Kocha Spurs amtema Richarlison

Muktasari:
- Ripoti zinaeleza kuwa hathamini mchango wa Richarlison, hasa kwa historia yake ya majeraha.
London, England. Mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil Richarlison amepokea ruhusa rasmi ya kuondoka Tottenham Hotspur majira haya ya joto, baada ya kocha mpya Thomas Frank kuamua kuwa hayumo kwenye mipango yake ya baadaye.

Richarlison, aliyesajiliwa kutoka Everton mwaka 2022 kwa dau la Pauni milioni 50, hajawahi kuonyesha ubora uliotegemewa ndani ya jezi ya Spurs, akiwa amefunga mabao 20 na kutoa pasi za mabao 10 katika mechi 90 takwimu ambazo hazijaridhisha mashabiki wala uongozi wa klabu hiyo.
Kwa mujibu wa The Sun, Tottenham sasa iko tayari kumuachia mchezaji huyo kwa dau la Pauni milioni 20 (Sh70 bilioni) tu, likiwa ni punguzo la zaidi ya nusu ya thamani ya awali, huku mkataba wake ukiwa bado unaendelea hadi mwaka 2027.

Ametemwa na kocha
Thomas Frank, ambaye ametua Tottenham akitokea Brentford kuchukua nafasi ya Ange Postecoglou, amekuwa akichambua kikosi alichorithi. Ripoti zinaeleza kuwa hathamini mchango wa Richarlison, hasa kwa kuzingatia historia yake ya majeraha, kutokuwa na ufanisi mkubwa mbele ya lango na kushindwa kuendana na kasi ya mchezo wa timu.
Katika msimu uliopita pekee, Richarlison alikosa mechi 30 kutokana na majeraha na hata alipokuwa fiti, mara nyingi alikuwa benchi huku Dominic Solanke akipewa nafasi ya kuanza na Postecoglou.

Wapi anaweza kwenda?
Kuna taarifa kuwa Galatasaray ya Uturuki imeonesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo, huku pia Everton, klabu yake ya zamani, ikitajwa kama chaguo jingine japo kocha wa sasa David Moyes haoneshi kuwa na mpango wa kumrudisha Merseyside.
Galatasaray walihusishwa pia na nia ya kumsajili Victor Osimhen wa Napoli aliyewika kwa mkopo msimu uliopita, lakini inaelezwa kwamba mchezaji huyo anaweza kuelekea klabu nyingine ya Ligi Kuu ya England, hivyo Richarlison anaweza kuwa mbadala wake.

Spurs watafuta washambuliaji wapya
Tottenham imeelekeza macho yake kwa nyota wapya wa safu ya ushambuliaji, ikiwemo Mohammed Kudus wa West Ham, ambaye ana kifungu cha kuachwa cha Pauni milioni 85 (Sh290 bilioni). Aidha, jina la Bryan Mbeumo pia limehusishwa na Spurs, japo inadaiwa kuwa Mbeumo anapendelea zaidi kutua Manchester United.
United tayari imekataliwa ofa yao ya pili kwa Mbeumo ya Pauni milioni 62.5 (215 bilioni), lakini bado wanaonekana kurudi tena mezani.