Fainali Mapinduzi Cup 2026...Vita ya ushambuliaji na ulinzi
Azam na Yanga kesho Jumanne zitacheza fainali ya Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba huku timu hizo kila moja ikiwa na hesabu za ubingwa.
Azam inasaka taji la tano baada ya kubeba mwaka 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019, huku Yanga ikilisaka kwa mara ya tatu. Tayari imelichukua 2007 na 2021.
Yanga hii inakuwa fainali ya nne katika historia ya Kombe la Mapinduzi ikifanya hivyo mwaka 2007, 2011, 2021 na sasa 2026. Azam ni fainali ya saba, kati ya sita zilizopita imebeba ubingwa mara tano na kukosa moja mwaka 2022 ilipochapwa na Simba.
Yanga na Azam hii ni mara ya kwanza zinakutana katika fainali ya Kombe la Mapinduzi. Rekodi zianonyesha mara ya mwisho zilikutana katika fainali ya Kombe la FA iliyochezwa Zanzibar Juni 2, 2024 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex. Yanga ilishinda kwa penalti 6-5 baada ya muda wa kawaida matokeo kuwa 0-0
Wakati kila moja ikiwa na hesabu zake, haitakuwa rahisi kutokana na timu hizo zilivyofanya kuanzia makundi hadi kufikia hapa.
Safari zao
Azam iliyokuwa kundi A, ilianza safari ya kusaka taji la sita kwa kutoka 1-1 dhidi ya Singida Black Stars, kisha ikaifunga Mlandege 2-0 na kumalizia kuichapa URA 2-1.
Hatua ya nusu fainali, ilikwenda kuichapa Simba bao 1-0, hivyo hadi kumaliza michuano hii, Azam itakuwa imekutana na timu tatu zilizomaliza nne bora ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita ambazo ni Singida, Simba na Yanga.
Kwa upande wa Yanga ilikuwa kundi C, imeshinda mechi zote ikianza kuifunga KVZ 3-0, ikaja kuichapa TRA United 1-0, nusu fainali ikaifunga Singida Black Stars 1-0.
Wachezaji wa kutazamwa
Jephte Kitambala wa Azam, ndiye kinara wa mabao aliyebaki katika mashindano haya akiwa nayo mawili. Ndiye mshambuliaji tegemeo wa Azam kuelekea mechi hii ya fainali.
Safu ya ulinzi ya Yanga inapaswa kumchunga kwani amekuwa hatari kwa wapinzani tangu atue msimu huu.
Tayari mshambuliaji huyo ameitungua Simba katika mechi ya ligi alipokutana nayo kwa mara ya kwanza. Pia anakwenda kucheza dhidi ya Yanga kwa mara ya kwanza.
Mbali na Kitambala, kuna Zidane Sereri, anayeunda pacha naye safu ya ushambuliaji ya Azam. Naye amefunga bao moja. Pia aliifunga Simba msimu uliopita, hivyo sio mgeni wa mechi kubwa.
Yanga ina Pacome Zouzoua, amefunga na kutoa asisti, ni mmoja wa wachezaji hatari eneo la kutengengeneza mashambulizi. Azam imchunge sana.
Mwingine ni Maxi Nzengeli. Ana tuzo zake mbili za mchezaji bora, hiyo inaonyesha ni mtu hatari ndani ya uwanja. Amefanikiwa kufunga bao moja.
Kazi ipo hapa
Kila upande una kazi ya kufanya kuhakikisha inabeba ubingwa. Azam iliyofunga mabao sita katika mechi nne, ina kazi ya kuipenya ngome ya Yanga ambayo haijaruhusu nyavu zake kutikiswa hadi sasa ikishuka dimbani mara tatu.
Hata hivyo, Azam imekuwa na rekodi ya kufunga bao kila mechi iliyocheza, hivyo timu kesho kazi ipo katika kuendeleza mwendo wao huo dhidi ya timu isiyofungika.
Yanga ina kazi ya kulinda lango lake na kuweka rekodi ya kumaliza bila nyavu zake kutikiswa, huku pia ikihitaji bao kuifanya pia ifunge kila mechi.
Pigo kwa Yanga
Kuna wachezaji kadhaa wanaweza kukosekana baada ya kupata majeraha katika mashindano haya akiwamo Sadio Kanoute wa Azam, Lassine Kouma na Aziz Andabwile upande wa Yanga.
Lakini pia Yanga itamkosa Mohamed Damaro anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa hatua ya nusu fainali.
Damaro alikuwa mchezaji tegemeo eneo la kiungo mkabaji, hivyo kukosekana kwake itamlazimu Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves kumpa majukumu mwingine. Iwe Duke Abuya au Mudathir Yahya ambaye amepona hivi karibuni.
Makocha wanasemaje?
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema: "Kufika fainali ni sehemu ya kuyafikia malengo yetu tuliyojiwekea wakati tunakuja kushiriki mashindano haya. Tunautaka ubingwa lakini pia tupo hapa kuimarisha kikosi kuelekea mechi za CAF ndio maana natoa fursa kwa wachezaji tofauti tuliokuja nao."
Kocha wa Azam, Florent Ibenge naye amesema: "Niliweka malengo ya kucheza mechi tano katika mashindano haya na hiyo inakwenda kutimia siku ya fainali. Lakini pia malengo ya ubingwa yapo palepale.
"Ubingwa utatupa nafasi nzuri ya kuona wapi tumefanikiwa kwani tunakabiliwa zaidi na mechi ngumu ya CAF ugenini dhidi ya Nairobi United."