Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dilunga afunguka kutemwa na Yanga

Muktasari:

  • HASSAN Dilunga ama ukipenda muite HD ni miongoni mwa viungo bora wa Simba, akiwa amepita katika timu nyingi kabla ya kutua Msimbazi ambapo ameonekana amekaa muda mrefu kuliko sehemu nyingine.

HASSAN Dilunga ama ukipenda muite HD ni miongoni mwa viungo bora wa Simba, akiwa amepita katika timu nyingi kabla ya kutua Msimbazi ambapo ameonekana amekaa muda mrefu kuliko sehemu nyingine.

Kinachomuweka hapo kiungo huyo ni ubora wake ambao ameonekana kuulinda kwa miaka aliyocheza Ligi Kuu Bara akipitia Yanga, JKT Tanzania, Stand United na Mtibwa Sugar.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Dilunga anaeleza mambo mbalimbali kwenye soka na juu ya ubora wa timu yake kwenye michuano ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo imetinga hatua ya robo fainali ikikusanya pointi 13. Fuatana naye katika mahojiano haya.

“Tunafahamu umuhimu wa kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo tumetinga robo fainali, na ili tushiriki kwa mara nyingine maana yake tunatakiwa kuchukua ubingwa wa ligi (kuu),” anasema Dilunga.

“Hivyo naipa nafasi kubwa timu yangu kufanya vizuri, lakini hata katika mashindano mengine kama Kombe la Shirikisho (ASFC) nalo tunaweza kufanya vizuri na tukachukua ubingwa.”


KUPANDA NA KUSHUKA

Dilunga anasema katika maisha kuna changamoto nyingi na hakuna binadamu ambaye kila siku yupo sawa kwani kuna wakati mambo huenda tofauti na kushindwa kufanya vile anavyotarajia.

“Nakumbuka mwisho wa msimu uliopita chini ya kocha Sven Vandenbroeck nilifanya vizuri na nilimaliza ligi nikiwa nimefunga mabao manane, jambo ambalo wakati huu limekuwa changamoto kwangu,” anasema.

“Kupanda na kushuka kwangu kwa sasa kunachangiwa na mambo mawili; kwanza nashindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kila mechi, licha ya mazoezi kufanya vizuri. Lakini upana wa kikosi chetu ambao wengi wanafanya vizuri na kumefanya tucheze kwa kupishana, jambo ambalo limenifanya nicheze dakika chache au kukosekana kabisa.”


MABADILIKO

Kwa miaka mitatu ambayo yupo katika kikosi hicho amekutana na makocha watatu tofauti ambao ni Patrick Aussems, Sven na Didier Gomes na hapa anasema mabadiliko hayo ni kama yamemuathiri ndio maana anakosa nafasi ya kucheza kwani wakati anatumika mara kwa mara wachezaji ambao wanacheza zaidi wakati huu walikuwa wanakaa benchi.

“Kikubwa ni nafasi ya kuch eza, ndio naipigania wakati huu licha ya kwamba kipindi cha Aussems nilikuwa natumika mara kwa mara tofauti na sasa ndio nione kama mabadiliko ya makocha yamenigusa,” anasema.


MABAO, ASISTI

Dilunga anasema licha ya kupitia wakati mgumu kucheza bado hajakata tamaa kutokana na rekodi zake zilivyo katika nafasi chache ambazo ametumika.

“Licha ya changamoto hiyo katika ligi msimu huu, nimecheza muda mchache lakini nimefunga mabao mawili na kutoa pasi za mwisho nne (assist) kwa wenzangu ambao walizitumia kufunga mabao ambayo yalikuwa msaada kwa timu,” anasema.

“Naamini nafasi yangu ya kucheza ipo, ila ni suala la muda tu kufika, hilo litawezekana na nitapambana kadri ambavyo naweza ili kufikia malengo yangu.”


NAMBA NANE

Licha ya kucheza kama winga, lakini anasema: “Kimsingi huwa napenda zaidi kucheza namba nane, ndio nafasi ambayo tangu nikiwa mdogo katika timu za vijana nilizocheza mpaka soka la ushindani ambayo naifurahia kucheza, nikiwa na furaha.

