Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hiki hapa kilichoiponza Crystal Palace kushushwa Europa League

Muktasari:

  • Nottingham Forest itashiriki Europa League msimu wa 2025/26, huku Palace ikishushwa kwenye Conference League.

Ndoto za Crystal Palace kucheza Europa League msimu huu zimeyeyuka baada ya Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) nchini Uswisi kuunga mkono uamuzi wa UEFA wa kuishusha klabu hiyo hadi UEFA Conference League kutokana na kukiuka kanuni za umiliki wa vilabu.

Palace iliondolewa kwenye Europa League baada ya UEFA kubaini kuwa mmiliki mwenza wa klabu na mfanyabiashara wa Marekani John Textor, alikuwa na ushawishi katika klabu mbili zilizofuzu michuano hiyo ambazo ni Crystal Palace na Lyon ya Ufaransa. Kwa mujibu wa kanuni, timu moja tu inayomilikiwa na mmiliki mmoja inaweza kushiriki, na Lyon ikapewa kipaumbele kwa kuwa ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya juu zaidi kuliko Palace.

Palace walikata rufaa CAS wakitaka uamuzi huo ubadilishwe, na nafasi yao irejeshwe kwa kuiondoa Nottingham Forest au Lyon. Walihoji kuwa Textor, kupitia kampuni yake Eagle Football Holdings, alikuwa na hisa 43% pekee hivyo hakuwa na ushawishi wa moja kwa moja kwenye maamuzi ya klabu. Pia walidai kuwa kulikuwa na upendeleo kwa vilabu vingine kama Nottingham Forest na Olympiakos zinazomilikiwa na Evangelos Marinakis ambao walichelewa kuchukua hatua za kujiepusha na mgongano huo.

Hata hivyo, CAS imekataa hoja hizo, ikisema ushahidi unaonyesha Textor alikuwa na nafasi ya ushawishi kwenye bodi za Palace na Lyon wakati wa tarehe ya tathmini ya UEFA. Mahakama hiyo pia imeeleza kuwa kanuni za UEFA ni wazi na hazitoi mwanya wa kubadilika kwa vilabu visivyokidhi masharti kufikia siku ya tathmini.

Uamuzi huu una maana kuwa Nottingham Forest itashiriki Europa League msimu wa 2025/26, huku Palace ikishushwa kwenye Conference League. Inakadiriwa Palace itapoteza hadi pauni milioni 20 (Sh68 bilioni) kutokana na kushushwa ngazi hiyo.

Hii si mara ya kwanza CAS kuunga mkono UEFA katika kesi kama hii kwani Juni mwaka huu walikataa rufaa ya Drogheda United ya Ireland, ambao pia waliondolewa Conference League kwa kukiuka kanuni za umiliki wa zaidi ya Klabu moja.