Lampard aumia mkono akishangilia ushindi
Muktasari:
- Kocha wa Everton, Frank Lampard amevunjika mkono wakati akishangilia bao lililofungwa na Alex Iwobi katika dakika ya 99 na kuiwezesha kuibwaga Newcastle kwa bao 1-0 na kuipandisha juu ya timu zilizo hatarini kushuka kwa tofauti ya pointi tatu.
Liverpool, Uingereza (AFP). Kocha wa Everton, Frank Lampard amevunjika mkono wakati akishangilia bao lililofungwa na Alex Iwobi katika dakika ya 99 na kuiwezesha kuibwaga Newcastle kwa bao 1-0 na kuipandisha juu ya timu zilizo hatarini kushuka kwa tofauti ya pointi tatu.
Sakata lililotokea kipindi cha pili lililosababishwa na mtu aliyeenda kujifunga shingo katika mwamba wa goli pamoja na kuangalia VAR kulikosababisha Allan aonyeshwe kadi nyekundu, kulimanisha kulikuwa na dakika 14 za majeruhi za mechi hiyo iliyofanyika Goodison Park.
Na walikuwa vijana wa Lampard waliotumia vizuri muda huo wakati Dominic Calvert-Lewin aliposhirikiana na Iwobi ambaye alifunga bao muhimu katika maisha yake Everton tangu anunuliwe kwa pauni milioni 40 za Kiingereza akitokea Arsenal miaka mitatu iliyopita.
"Nimevunjika mkono wangu wakati wa shangwe," alisema Lampard, akionyesha mchubuko mkubwa katika mkono wake wa kushoto.
Ukiwa ushindi wa pili katika mechi 12 za ligi, shangwe zilikuwa lazima baada ya mchezo kuisha huku kukiwa na uwezekano wa athari za kifedha kwa Everton iwapo itaporomoka.