Man United, Arsenal zamgombea Sane
Muktasari:
- Leroy Sane ni mtoto wa kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, Souleymane Sane ambaye pia amewahi kuichezea timu ya taifa ya Senegal.
Londond. Arsenal na Manchester United zimeanza mikakati ya kuwania saini ya winga wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Leroy Sane.
Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta anataka kumsajili Sane akiamini kuwa ataongeza ubora katika timu yake katika nafasi ya winga.
Kana kwamba haitoshi, Arsenal inamtazama Sane kama mchezaji sahihi ambaye ataongeza ushindani kwa winga wake wa kulia, Bukayo Saka ambao utakuwa na faida chanya kwa timu.
Ruben Amorim ambaye ameanza kibarua cha kuinoa Manchester United wiki hii, naye inaripotiwa kuwa ameuambia uongozi wa timu yake uanze harakati za kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28.
Mkataba wa Sane na Bayern Munich utafikia tamati Juni 30, 2025 na hadi sasa klabu yake haijaonyesha mpango wowote wa mazungumzo ya mkataba mpya jambo ambalo linamuweka mchezaji huyo katika uwezekano mkubwa wa kuondoka baada ya kutumikia timu hiyo ya Ujerumani kwa miaka minne.
Bayern Munich inaripotiwa kuwa katika mpango wa kupunguza gharama za mishahara kwa wachezaji wake ikiwemo kuwauza au kuwalazimisha wakubali punguzo katika mikataba mipya.
Hilo linaonekana kuwa gumu kwa Sane ambaye kwa sasa anapokea kiasi cha Pauni 16.6 milioni na ili abaki anatakiwa akubali kulipwa kiasi cha Pauni 12.4 milioni.
Msimu huu unaonekana kuwa mgumu kwa Sane kutokana na dakika chache za kucheza ambazo amekuwa akipata chini ya kocha Vincent Kompany jambo ambalo linaweza kumshawishi zaidi kuchukua uamuzi wa kuondoka.
Sane amecheza mechi 11 za Bayern Munich za mashindano tofauti msimu huu kwa dakika 386 ambazo ni wastani wa dakika 35 tu kwa mchezo.
Uwepo wa mawinga Michael Olise, Serge Gnabry na Kingsley Coman unaonekana kuongeza zaidi ugumu kwa Sane kupata nafasi ya kutosha ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Bayern Munich na haionekani kama anaweza kukataa ofa nzuri ya kujiunga na timu nyingine msimu huu.