Isak aikacha Newcastle
Muktasari:
- kuna taarifa kuwa klabu kutoka Mashariki ya Kati pia zinafuatilia kwa karibu mwenendo wa mshambuliaji huyo.
Nyota wa Newcastle United, Alexander Isak, amezidi kuwa gumzo baada ya kubainika kuwa hajaungana na kikosi cha timu hiyo kilichosafiri kwenda Singapore kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya huku tetesi za kujiunga na Liverpool zikizidi kushika kasi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Mail Sport, Isak alionekana akifanya mazoezi peke yake Jumanne, hali ambayo imezua hofu kwa mashabiki wa Newcastle, licha ya klabu kudai kuwa ameachwa kwa sababu ya maumivu madogo ya paja yanayoweza kuathiriwa na safari ndefu ya ndege.
Liverpool wapo, lakini bei ni kigingi
Liverpool wanatajwa kuwa na nia kubwa ya kumnasa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25, lakini Newcastle wameweka wazi kuwa mchezaji huyo hauzwi isipokuwa kwa ofa ya zaidi ya pauni milioni 125.
Hii inakuja siku moja tu baada ya Liverpool kutangaza rasmi usajili wa Hugo Ekitike kwa dau la paundi milioni 79 (Sh247 bilioni) kutoka Eintracht Frankfurt, hatua inayozua maswali iwapo bado wataendelea kumfuatilia Isak.
Wakala wake afunguka
Wakala wake, Gonzalo Gaitán, amethibitisha kwa gazeti la Arriyadiyah la Saudi Arabia kuwa wako kwenye hatua za mwisho za kuamua mustakabali wa mchezaji huyo.
“Tupo karibu kufanya maamuzi. Tunasoma na kuchambua kila chaguo lililopo. Inawezekana tukakaribia kukamilisha hatua inayofuata kwa mchezaji, bila kufichua kama atasalia Newcastle au kuondoka,” amesema Gaitán.
Kwa mujibu wa talkSPORT, Isak pia ameweka wazi masharti ya kusaini mkataba mpya akiomba mshahara wa paundi 300,000 (Sh1 bilioni) kwa wiki, mara mbili na zaidi ya kile anachopokea sasa Sh416 milioni kwa wiki tangu asaini kutoka Real Sociedad mwaka.
Takwimu hizo zingevunja mfumo wa malipo wa Newcastle, ambao kwa sasa unamweka Bruno Guimarães kama mchezaji anayelipwa zaidi paundi160,000 sawa na Sh556 milioni kwa wiki.
Kocha mkuu Eddie Howe alifunguka baada ya kuachwa kwa Isak katika kichapo cha 4-0 dhidi ya Celtic mwishoni mwa wiki, akieleza kuwa walikubaliana mchezaji huyo asihusike kutokana na presha ya mazungumzo ya usajili.
“Nilimrudisha nyumbani. Hatukutaka akae jukwaani wakati hajacheza, huku watu wakimwangalia. Ilikuwa uamuzi wa pande zote, na Alex yupo fiti, lakini hatukutaka kumuweka kwenye shinikizo.
“Nimezungumza naye jambo la kawaida. Alex ni mchezaji bora, anapendwa na wachezaji wenzake na benchi la ufundi. Ningependa abaki, lakini ni vigumu kutoa uhakika wa asilimia 100 kwa mchezaji yeyote,” alisema Howe.
Mbali na Liverpool, kuna taarifa kuwa klabu kutoka Mashariki ya Kati pia zinafuatilia kwa karibu mwenendo wa mshambuliaji huyo, huku ofa kubwa za kifedha zikitarajiwa kuwasilishwa kabla ya dirisha la usajili kufungwa.
Pamoja na klabu yake kusisitiza haina nia ya kumuacha, hali ya sintofahamu juu ya Isak inaendelea kuwa kubwa hususani baada ya kusalia England, kufanya mazoezi uwanjani peke yake, huku masharti ya mkataba mpya yakiweka presha kwa uongozi.