Kenya yaitungua Morocco, yaendeleza ubabe CHAN 2024
Muktasari:
- Mchezo mwingine wa kundi A utazikutanisha timu ya Taifa ya Zambia dhidi Angola.
Timu ya Taifa ya Kenya, ‘Harambee Stars’, imeendelea kuwashangaza wengi kwenye fainali za CHAN 2024 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Morocco, katika mchezo uliochezwa leo Jumapili Agosti 10, 2025 kwenye Uwanja wa Moi Kasarani, Nairobi.
Bao pekee la Harambee Stars limefungwa na Rambok Ogam katika dakika ya 38 na kuipa timu yake pointi tatu muhimu. Ushindi huu umeifanya Kenya kushinda mechi mbili kwenye mashindano haya huku ikitoka sare mara moja dhidi ya Angola.
Kwenye mchezo wa leo, Kenya ilipata pigo dakika ya 44 baada ya kiungo Chris Erambo kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kucheza rafu mbaya, lakini ilionyesha nidhamu ya hali ya juu katika kuzuia mashambulizi ya Morocco.
Kwa matokeo hayo, Kenya inabaki kileleni mwa kundi A ikiwa na pointi saba baada ya michezo mitatu, ikifuatiwa na Morocco yenye pointi tatu baada ya michezo miwili.
Mchezo mwingine wa kundi A utazikutanisha timu ya Taifa ya Zambia dhidi Angola. Kwa upande wa Zambia hadi sasa hawajaonja ladha ya ushindi baada ya kupoteza mechi yao ya kwanza dhidi ya DR Congo wakati Angola ilitoka sare mechi moja na kupoteza mara moja dhidi ya Morocco.