“Muda mwingine huwa napenda kucheza namba 10 kwani ndio nafasi ambazo kama majukumu yake yanalingana, lakini kutokana na jukumu langu ni kucheza siwezi kuchagua eneo la kulitumikia.”


KUTIMKA YANGA

Mchezaji huyo anasimulia namna alivyoondoka Yanga kuwa, ilitokana na mambo mengi kutokana na timu kubwa zilivyo.

Anasema hakuondoka kutokana na kushuka kwa kiwango chake, bali kuna vitu vilitokea akiwa timu ya taifa ambapo alikutana na taarifa kutoka kwa mabosi wake kuchagua moja kati ya kuachwa au kutolewa kwa mkopo.

“Sifahamu kitu gani ambacho kilifanya mpaka kuondoka pale, lakini nashukuru kuondoka kwangu kulinipa akili mpya ya kwenda kupata changamoto nyingine nilipoenda mpaka kurudi timu kubwa,” anasema.

“Sijajua kwa upande wa Yanga, ila kwangu haikuwa wakati wangu wa kuondoka, halikuwa jambo sahihi kwani nilikuwa nacheza na nilitoka timu ya taifa.”


MECHI YA DABI

Kuhusu mechi ya watani wa jadi, mchezaji huyo anasema anafurahia zaidi kucheza mechi hiyo kutokana na umuhimu wake.

“Binafsi napenda sana kucheza hizi mechi kubwa kama Simba na Yanga, Simba na Azam kwani hizo ni aina ya mechi ambazo natakiwa nicheze ili nionekane vile vitu bora ambavyo natakiwa kufanya,” anasema.

“Nakumbuka nikiwa Yanga nilicheza mechi dhidi ya Simba, ilikuwa Mtani Jembe, niliingia kipindi cha pili na nilicheza vizuri, huku nilipo ndio nimetumika nyingi dhidi ya Yanga tena kwa kiasi kikubwa na nashukuru nimekuwa nikifanikiwa kucheza vizuri na kutoa kile ambacho nimebarikiwa nacho na timu yangu kufanya vizuri.

“Ukiondoa presha waliyonayo mashabiki wangu (dhidi ya mechi kubwa) naichukulia kama mechi ya kawaida ambayo nikipata nafasi napenda kuonyesha vitu bora ili kuisaidia timu kupata ushindi.”


TIMU NYINGI, YUPO BOMBA

Kiungo huyo amepitia timu nyingi na sasa Simba ambapo anasema wachezaji wengi huondoka kwenye timu kubwa (za Simba na Yanga) na mara nyingi huenda chini wanapotea moja kwa moja, lakini kwake haikuwa hivyo.

“Hata wakati naondoka Yanga sio kama nilikuwa mchezaji mbaya, hapana, bali na aliyekuwa anacheza nafasi yangu hakunizidi sana kiwango, ila ndio alikuwa chaguo la kwanza la kocha,” anasema.

“Baada ya kuondoka niliweka malengo ya kupambana na kurudi tena timu kubwa, nashukuru hilo nimefanikiwa, ndio maana nipo hapa wakati huu.”


MIAKA MITATU SIMBA

Mchezaji huyo anasema mkataba wa miaka mitatu Simba umekuwa na mafanikio makubwa kwake na hajutii kuitumikia.

“Ndani ya timu nilikuwa sehemu ya historia kuifikisha robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, tumechukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho na Ngao ya Hisani, kila moja kwa awamu mbili nami nipo,” anasema Dilunga.

“Tumechukua ubingwa wa ligi mara tatu na hii ni awamu yangu ya nne tunaenda kuuchukua tena, na kutokana na mwenendo wa ligi sioni kama tunaweza kushindwa kulibeba tena.”


MSUVA AMSHTUA

Kabla ya kutua Simba, Dilunga alihusishwa kusajiliwa na timu ya Difaa El Jadida ya Morocco aliyokuwa akiichezea Saimon Msuva.

Hata hivyo, mchezaji huyo anaeleza kuwa: “Nakumbuka baada ya Simba kuonyesha nia ya kunitaka kulikuwa na viongozi fulani hivi walinifuata na kuniambia jambo la kwenda timu hiyo (El Jadida), lakini kadri muda ulivyozidi kwenda sikuona mwendelezo wa jambo hilo.

