Fainali ya Aziz Ki, Fei Toto
Dar es Salaam. Hapana shaka fikra za wengi zinawawaza zaidi viungo washambuliaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC na Stephane Aziz Ki wa Yanga katika mechi baina ya timu zao kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar leo.
Baada ya Stephane Ki kuibuka mshindi wa vita ya kuwania ufungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliomalizika, leo wawili hao wana kibarua kingine cha tofauti cha kila mmoja kuhakikisha anaisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB katika mechi ya fainali itakayochezwa kuanzia saa 2:15 usiku.
Uwezo wa kufumania nyavu ulioonyeshwa na Aziz Ki aliyeibuka mfungaji bora akifunga mabao 21 na Fei Toto aliyeshika nafasi ya pili akifunga mabao 19 walionyesha kwenye Ligi Kuu ni wazi kwamba unawafanya kuwa wachezaji tegemeo zaidi kwa kila upande ingawa wapo nyota wengine wanaoweza kuiamua mechi hiyo ikiwa mmojawapo au wawili hao wakishindwa kufua dafu.
Hii ni mara ya kwanza katika historia kwa mechi ya fainali ya mashindano hayo kuchezwa katika Uwanja wa Amaan na mara zote za nyuma zilikuwa zikichezwa katika viwanja na miji tofauti Tanzania Bara.
Ni fainali ya muhimu kwa kila timu kuibuka na ushibdi ambao utaipatia taji litakaloifanya imalize msimu kwa heshima.
Ushindi kwa Azam FC utaihakikishia kumaliza na taji moja kubwa msimu huu baada ya kushindwa kuchukua lile la Ligi Kuu ambalo lilichukuliwa na Yanga na Ngao ya Jamii lililotwaliwa na Simba.
Yanga kama itashinda mchezo, kutwaa taji hilo kutamaanisha kuwa ndio klabu iliyofanikiwa zaidi msimu huu hapa nchini kwani litakuwa taji lake la pili kubwa baada ya kunyanyua la Ligi Kuu wiki mbili zilizopita.
Hadi inafika hatua ya fainali, Yanga ilizitoa Hausung, Polisi Tanzania, Dodoma Jiji, Tabora United na Ihefu wakati Azam FC ilizitupa nje timu za Alliance, Green Warriors, Mtibwa Sugar, Namungo na Coastal Union.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, ikiwa dakika 90 zitamalizika pasipo kuwa na mshindi, kutaongezwa dakika 30 na kama nazo zitamalizika kwa sare, mikwaju ya penalti itapigwa kusaka mshindi wa fainali hiyo.
Hakuna mnyonge
Ni fainali inayokutanisha timu ambazo matokeo ya mechi tano ambazo kila moja imecheza kwenye mashindano hayo msimu huu yanathibitisha kwamba zilistahili kufika hapo zilizopo.
Timu zote mbili zimeonyesha makali ya kufumania nyavu kwenye mashindano hayo msimu huu huku zikionyesha uimara wa hali ya juu kwenye safu zao za ulinzi na zimetofautiana kwa bao moja moja tu katika kufunga na hata kuruhusu nyavu zao kutikiswa.
Azam imefunga mabao 17 katika mechi tano zilizopita ikiwa ni wastani wa mabao 3.4 kwa mchezo na imeizidi Yanga bao moja tu kwani wapinzani wao hao wamefunga mabao 16 ikiwa ni wastani wa mabao 3.2 kwa mechi.
Yanga imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu katika michezo mitano iliyopita ya Kombe la Shirikisho la CRDB msimu huu ikiwa ni wastani wa bao 0.2 kwa mechi na Azam imefungwa mabao mawili ikiwa ni wastani wa bao 0.4 kwa mchezo.
Kisasi na ubabe
Hii ni fainali ya tisa ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la CRDB tangu mashindano hayo yalipoanza msimu wa 2015/2016 na baadhi kati ya nane zilizopita zinafanya upande mmoja kuwa na hamu ya kuendeleza ubabe kwa mwenzake na mwingine kuwa na hamu ya kulipa kisasi.
Yanga imekuwa na historia nzuri ya ubabe katika mechi za fainali za mashindano hayo dhidi ya Azam FC ambapo timu hizo zimewahi kukutana mara mbili tofauti na Yanga imeibuka na ushindi mara zote.
Mara ya kwanza ilikuwa ni fainali ya msimu wa 2014.2015 ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 na mara ya pili ni msimu uliopita ambapo Azam ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0.
Kwa maana hiyo, ushindi kwa Azam FC leo utakuwa angalau umeifanya ilipe kisasi cha kuonewa na Yanga kwenye mechi za fainali za mashindano hayo.
Sopu na Mzize wana vita yao
Wakati Azam na Yanga kila moja ikiwa na kiu ya taji katika mechi ya leo, nyota wao wawili, Clement Mzize na Abdul Sopu wao watakuwa na kibarua cha kusaka ufungaji bora wa mashindano hayo msimu huu kwani ndio wanafukuzana kileleni katika chati ya kufumania nyavu katika Kombe hilo.
Mzize ndiye kinara wa ufungaji wa mashindano hayo hadi sasa akiwa amefunga mabao matano na anafuatwa kwa ukaribu na Sopu ambaye yeye amefunga mabao manne hadi sasa.
Rekodi kuchochea moto
Ushindi kwa Yanga utaifanya iandike rekodi ya kuwa timu iliyochukua taji hilo mara nyingi zaidi tangu msimu wa 2015/2016 mashindano hayo yalipoanza ambapo kwa sasa ipo sawa na Simba kila moja ikitwaa taji mara tatu.
Itakuwa ni mara ya pili kwa Azam FC kutwaa taji hilo iwapo leo itaibuka na ushindi mbele ya Yanga.
Makocha macho kwenye taji
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema kuwa hawatoingia na fikra za kukumbuka mechi iliyopita baina yao na badala yake wataifikiria zaidi mechi ya leo.
"Kwenye mpira hakuna kulipiza kisasi ukienda kwenye mchezo kwa nia ya kulipiza kisasi hutakuwa na mchezo mzuri, namuheshimu mpinzani wangu Azam na lazima twende tukacheze mchezo wenye mbinu nzuri ili tuweze kuibuka na ushindi.
"Tumepata muda mzuri wa maandalizi na leo (jana) tutafanya maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo wetu wa fainali kesho (leo). Niwapongeze kwa kuchagua Uwanja wa Zanzibar kwasababu ni uwanja mzuri wa kisasa na watu wa Zanzibar pia wataweza kupata nafasi ya kushuhudia fainali hii kubwa," alisema Gamondi.
Kocha wa Azam FC, Bruno Ferry alisema kuwa wamewaelekeza wachezaji wao kuwa na utulivu katika mechi ya leo.
"Hatutaki wachezaji wawe na presha, tunataka wacheze kwa furaha na wafurahie mechi," alisema Ferry.
Mabingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB
Yanga- 2015/2016
Simba- 2016/2017
Mtibwa- 2017/2018
Azam- 2018/2019
Simba- 2019/2020
Simba- 2020/2021
Yanga- 2021/2022
Yanga- 2022/2023