Prime
Guede, Freddy walivyobadili upepo Simba, Yanga
Dar es Salaam. Pamoja na kuanza msimu vibaya washambuliaji wawili, Freddy Michael Kouablan wa Simba na Joseph Guede wa Yanga wameonyesha kuwa wana uwezo wa hali ya juu kwenye timu hizo na sasa mashabiki wameanza kuwaelewa.
Michezo ya mwanzoni ya msimu huu, mastaa hao ambao wanacheza eneo la ushambuliaji kwenye timu zao, walipigwa vita na mashabiki wa timu zote kutokana na kushindwa kuonyesha kiwango cha juu.
Lakini kwenye michezo kadhaa ya hivi karibuni, mastaa hao wote raia wa Ivory Coast wameonyesha kuwa namba zao zinastahili kuwabeba na kubaki kwenye timu hizo.
Guede na Michael walianza kuonyesha kuwa ni wakali kwenye mchezo wa dabi ya Kariakoo uliopigwa mwezi uliopita ambapo Yanga ilishinda 2-1, ambao kila mmoja alifunga bao safi sasa wanaonekana kuwa wachezaji muhimu kwenye vikosi vyao.
FREDDY
Freddy alijiunga na Simba katika dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea Green Eagles ya Zambia ambapo hadi anaondoka alikuwa mfungaji bora akiwa na mabao 14, ambayo hadi leo hayajafikiwa na mchezaji mwingine yoyote, nyuma yake yupo Andrew Phiri wa Maestro United wenye 10 kila mmoja.
Nyota huyo alitua kwa ajili ya kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mshambuliaji wa kikosi hicho, Jean Baleke aliyeondoka na mabao manane ya Ligi Kuu Bara dirisha dogo la Januari mwaka huu na kujiunga na Al-Ittihad ya Libya.
Simba imekuwa na matatizo mengi kwenye utupiaji wa mabao kutokana na kutengeneza nafasi nyingi licha ya uwepo wa nyota washambuliaji asilia wakiongozwa na Freddy na Pa Omary Jobe walioingia dirisha dogo na mkongwe, John Bocco ambaye hayupo kikosini.
Katika mechi zao za hivi karibuni, benchi la ufundi la Simba limekuwa likimlazimisha Saidi Ntibanzokiza 'Saido' ambaye kiasili ni winga kucheza eneo la ushambuliaji lakini hajawa na matokeo chanya kama ilivyo kwa Freddy akicheza eneo hilo.
Wachezaji wengine wa Simba ambao wamekuwa wakitumiwa kwenye eneo la ushambuliaji ni Kibu Denis, Clatous Chama na Sadio Kanoute lakini namba za Freddy zinaonekana kuwazidi wote kutokana na muda aliopata uwanjani.
Saido hadi sasa amecheza mechi 20 za ligi na kuhusika kwenye mabao tisa, akifunga saba na kutoa pasi za mwisho 'asisti' mbili, ingawa hata hivyo katika mabao hayo yote saba aliyoyafunga, matano ameyafunga kwa mikwaju ya penalti na alianza na timu mwanzoni mwa msimu, lakini kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa amefunga mawili.
Kwa upande wa Kibu Denis ambaye amecheza michezo 19 ya Ligi Kuu Bara tayari amehusika na mabao manne tu akifunga moja na kutoa asisti tatu, namba ambazo sio nzuri kwa mshambuliaji huyo ambaye anamaliza mkataba wake na kikosi hicho msimu huu.
Freddy anawapiga bao wote hao kulingana na muda aliocheza na mabao aliyofunga, ambapo hadi sasa amecheza mechi 13 za ligi, huku akianza mechi nane na tano akiingia, lakini kwa ujumla amecheza kwa dakika 521 tu kwenye ligi ambao ni wastani wa michezo sita, juzi kwenye mchezo dhidi ya Namungo alicheza mechi yake wa kwanza kwa dakika tisini akiwa na timu hiyo.
Katika mashindano yote, Freddy amefunga mabao tisa, ambapo katika Ligi Kuu Bara amefunga manne, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) amefunga manne, Kombe la Muungano amefunga bao moja.
Faida kwa mshambuliaji huyo ni kugawa mabao yake kwenye mashindano yote ambayo timu yake imeshiriki, lakini akionekana kuwa na faida kubwa pamoja na kutumika muda mfupi.
