanga wenye pointi 51.