Kocha wa Diarra atimuliwa, Finidi naye kimemkuta

Muktasari:

  • Mali inashika nafasi ya nne katika msimamo wa kundi I la kuwania kufuzu Kombe la Dunia wakati Nigeria inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa kundi C.

Dar es Salaam. Matokeo yasiyoridhisha katika mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia zilizochezwa hivi karibuni yamepelekea kutimuliwa kwa makocha Finidi George wa Nigeria na Eric Chelle

Kufanya vibaya katika mechi mbili za Mali anayochezea kipa wa Yanga, Djigui Diarra katika mechi dhidi ya Ghana na Madagascar kumeshawishi Shirikisho la Mpira wa Miguu Mali, kumtimua kocha Chelle leo hii.

Juni 6, Mali ilipoteza kwa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Ghana na Juni 11 ikatoka sare tasa ugenini na Madagascar, matokeo yaliyoifanya iangukie nafasi ya nne kwenye msimamo wa kundi I linaloongozwa na Comoro yenye pointi tisa.

Sare ya bao 1-1 nyumbani na Afrika Kusini, Juni 7 na kichapo cha mabao 2-1 ugenini kwa Benin, Juni 10 ni matokeo ambayo yamegeuka mwiba kwa kocha wa Nigeria, Finidi George ambaye naye leo ametupiwa virago.

Nigeria yenye pointi tatu ilizokusanya katika mechi nne, inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa kundi C linaloongozwa na Rwanda yenye pointi saba.