Klopp avunja ukimya kuondoka kwa Salah Liverpool
Aliyekuwa kocha wa Liverpool akizungumza na mshambuliaji wa klabu hiyo, Mohammed Salah. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Akiwa na Klopp, Salah alicheza mechi 349 na kufunga mabao 211 tangu ajiunge na klabu hiyo mwaka 2017 akitokea AS Roma.
Aliyekuwa Meneja wa Liverpool, Jürgen Klopp ameonyesha heshima kubwa kwa Mohamed Salah kufuatia tangazo lake la kuondoka katika timu hiyo mwishoni mwa msimu huu, akimtaja kuwa ni miongoni mwa wachezaji bora duniani.
Salah ametangaza wiki hii kuwa atahitimisha safari yake ya miaka tisa Liverpool, ikiwa ni miaka miwili tangu Klopp aondoke klabuni hapo.
Akizungumza akiwa England kwa ajili ya mechi ya hisani kati ya wachezaji wa zamani wa Liverpool na Borussia Dortmund, Klopp amefichua kuwa aliwasiliana na Salah kwa ujumbe mfupi na kumtakia kila la heri katika mechi zilizobaki.
“Najua anafurahia zaidi anaposhinda na kufunga. Natumaini siku ya mwisho ya msimu atakuwa na tabasamu na kujivunia kuwa sehemu ya moja ya safari bora kabisa katika soka,” amesema Klopp.
Mjerumani huyi amesema kuwa kufanya kazi na Salah ilikuwa safari yenye mafanikio makubwa.
“Ilikuwa furaha, changamoto na kazi ngumu kwa pande zote mbili, lakini matokeo yake yalikuwa ya kipekee. Alifikia viwango ambavyo vinaweza visifikiwe tena,” amesema Klopp.
Katika kipindi chake chini ya Klopp, Salah alicheza mechi 349 na kufunga mabao 211 tangu ajiunge na klabu hiyo mwaka 2017 akitokea AS Roma.
Klopp pia amegusia jinsi Salah alivyokuwa na wasiwasi mwanzoni kuhusu nafasi yake kikosini kutokana na uwepo wa Sadio Mané.
“Aliniuliza atacheza wapi. Nilimwambia winga wa kulia, akasema Mane yupo pale. Nikamwambia anaweza kwenda kushoto. Leo huwezi kulinganisha Salah wa sasa na yule wa mwanzo,” ameeleza.
Kuhusu tetesi zilizodai kuwa Klopp alimtaka zaidi Julian Brandt badala ya Salah, kocha huyo amekanusha.
“Ni kawaida kuzungumza na wachezaji wengi kabla ya kusajili. Tulizungumza na Brandt, lakini pia tulizungumza na Salah. Wakati huo tuliamini kabisa Salah ndiye chaguo sahihi,” amesema Klopp.
Klopp amehitimisha kwa kumtaja Salah kuwa sehemu ya safu bora ya ushambuliaji duniani kwa muda mrefu, akirejea ushirikiano wake na Mane ambao uliiwezesha Liverpool kutwaa mataji makubwa ikiwemo Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kuondoka kwa Salah kunatarajiwa kuacha pengo kubwa ndani ya Liverpool, huku mashabiki wakikumbuka mchango wake mkubwa uliodumu kwa karibu muongo mmoja.