Klabu za Madrid zategemewa kudhibiti soka Hispania kuporomoka

Tuesday February 23 2021
klabu pic

Madrid, Hispania (AFP). "Florentino, msajili," mashabiki wa Real Madrid waliandika katika akaunti zao za Twitter kabla ya kumtaka Zinedine Zidane atume ujumbe huo kwa rais wa klabu hiyo, Florentino Perez.
Siku hiyo, ndio kwanza Kylian Mbappe alikuwa ameisambaratisha Barcelona katika uwanja wa Camp Nou, na saa 24 baadaye Erling Haaland aliifanyia hivyo Sevilla katika uwanja wa Ramon Sanchez Pizjuan.
Wakati huo, Real Sociedad ilikuwa nyuma kwa mabao 4-0 dhidi ya Manchester United, na hisia zikawa bayana kuwa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, inaporomoka.
Lakini baadaye usiku huo, Granada ikaishinda Napoli na Villarreal wakaishinda Salzburg katika michuano ambayo ni lazima ikumbukwe kwamba ni miezi sita tu iliyopita, Sevilla ilitwaa ubingwa wake kwa mara ya nne katika miaka saba.
Na kwa kweli, timu za Hispania zimetwaa ubingwa wa Ligi ya Europa mara saba kati ya 11.
Makombe matatu kati ya hayo yamechukuliwa na Atletico Madrid, ambao leo Jumanne wanakutana na Chelsea katika mechi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya kuwang'oa mabingwa wa msimu uliopita, Liverpool.
Real Madrid itakutana na Atalanta kesho, ikitegemea kuepuka kumaliza mwaka wa tatu bila ya kutwaa kombe la michuano hiyo, baada ya kushinda kwa miaka mitatu mfululizo.
"Timu za Hispania bado ni imara, ni suala la muda tu," alisema kocha wa Barcelona, Ronald Koeman wiki iliyopita. "Huwezi kuhitimisha (tu kwamba zinaporomoka)."
Kama kuna haja ya mjadala - kwamba kasi ya kuanguka inatokana na viwango vilivyofikiwa awali na klabu za nchi hiyo- ubabe wa Hispania katika soka barani Ulaya umekuwa unaanguka kwa kwa muda sasa.
Kuanguka kunaweza kuwa kulianza wakati Barcelona iliposhindwa na Roma mwaka 2018, kukaendelea wakati Neymar na Cristiano Ronaldo walipoondoka Hispania, kabla ya kuingia matatizoni wakati hali ya kifedha ilipozizuia klabu za Hispania kufufuka kiuchumi.
Ni dhahiri kwa Barcelona na Real Madrid, kusita kujenga upya vikosi vyao kumekuwa kukisukumwa kwa kiwango kikubwa na hali ya kifedha, janga la virusi vya corona likizilamisha kutotumia hata senti moja kusajili wakati wa majira ya joto wakati zikihitaji sana wachezaji.
Chipukizi wa Real Madrid bado hawajapevuka, wakati Barcelona imeshuhudia enzi ya kihistoria ikianza kusahaulika, wachezaji kuondoka au kustaafu.
Atletico Madrid inaendelea kujijenga upya baada ya kushuhudia wachezaji nyota wakiondoka. Sevilla imestahimili lakini Valencia iko matatizoni.
Kwa kipindi kirefu cha karne hii, limekuwa ni suala la vipaji vya soka kuhamia Hispania lakini sasa hakuna uhakika.
Kwa muda mrefu, Mbappe amekuwa akihusishwa na Zidane lakini, kama Lionel Messi alivyoonyesha, wachezaji bora hujihusisha na kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa na nani anaweza kusema Paris Saint-Germain na Manchester City hazitawachukua nyota hao wengi katika miaka ijayo kuliko Barcelona na Real Madrid?
Ronaldo na Neymar waliondoka, kabla ya Messi kujaribu na bado anaweza kuwa anajaribu. Mwaka jana, City ilimnasa mchezaji chipukizi anayevutia sana, Ferran Torres, wakati Atletico walishindwa hata kumzuia Thomas Partey kujiunga na Arsenal.
Na wakati Pep Guardiola na Jose Mourinho waliongoza mafanikio ya La Liga mwishoni mwa muongo uliopita, makocha wa kisasa wenye mvuto - Jurgen Klopp, Mauricio Pochettino, Thomas Tuchel na Julian Nagelsmann - wameenda kufanya kazi sehemu nyingine-- si Hispania.
Pamoja na Guardiola, wameongoza mageuzi hayo kwa kutumia mchezo wa nguvu, wa moja kwa moja, wa kubana, ambao unaonekana kuzifanya klabu za Hispania kupata shida.
"Mara nyingi Barca imekuwa timu ambayo hufuata wachezaji wengi kwa kuangalia ubora wao wa kiufundi na si nguvu," alisema Koeman Jumamosi.
"Lazima uwe navyo vyote, uwe na mizania unapotaka kucheza mpira, kucheza kuanzia nyuma na kutengeneza nafasi.
"Timu hii imecheza vizuri kwa njia hiyo msimu huu, lakini inatakiwa iwe na mizania, hiyo inaweza kuwa ni kutumia nguvu, kujilinda na kufanya mambo yote mengine. Ili kujilinda ni lazima uwe na miguu."
Chini ya yote hayo ni ukweli kuhusu hali ya kifedha, kwamba klabu za Hispania, zikiwemo hizo mbili kubwa, si walipaji wazuri wa ada ya uhamisho au mishahara.
Licha ya majaribio ya La Liga kusambaa duniani, wawekezaji kutoka nje hawakimbilii Hispania bali England, wakivutiwa na mikataba minono ya televisheni na wigo mkubwa wa watazamaji kote duniani.
Wakati Barcelona na Real Madrid zikifunga maduka kipindi cha usajili cha katikati ya mwaka jana, Chelsea na Manchester City walitumia fedha bila vikwazo, wamiliki wao ambao ni mabilionea wakiwalinda na janga la corona ambalo lilikuwa likiyumbisha klabu kila mahali.
Rais wa La Liga, Javier Tebas alisema usajili katika Ligi Kuu ya England "ulikithiri" lakini bado udhibiti a matumizi nchini Hispania unaweza kusaidia kuwepo na malipo ya faida baadaye.
"Uwezo wa kifedha wa kulipa ni muhimu sana," alisema Tebas. "Wakati janga litakapoisha, klabu zetu zitakuwa imara kama awali."
Kama kufufuka kiuchumi kutakuwa kwa haraka, kujenga upya kutachukua muda mrefu. Mbappe na Haaland hawatajiunga na klabu bora Ulaya, watakuwa kichocheo cha kurudi katika hali ya kawaida.

Advertisement