Marefa Tanzania wapewa shavu FIFA

Muktasari:

  • Arajiga alichezesha mechi mbili za watani wa jadi kwenye Ligi Kuu msimu huu ambazo zote Yanga iliibuka na ushindi dhidi ya Simba.

Dar es Salaam. Marefa wanne wa Tanzania, wameteuliwa kuchezesha mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia katika kundi H baina ya Malawi na São Tomé na Principe utakaochezwa Juni 6 mwaka huu jijini Lilongwe kwenye Uwanja wa Bingu.

Mchezo huo umepangwa kuchezwa saa 9:00 alasiri kwa muda wa Malawi ukiwa ni wa raundi ya tatu.

Katika uteuzi huo, Ahmed Arajiga ameteuliwa kuwa mwamuzi wa kati ambapo atasaidiwa na Frank Komba na Kassim Mpanga.

Mwamuzi wa kimataifa wa Tanzania, Hery Sasii yeye ameteuliwa kuwa mwamuzi wa akiba katika mchezo huo.

Waamuzi hao watakuwa wakifanyiwa tathmini na Kouame N’Dri wa Ivory Coast ambaye ameteuliwa kuwa mtathmini wa waamuzi katika mchezo huo.

Ukiondoa hao, FİFA pia imemteua Suleiman Awuye kutoka Uganda kuwa kamishina wa mechi hiyo.

Malawi katika mechi mbili zilizopita za kuwania kufuzu Kombe la Dunia katika kundi hilo, ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Liberia kisha ikapoteza mbele ya Tunisia kwa bao 1-0.