JOSEPH GUEDE
Nyota huyu alitua pia dirisha dogo msimu huu akitokea klabu ya Tuzlaspor ya Uturuki, huku akiwa kwenye presha kubwa ya kuziba nafasi iliyoachwa wazi na kinara wa mabao wa kikosi hicho, Fiston Mayele aliyejiunga na miamba ya Misri, Pyramids FC.
Guede alianza taratibu pia ndani ya timu hiyo kama ilivyokuwa kwa, Freddy ila taratibu ameanza kujipata kwani mashabiki wa Yanga wameanza kumuelewa kutokana na ubora wake anaoendelea kuuonyesha kwenye kutupia mabao ya kila aina.
Katika michezo mitano kati ya minne iliyopita ya Yanga katika Ligi Kuu Bara, Guede amehusika na mabao manne akifunga mawili dhidi ya Singida Fountain Gate (Aprili 14, 2024), Simba (Aprili 20, 2024) na Coastal Union (Aprili 27, 2024).
Kiujumla amefunga mabao manne ya Ligi Kuu Bara na kuchangia moja 'asisti' huku bao la juzi la Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Tabora United likiwa la tatu na moja la Ligi ya Mabingwa Barani Afrika lililoipeleka hatua ya robo fainali, hivyo akiwa ameshafunga mabao nane kwenye michuano yote.
Katika Ligi Kuu Bara, nyota huyo amecheza kwa dakika 746 kwenye michezo yake 12 kati ya 24 iliyocheza timu nzima msimu huu.
Guede alifunga bao moja wakati timu hiyo ilipoifunga CR Belouizdad ya Algeria mabao 4-0, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Februari 24, mwaka huu hatua ya makundi na kuipeleka nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo.
Timu hii ilimaliza kundi 'D' ikiwa nafasi ya pili na pointi nane sawa na CR Belouizdad ya Algeria ila Yanga ilinufaika tu na faida ya jinsi zilivyokutana zikiwa nyuma ya mabingwa mara 11 wa michuano hiyo, Al Ahly iliyomaliza na pointi 12.
Katika msimu huu, Yanga iliishia hatua hiyo na kutolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti 3-2, baada ya michezo yote miwili iliyopigwa jijini Dar es Salaam na kule Pretoria Afrika Kusini miamba hiyo kutoka suluhu.
Inaonekana kuwa alikuwa na nafasi ya kufanya vizuri zaidi kama angeanza na timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu.
MAONI YA WADAU
Nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Zamoyoni Mogella alisema wachezaji wanaposajiliwa kiu ya mashabiki na viongozi ni kuona wanafanya vizuri wakati huohuo, jambo ambalo sio kweli kwa sababu mazingira wanayotoka na huku ni tofauti kabisa.
"Ukiangalia wamekuja katika mazingira magumu na yenye presha kwa sababu Freddy alikuja kama mbadala wa Jean Baleke sawa na Joseph Guede aliyekuja kuziba pengo la Fiston Mayele hivyo isingekuwa rahisi kwao ila taratibu wamezoea hali halisi na wanaonekana ni wachezaji wazuri sehemu tulikuwa tanawapa presha kubwa bila sababu."
Kwa upande wa aliyekuwa Kocha wa Yanga, Boniface Mkwasa alisema, sio kila mchezaji anayesajiliwa anaweza kuingia moja kwa moja kwenye mfumo wa timu kutokana na mazingira ya alipotoka kwani wengi wao huchukua hata zaidi ya msimu mzima.
"Wapo wachezaji wanasajiliwa lakini hadi msimu unaisha bado hawajaonyesha uwezo wao kama walipotoka, hii inatokea hata timu za wenzetu zilizoendelea na wanakuwa na subra juu yao japo huku kwetu ni tofauti kwani wanataka matunda ya moja kwa moja, ukiwatazama hawa wachezaji kama makocha wangekata tamaa wasingepata hiki wanachopata sasa."
Kwa upande wa kocha wa msaidizi wa Simba, Selemani Matola, anasema wachezaji wote ni wazuri, ingawa anaamini wanahitaji muda ili wazoee mazingira halisi ya soka la Tanzania.
"Kwa ujumla wote ni wachezaji wazuri, hawakuwa hapa hivyo wanatakiwa kupewa muda wa kutosha ili wazoee mazingira ya ligi yetu, nafikiri wanaweza kufanya vizuri zaidi huko mbele," alisema Matola.