“Niliamua kumpigia simu Msuva na kumuuliza kama alisikia jambo lolote kuhusu kuhitajika na timu hiyo ndio alinishtua kuwa hakuna jambo kama hilo. Baada ya hapo ndio nikafanya uamuzi wa kusaini Simba ambao walikuwa wamenifuata na kila kitu tulichokubaliana.”


MFANYA BIASHARA

Dilunga anasema kama asingekuwa mwanasoka, basi wakati huu angekuwa mfanyabiashara kwani alikuwa na mambo kibao ya kufanya katika biashara.

“Baba yangu ni mfanyabiashara na kabla ya maisha ya mpira kunicha-nganyia nilikuwa nikimsaidia kwenye biashara zake, na nahisi mwenyewe aliamini, nami nitakuja kuwa kama yeye,” anasema.

“Sijui ningekuwa mfanyabiashara wa nini wakati huu, ila kutokana na maisha ambayo nimekulia pamoja na kumsaidia baba ningekuwa nafanya moja ya biashara halali iliyokuwa hapa mjini.”


AMKUBALI KAZIMOTO

Mchezaji huyo anasema miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa wanamvutia kabla hajaanza rasmi kucheza soka ni kiungo wa JKT Tanzania, Mwinyi Kazimoto.

“Wakati nacheza mpira kuna jamaa mmoja alinifuata na kuniambia kuwa nacheza mpira kama Kazimoto, tena wakati huo nilikuwa simfahamu na baada ya hapo nilianza kumfutilia na kumuangalia anavyocheza.

Baada ya kumuona akicheza, nikatokea kumkubali mpaka leo nasikia raha kumuona akiwa anacheza na niliwahi kutamani siku nije kucheza naye.

“Sikubahatika kucheza naye timu moja, lakini ni moja ya watu ambao wananishauri kufanya maisha nje ya soka ili nifanikiwe, mpaka leo tunawasiliana. Wakati naenda Ruvu Shooting mechi ya kwanza kucheza tu kikosi kizima kiliniambia huyo ni mbadala wa Kazimoto,” anasema Dilunga.


TSHABALALA, NDEMLA WASHIKAJI

Ukimuuliza ni wachezaji gani kikosini ambao anaiva nao kwa miaka mingi, Dilunga anawataja mastaa wawili waliokulia Msimbazi.

“(Mohamed Hussein ‘Tshabalala na Said Ndemla) hawa ni washikaji zangu zaidi kwani kabla hata ya kuja hapa (Simba) tukiwa wadogo katika timu za vijana huko tulikuwa tunakutana na kuwasiliana mara kwa mara,” anasema.

“Lakini hata wakati huu huwa tunaongea na kuwa wote muda mwingi na hata muda mwingine tunapigiana simu za kwenda kufanya mazoezi kwa pamoja, tofauti na yale ambayo tunafanya tukiwa na timu.

“Siyo kama wachezaji wengine sio rafiki zangu nisieleweke vibaya, bali hawa tulikuwa wote tangu wadogo na hatukuwa tunafikiria kama tutakuja kucheza timu kubwa kama hii kwa pamoja.”


MECHI MBILI

Kiungo huyo anasema kwa muda ambao ameishi katika kikosi cha Simba hatazisahau mechi mbili dhidi ya Mtibwa Sugar na Nkana Red Devils ya Zambia.

“Mechi na Mtibwa ya Ngao ya Hisani ndio ilikuwa ya kwanza kwangu, niliifunga bao timu hiyo ambayo nilitokea na nilitoa pasi ya mwisho ya bao la Meddie Kagere,” anasema.

“Nakumbuka baada ya mechi hiyo familia yangu ilinipigia simu na kunipatia zawadi ya kile ambacho nimekionyesha, lakini mechi nyingine ni dhidi ya Nkana niliingia kipindi cha pili na nilitoa pasi ya mwisho kwa Clatous Chama ambaye alifunga bao la ushindi kwa timu yetu tukaenda hatua ya makundi.”