Coastal Union yaomba radhi kwa vurugu
Kikosi cha Coastal Union
Muktasari:
Mchezo huo wa Ligi Kuu ulimalizika kwa vurugu kabla ya kikosi cha kutuliza ghasia kuingilia kati na kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki wa Coastal Union kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani.
Tanga. Klabu ya Coastal Union imewaomba radhi wadau pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa vurugu zilizotokea katika mchezo wao dhidi ya Mbeya City uliofanyika Jumamosi.
Mchezo huo wa Ligi Kuu ulimalizika kwa vurugu kabla ya kikosi cha kutuliza ghasia kuingilia kati na kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki wa Coastal Union kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani.
Vurugu hizo zilitokea baada ya mwamuzi, Erick Enock kutoka Arusha kuamuru ipigwe penalti kwa upande wa Coastal Union katika dakika za majeruhi na Mbeya City kusawazisha kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare bao 1-1.
Coastal Union iliomba radhi katika barua yake iliyoandikwa na kutiwa saini na Mwenyekiti Dk Ahmed Twaha kwenda kwa Katibu wa TFF na nakala kwa Rais Jamal Malinzi, Ofisa Mtendaji Mkuu Bodi ya Ligi na Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Tanga (TRFA).
Katika barua hiyo ambayo Mwananchi imepewa nakala, Mwenyekiti huyo alisema alilazimika kuitisha kikao cha dharura cha kamati ya utendaji kujadili nini cha kufanya.
Katika kikao hicho alisema kamati ya utendaji imelaani vurugu hizo na imeazimia kuwachukulia hatua waliohusika
“Tunaomba radhi kwa TFF na TRFA kwa matukio hayo yaliyofanywa Oktoba 31, tunatoa ahadi klabu ya Coastal Union kufidia gharama za uharibifu utakaothibitika na kuwachukulia hatu waliohusika,” ilieleza sehemu ya barua hiyo ya Dk Twaha.