Karia ajiuzulu kupisha Uchaguzi Mkuu
Rais anayemaliza muda wake, Wallace Karia.
Muktasari:
- Mkutano huo unafanyika ikiwa ni siku moja tu baada ya kutupiliwa mbali kwa ombi la zuio la uchaguzi huo lililofunguliwa na Mawakili wanne katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam.
Tanga. Wakati Mkutano Mkuu Wa Shirikisho La Soka Tanzania (TFF), ukifanyika leo Agosti 16, 2025, jijini Tanga, Rais anayemaliza muda wake, Wallace Karia ametangaza rasmi kujiuzulu.
Karia aliyeongoza TFF kwa kipindi cha miaka nane, ametangaza uamuzi huo ili kupisha uchaguzi mkuu wa kumchagua Rais na Ujumbe wa Kamati ya Utendaji unaofanyika leo.
"Kuanzia muda huu nachukua nafasi hii ya kujiuzulu rasmi ili kupisha hatua nyingine za uchaguzi mkuu kuendelea,"amesema Karia.
Baada ya tamko hilo la Karia, Wajumbe mbalimbali waliohudhuria mkutano huo walionyesha kufurahia huku wakipiga makofi na kupongeza kwa hatua iliyoonyeshwa na rais huyo anayemaliza muda wake.
Katika mkutano huo, umehudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo, Mjumbe wa Baraza la Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Souleyman Waberi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Djibouti.
Mkutano huo unafanyika ikiwa ni siku moja tu baada ya kutupiliwa mbali kwa ombi la zuio la uchaguzi huo lililofunguliwa na Mawakili wanne katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam.