Coastal Union yawinda vipaji chipukizi kupitia Tanga City Cup
Muktasari:
- Timu ya Coastal Union ya jijini Tanga imeanza kunufaika na mashindano ya Tanga City Cup kwa kubaini na kuwinda vipaji vipya vya soka kutoka kata mbalimbali, hatua inayolenga kuimarisha kikosi chao huku wakipunguza gharama za uendeshaji wa timu.
Tanga. Timu ya Coastal Union ya jijini Tanga imeanza mchakato wa kuwanyemelea wachezaji chipukizi wenye vipaji maalumu waliojitokeza katika mashindano ya Tanga City Cup yaliyoanza Aprili 11, 2026, yakishirikisha timu kutoka kata zote 27 za Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Hatua hiyo inalenga kuongeza ubora wa kikosi cha Coastal Union huku ikipunguza gharama za kambi kwa kutegemea zaidi vipaji vya ndani vinavyoibuliwa kupitia mashindano hayo ya ngazi ya jamii.
Akizungumza wakati wa hafla ya droo ya hatua inayofuata ya mashindano hayo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Tanzania na Mwenyekiti wa Klabu ya Coastal Union, Hassan Muksin, amesema kuwa ligi hiyo imekuwa chachu ya maendeleo ya soka nchini pamoja na kuibua vipaji vipya kwa klabu hiyo.
“Kupitia ligi hii tayari tumebaini vipaji vipya vya mpira wa miguu. Hii itapunguza gharama kwa Coastal Union kwenda kutembelea kata mbalimbali kutafuta wachezaji chipukizi wenye vipaji. Mkurugenzi wa jiji asichoke kwenye hili, atalisaidia jiji letu na mkoa kwa ujumla,” amesema Muksin.
Ameongeza kuwa hata timu ambazo hazikufanikiwa kufika hatua za juu zisikate tamaa bali ziendelee kushiriki pale fursa zitakapotolewa tena.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Tanzania na Mwenyekiti wa Klabu ya Coastal Union, Hassan Muksin akizungumzia mpango wao wa kutumia wachezaji wa ndani kwenye timu hyo watakaowapata kwenye ligi ya Tanga City Cup.
“Timu zilizoshiriki ambazo hazikufika kwenye hatua ya nusu fainali zisikate tamaa; wakati mwingine Mkurugenzi wa jiji atakapotoa tangazo tena, timu zijitokeze kama zilivyofanya kwenye mashindano haya ili tuendelee kutafuta wadau na kuboresha zaidi mashindano haya,” amesema mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake, Afisa Michezo wa Jiji la Tanga, Yusuph Linza, amesema mashindano hayo yamefanyika katika kata zote za jiji pamoja na tarafa zote nne za wilaya ya Tanga, na kwamba yamekuwa na mchango mkubwa kwa jamii.
Kiongozi huyo wa Coastal Union amebainisha kuwa mashindano hayo ni muhimu hasa katika kipindi ambacho timu inakabiliwa na changamoto za kifedha, akisisitiza umuhimu wa kuwa na wachezaji wengi wa ndani.
“Timu yetu iko kwenye changamoto kidogo ya kifedha, hivyo tutakapopata wachezaji wa ndani tutaondokana na gharama za kuwaweka kambini. Hili litaturahisishia sana kwa kuwa tutakuwa tumepata vijana wa kutumia na kuwapa nafasi ya kucheza kwenye timu za ndani na nje ya mkoa wa Tanga,” amesema Muhsin.
“Kwa kiasi kikubwa tunaweza kusema ligi hii imefanikiwa; tumeona vipaji vingi na fursa mbalimbali. Tumefika hadi maeneo ya mbali kama Tongoni na kuibua vipaji vipya vitakavyotumika kwenye timu zetu,” amesema Linza.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Fedha, Mipango na Rasilimali wa Coastal Union, Said Bandawe, amesema mashindano hayo ni fursa muhimu kwa vijana wa Tanga kujiunga na klabu hiyo.
“Zamani asilimia kubwa ya wachezaji wa Coastal Union walitoka Tanga, lakini sasa wengi wanatoka nje. Hatukatai hilo kwa kuwa ni Tanzania nzima, lakini tungependa kuona vijana wa Tanga wanapata nafasi zaidi huku tukipunguza gharama za uendeshaji,” amesema Bandawe.
Mdau wa michezo na Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji ya Tanga Yetu, Juma Iddy, ambao ndio wadhamini wakuu wa mashindano hayo, amesema wana nia ya kuendelea kudhamini ligi hiyo kutokana na mchango wake kwa jamii.
“Ukiwaona wachezaji kama Mwamnyeto wakicheza Yanga, kipato wanachopata hurudi kusaidia familia na kuchangia uchumi wa Tanga. Hii inaonyesha wazi kuwa michezo ni ajira,” anasema Iddy.
Ameongeza kuwa lengo lao ni kuifanya Tanga kuwa sehemu salama kwa vijana na watoto kupitia michezo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa timu ya kata ya Ngamiani Kati, Ally Jumamosi, amesema mashindano hayo yameleta hamasa kubwa na kuibua vipaji katika eneo lake.
“Tumeanzia mbali kwenye zone yetu; tumeanza na timu za kata yetu hadi kufikia robo fainali na sasa tupo nusu fainali,” anasema Jumamosi.
Mashindano ya Tanga City Cup yanaendelea kuonekana kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji, kukuza ajira kupitia michezo, na kuimarisha maendeleo ya soka katika jiji la Tanga na Tanzania kwa ujumla.