Kauli ya Guardiola kuhusu Ubingwa wa EPL
Muktasari:
- Man City wapo nyuma kwa pointi tatu huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya vinara wa ligi Arsenal.
Manchester, England. Kwa mashabiki wa soka duniani, juzi zilipigwa mechi nyingi katika ligi mbalimbali, lakini lile bato kati ya Manchester City na Arsenal kwenye Ligi Kuu England ndilo lililogeuka gumzo kutokana na vita ya ubingwa ilivyo baina ya timu hizo.
Hali ikiwa hivyo, kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, amesema ushindi wao wa mabao 2-1, haujafunga mbio za ubingwa, bali umezifungua zaidi.
Baada ya mchezo, walikuwa ni Manchester City walioondoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wageni wao uwanjani Etihad, hivyo kupunguza pengo la pointi kuwa tatu, huku Man City wakiwa na mchezo mmoja mkononi. Arsenal wanaongoza wakiwa na pointi 70 baada ya mechi 33, huku Man City wakiwa nazo 67 katika mechi 32.
Wakati wa mvutano kati ya mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland dhidi ya beki wa Arsenal, Gabriel Magalhaes katika mechi ya Ligi Kuu England iliyopigwa Aprili 19, 2026.
Lakini, bato kali miongoni mwa wachezaji lilikuwa katika eneo la ushambuliaji la Man City, lililoongozwa na kinara wa ufungaji mabao katika ligi hiyo, Erling Haaland dhidi ya beki wa Arsenal, Gabriel Magalhaes, ambapo muda wote walikuwa ng'adu kwa ng'adu, kiasi kwamba baada ya siku moja ya mchezo straika huyo alisikika akisema hatawasahau mabeki wa wapinzani wao walivyombana.
Haaland alitoa maelezo hayo wakati akizungumzia bato lililokuwapo yake na Magalhaes, ambapo mvutano ulikuwa mkali na kwamba hakuamini baada ya mechi kumalizika kwamba iliisha bila majeraha.
Alisema katika tukio mojawapo lililojumuisha mgongano wa vichwa katika kuwania mpira lilimfanya kuhisi kwamba ameumia vibaya, lakini kumbe haikuwa hivyo isipokuwa hofu pekee ndiyo iliyokuwa katika fikra zake.
Mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland wakati akifunga bao la pili katika mechi ya EPL dhidi ya Arsenal katika Uwanja wa Etihad, Aprili 19, 2026.
Katika mchezo huo, Haaland na Magalhaes walivutana, kusukumana na kupigania nafasi kila wakati, na mambo yaliharibika zaidi Magalhaes alipoonekana kugongesha kichwa chake kwa Haaland katika tukio lenye utata. Licha ya ukali wake, wote walionyeshwa kadi za njano jambo lililozua mjadala mzito.
“Mechi kama hizi huwa na mipambano mingi, wengine wanaweza kuamua nani ashinde pambano. Nilifunga bao, kwa hiyo nilishinda wakati huo. Lilikuwa bao muhimu na tulishinda,” alisema Haaland.
Bao lake la dakika ya 65, ndilo lililoipa Man City ushindi, baada ya Rayan Cherki kufunga la utangulizi dakika ya 16, kabla ya Kai Havertz kusawazisha dakika ya 19.
Ikiwa Man City watashinda mechi ya kesho Jumatano dhidi ya Burnley, wanaweza kupanda kileleni kwa mara ya kwanza tangu Agosti, mwaka jana, hivyo kuifanya Arsenal iendelee kuteseka kusaka ubingwa wa ligi tangu ilipoubeba 2003-2004.
Kiungo wa Man City, Bernardo Silva wakati akimzuia mshambuliaji wa Arsenal, Kai Harvert katika pambano la Ligi Kuu England kwenye Uwanja wa Etihad. Picha na Mtandao
Hata hivyo, makocha Arteta na Pep Guardiola walikubaliana jambo moja; ushindi wa Man City wa mabao 2-1 haujafunga mbio za ubingwa, bali umezifungua zaidi, ambapo Guardiola alisema: “Nani anaongoza ligi? Sisi siyo. Hiyo mechi imetupa matumaini tu.”
Hata hivyo, mbio hizo bado ziko wazi. Arsenal wana mechi tano za Premier zilizobaki dhidi ya Newcastle, Fulham, West Ham, Burnley na Cristal Palace, pamoja na nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid. Licha ya mwezi mbaya, ndoto ya makombe mawili bado ipo hai.
Hofu kubwa kwa Arteta na wachezaji wake ni historia inayojirudia, ambapo waliwahi kuongoza ligi kwa siku 248 msimu wa 2022-23 lakini wakaachwa na Man City mwishoni. Msimu huu wameongoza kwa siku 208 hadi sasa, lakini wana hatari ya kupitwa.
Man City katika mechi sita za Premier zilizobaki, itacheza dhidi ya Burnley, Everton, Brentford, Bournemouth, Crystal Palace na Aston Villa, huku pia ikiwa na nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Southampton.