Fainali ya ‘vurugu’ Senegal ikitwaa ubingwa AFCON
Senegal ikishangilia ubingwa baada ya kukabidhiwa kombe. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Kabla ya Fainali za AFCON 2025, mara ya mwisho kwa Senegal kutwaa ubingwa wa mashindano hayo ilikuwa ni katika fainali za 2021 na Morocco ilifanya hivyo mwaka 1976.
Dar es Salaam. Senegal imeishtua Morocco baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 iliyochezwa Jumapili Januari 18, 2025, matokeo ambayo yamewanyima fursa wenyeji Morocco kutwaa ubingwa wa mashindano kwa mara ya kwanza tangu walipofanya hivyo mwaka 1976.
Bao pekee la Pape Gueye katika dakika ya 94 ya mechi hiyo iliyochezwa kwa dakika 120, lilitosha kuipa ushindi Senegal dhidi ya wenyeji, katika mechi ambayo iliyogubikwa na matukio ya aibu kufuatia uamuzi tata wa penalti waliyopata Morocco.
Brahim Diaz angeweza kuipatia Morocco taji hilo alipokwenda kupiga penalti katika dakika ya 24 ya muda wa nyongeza mwishoni mwa muda wa kawaida.
Hata hivyo, kipa wa Senegal Edouard Mendy aliokoa kwa urahisi penalti ya winga wa Real Madrid, ambaye alijaribu kufunga kwa staili ya upigaji penalti ya ‘Panenka’.
Mwamuzi wa mechi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jean-Jacques Ndala, alitoa penalti hiyo mwishoni kabisa mwa dakika nane za nyongeza baada ya kufanya marejeo katika VAR kwa kosa lililofanywa dhidi ya Diaz ndani ya boksi na beki wa Senegal El Hadji Malick Diouf.
Diaz, wachezaji wengine wa Morocco pamoja na benchi lao la ufundi walionekana kumshawishi kwa nguvu mwamuzi huyo wakimtaka atazame tena picha za marudio, lakini uamuzi wa mwisho wa kutoa penalti hiyo ulionekana kuwakasirisha sana Senegal na mashabiki wao.
Kocha wa Senegal, Pape Thiaw aliwaamuru wachezaji wake kutoka nje ya uwanja kama njia ya kuonyesha hawakufurahishwa na uamuzi huo.
Wakati wachezaji wengi wa Senegal wakitoka uwanjani, baadhi ya mashabiki wao waliokuwa katika sehemu ndogo ya mashabiki wageni upande wa pili wa uwanja walirusha viti na vitu vingine, na kujaribu kuingia ndani ya uwanja wa mchezo.
Hatimaye walizuiliwa na ukuta mkubwa wa polisi na walinzi, na hasira yao ikageuka kuwa furaha na mshangao mkubwa pale penalti hiyo ilipookolewa.
Awali, timu ya Senegal ilikuwa imekasirishwa na uamuzi wa mwamuzi kuikataa bao walilofunga katika dakika ya pili ya nyongeza, ambapo Abdoulaye Seck alipiga kichwa mpira ukagonga mwamba wa lango kwenye kona, kisha Ismaila Sarr akafunga kwa kumalizia mpira uliorudi.
Baada ya Diaz kukosa penalti, ilionekana kana kwamba ilikuwa jambo lisiloepukika kwa Senegal iliyopata nguvu mpya kuendelea na kufunga bao, na walifanya hivyo katika dakika ya nne ya muda wa ziada, na kuwaacha mashabiki wa nyumbani wakiwa na mshtuko katika Uwanja wa Prince Moulay Abdellah.
Licha ya Morocco kujaribu kusawazisha, Senegal ilikuwa imara na kulinda ushindi wake hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa.
Hilo ni taji la pili la AFCON kwa Senegal baada ya kutwaa kwa mara ya kwanza mwaka 2021.
Tuzo za AFCON
Mchezaji Bora- Sadio Mane (Senegal)
Mfungaji Bora- Brahim Diaz (Morocco)
Kipa Bora- Yassine Bounou (Morocco)
Tuzo ya Uungwana- Morocco