Horoya hatoki, kila dakika Simba Sh2 milioni

Muktasari:

  • Tajiri kaweka milioni 200 mezani ambazo kwa hesabu ya kawaida ndani ya dakika 90 kwenye kila dakika watakayokuwa uwanjani watalipwa Sh2.2 milioniĀ 

Dar es Salaam. Timu ya Simba imepania kurejea robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ili kuvuta mabilioni ya pesa kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF), na kuhakikisha hilo linatimia vigogo wa Msimbazi wametangaza bonasi mpya kwa wachezaji katika mchezo ujao dhidi ya Horoya ya Guinea ambao kama watashinda basi watakuwa wametoboa.

Tajiri kaweka milioni 200 mezani ambazo kwa hesabu ya kawaida ndani ya dakika 90 kwenye kila dakika watakayokuwa uwanjani watalipwa Milioni 2.2. Hapo bado ule mkwanja wa Rais Samia Suluhu haujaingia.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa Wachezaji wa kikosi hicho watawekwa kikao leo na kesho kuweka mikakati mizito pamoja na kutajiwa dau hilo ambalo mabosi akiwemo, Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya timu hiyo, Salim Abdallah 'Try Again' ambaye amewaeleza kuwa rais wa heshima na mfadhili wa timu hiyo Mohamed Dewji 'Mo' wamekubaliana. Wameongeza bonasi hilo kwenye mechi ijayo dhidi ya Horoya ambapo badala ya Sh100 milioni walizozowea sasa ni Sh200 milioni kama watashinda.

Mkwanja huo ni hamasa kuhakikisha Simba inafuzu robofainali wikiendi ijayo kwenye ardhi ya nyumbani badala ya kujiongezea ugumu kutegemea hesabu za vidole mechi za mwisho ugenini.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imeambiwa ni kwamba, Simba ambayo ilishaenda robo mara mbili, wachezaji na benchi la ufundi walikuwa wakivuta bonasi ya hadi sh 150 milioni kama wakishinda mechi za ugenini na sh 100 milioni ikitoa sare ugenini huku ushindi kwenye mechi za nyumbani wakivuta Sh100 milioni na sare kuchukua Sh50 milioni bonasi ambayo katika mechi na Horoya imepanda na sasa watakuwa wakichukua Sh200 milioni kama watashinda.

Simba hawataki kutegemea matokeo ya mechi zingine, wamepania kuhakikisha wanamaliza kila kitu wenyewe na hapo akaunti za timu hiyo zitapokea zaidi ya bilioni moja kutoka CAF ikiwa ni bonasi ya kufika robo.

CAF hutoa bonasi kwa timu shiriki kuanzia hatua ya makundi ambapo kwa msimu huu timu zote zitazofika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitapewa kitita cha dola 650,000 ambazo ni zaidi ya Sh 1.4 bilioni za Kitanzania.
Hivyo mabosi wa Simba hawataki kuukosa mkwanja huo ndio maana wamejipanga kuongeza bonasi kutoka sh 150 milioni kwenye ushindi wa nyumbani kwenda milioni 200, kiasi ambacho rasmi wachezaji watatangaziwa leo au kesho kambini. Lakini mmoja wa vigogo wa Simba amedokeza kuwa dakika za mwisho kabla ya wikiendi dau hilo linaweza kupanda zaidi kwani kuna wadau wenye mapenzi na Simba wanajipanga kimyakimya.
Hata hivyo, bonasi hiyo imeongezwa kwa ushindi tu na kama watatoa sare basi watavuta sh 50 milioni iliyozoeleka na wakifungwa basi watatoka patupu.


