Leicester yatangaza kuachana na Ruud van Nistelrooy
Muktasari:
- Kabla ya kujiunga na Leicester, Van Nistelrooy alikuwa msaidizi wa muda katika benchi la Man United baada ya kufukuzwa kwa Erik ten Hag.
Baada ya ukimya na minong’ono mingi kuhusu hatma yake, Leicester City hatimaye imethibitisha kuachana na kocha wa Kiholanzi, Ruud van Nistelrooy, hatua inayokuja siku chache kabla ya wachezaji kurejea kambini kwa maandalizi ya msimu mpya wa Championship.
Taarifa hiyo imekuja licha ya ukweli kwamba kushuka kwao daraja kulithibitishwa rasmi Aprili 20, baada ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Liverpool ikiwa ni kichapo chao cha tisa mfululizo nyumbani bila kufunga bao.
Kwa mujibu wa Daily Mail, sababu ya kuchelewa kwa tangazo hilo inatajwa kuwa ni hofu ya kuvunja kanuni za matumizi ya fedha (FFP), kwani fidia ya kuachana na Van Nistelrooy imepangwa kuingizwa kwenye vitabu vya fedha vya mwezi ujao hivyo kuzuia klabu kuweka malipo ya makocha wawili katika kipindi kimoja cha fedha kinachomalizika Juni 30.
Van Nistelrooy, ambaye alichukua nafasi ya Steve Cooper mwezi Novemba 2023 kwa mkataba hadi 2027, aliiongoza Leicester katika mechi 27, akishinda tano pekee na kupoteza 19 matokeo yaliyoisukuma klabu hiyo kuangukia Ligi ya Championship.
Licha ya kushindwa kufanikisha malengo, Leicester wameeleza kuwa kuachana naye kumeafikiwa kwa makubaliano ya pande zote na kumpongeza kocha huyo kwa uaminifu na kujituma kwake kwa dhati.
Kwa sasa, maandalizi ya msimu mpya yataongozwa na benchi lililobaki, linaloongozwa na Andy King mchezaji wa zamani wa Leicester aliyeisaidia kutwaa ubingwa wa EPL mwaka 2016 ambaye anatajwa kuwa mmoja wa wanaoweza kupewa mikoba kwa muda mfupi.
Wakati huohuo, majina ya Sean Dyche aliyekuwa kocha wa Everton na Danny Rohl ambaye ni kocha wa Sheffield Wednesday wanatajwa kuchukua mikoba ya kudumu, hasa kutokana na historia yao ya kufanya kazi na mkurugenzi wa kiufundi wa Leicester, Martyn Glover.
Van Nistelrooy ametoa tamko la kuwaaga mashabiki akisema:
“Ningependa kuwashukuru wachezaji wa Leicester, benchi la ufundi, vijana wa akademi na wafanyakazi wote kwa taaluma na kujituma wakati wote niliokuwa hapa. Nashukuru pia mashabiki kwa sapoti yao na kuitakia klabu mafanikio mema huko mbele.”
Zaidi ya matatizo ya uwanjani, Leicester pia wanakabiliwa na tishio la kupokonywa pointi kutokana na kuvunja kanuni za faida na uendelevu (PSR) katika msimu wa 2023/24. Hatua hiyo inaweza kuwaathiri zaidi wanapoanza maisha mapya katika Championship.
Aidha, Mdhamini mkuu wa Leicester City, King Power anakumbwa na matatizo makubwa ya kifedha. Mkurugenzi Mtendaji mpya, Nitinai Sirismatthakarn, amekiri kuwa kampuni hiyo inayotegemea kwa kiasi kikubwa mapato kutoka biashara ya bidhaa zisizotozwa kodi (duty free) viwanja vya ndege nchini Thailand, sasa iko katika hali ngumu kiuchumi.
“Ni kama mgonjwa anayevuta oksijeni. Tumewaomba AOT (Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Thailand) waondoe oksijeni hiyo maana hatuwezi tena. Huo ndiyo ujumbe tuliotuma,” amesema Sirismatthakarn kwa kusisitiza ukubwa wa changamoto hiyo.
Kwa sasa, macho yote yapo kwa uongozi wa Leicester kuona kama wataweza kuipanga upya timu yao na kumrudisha klabuni kocha mwenye maono sahihi ya kuwarejesha Ligi Kuu, huku wakikwepa vikwazo vya kifedha na matatizo ya ndani.