KILA DAKIKA 2MIL
Ukiachana na hesabu ya mgawanyo wa idadi ya wachezaji, fungu hilo lina maana kuwa kila sekunde kwa Simba kwenye mchezo huo itakuwa na jasho na damu, kwani kimahesabu inaonekana kuwa watakuwa na uhakika wa kuingiza sh 37,000 kwa sekunde moja, iwe ya mpira wa kurushwa faulo, mchezaji amedondoka au vinginevyo lakini fedha hiyo itaingia kibindoni kama watashinda.
Lakini pia dakika moja yenye sekunde 60, ndiyo wanatakiwa kuitumia vizuri zaidi kwani kwa kila dakika Jumamosi watakuwa wanaingiza milioni 2,200,000.
Hii ikiwa na maana kuwa kuanzia dakika ya kwanza hadi ya 90 itakuwa muhimu sana kwa timu hiyo kuingiza fedha na kuweka rekodi, kama fedha hizo zitagawanywa kwa kila dakika 45, inaonyesha kuwa wachezaji wa Simba wakizitumia vyema dakika za kipindi cha kwanza ambazo watakuwa wamejikusanyia shilingi milioni 100, na kipindi cha pili watakusanya 100 nyingine.
Simba imesajili wachezaji 30 kwenye michuano hii ya kimataifa na inaonyesha kuwa kama mgawanyo utakuwa sawa, maana yake kila mchezaji atakuwa na uhakika wa kuchukua shilingi milioni 6.6 kwenye dakika tisini tu za mchezo huo bila kuweka bonasi nyingine ambazo wanaweza kuzipata kutoka sehemu nyingine, huko nyuma fedha ambazo zilikuwa zinatolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Samia Suluhu Hassani kwa kila bao ambalo watafunga ni milioni 5, lakini ukiweka na wadau wengine ilifika milioni 11.


HESABU ZIKO HIVI
Nguvu yote hiyo ina malengo kwani Simba inahitaji kumaliza kazi mapema kwa Horoya kabla ya mchezo wa mwisho wa kundi C itakaporudiana na Raja Casablanca ya Morocco ugenini baada ya mwanzo Mnyama kuchapwa 3-0 nyumbani.
Hadi sasa Simba ipo nafasi ya pili kwenye kundi C na alama sita nyuma ya Raja wenye pointi 12, ambao tayari wamefuzu na kuacha msala wa nafasi moja iliyobaki kwa Simba, Horoya yenye alama nne na Vipers walio na moja ambao wao hawana nafasi hata kidogo.
Simba ikishinda mbele ya Horoya itafikisha alama tisa ambazo si Horoya wala Vipers haitazifikia baada ya mechi zake za mwisho hata kama zikishinda.
Lakini kama Simba itatoa sare na Horoya itafikisha alama saba na Waguinea hao watakuwa na tano, na mechi za mwisho Simba itacheza na Raja na watakuwa wanalazimika kushinda mchezo huo kwa kuwa Horoya watavaana na Vipers ambao hawana cha kupoteza.
Maana yake karata ya Simba ya kwenda robo fainali ipo mkononi mwa Horoya Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa.
Hata hivyo, kama itashindwa kufika robo fainali, Simba haitatoka mikono mitupu kwenye michuano hiyo kwani itapata bonasi ya dola 550,000, zaidi ya sh 1.2 bilioni za Kitanzania ambazo ni mgao wa timu zinazomaliza kwenye nafasi ya tatu na nne kwenye kundi, kutoka CAF, lakini kumbuka tageti ya Simba msimu huu ni hatua ya nusu fainali.


IKO HIVI..
Mshindi wa kwanza na wa pili kwenye kila kundi atafuzu hatua ya robo fainali na kanunu zinaonyesha kuwa kutafuta hatua ya nusu fainali, timu ambayo ilimaliza ya kwanza kwenye kundi itakutana na timu itakayomaliza ya pili.
Kama Simba watamaliza wa pili kwenye kundi lao, watakutana na kati ya vigogo watatu ambao kwa sasa wanaongoza kwenye makundi yao, Mamelodi, Waydad Casablanca au Esperance ya Tunisia na wakishinda hapo ndiyo watakwenda nusu fainali, tusubiri.