Mashujaa wa rekodi mara mbili Afcon

Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakiwa na furaha baada ya Taifa lao kutinga fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2023), Taifa Stars imeandika rekodi ya kufuzu kushiriki fainali hizo kwa mara ya tatu.

Mara ya kwanza Tanzania kufuzu ilikuwa 1980, ikiwa chini ya kocha Joel Bendera (sasa marehemu), ikafuzu tena 2019 chini ya Mnigeria, Emmanuel Amunike na sasa imefuzu ikiwa chini ya raia wa Algeria, Adel Amrouche.

Katika kampeni hizo, Tanzania ilipangwa Kundi F pamoja na Uganda, Niger na Algeria. Mchezo wa mwisho dhidi ya Algeria, uliochezwa Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa 19 May 1956, nchini humo, Tanzania ilihitaji ushindi au sare yoyote kufuzu na hadi dakika 90 zinakamilika, timu hizo hazikufungana, matokeo ambayo yalikuwa ni furaha kwa kila Mtanzania.

Tanzania imemaliza kundi hilo ikiwa nafasi ya pili kwa pointi nane nyuma ya vinara Algeria waliomaliza na pointi 16, Uganda ilimaliza wakiwa nafasi ya tatu kwa pointi saba na Niger ikiburuza mkia ikiwa na pointi mbili.

Katika kampeni hizo, Tanzania ilishinda michezo miwili, ilitoka sare michezo miwili na kupoteza michezo miwili wakati ikifunga mabao matatu na kufungwa mabao manne.

Katika kikosi cha wachezaji 25 waliokuwa wameitwa kucheza mchezo wa mwisho dhidi ya Algeria, ni wachezaji nane pekee ambao wameandika rekodi ya kuipeleka Tanzania kwa mara ya pili katika mashindano hayo.

Katika kampeni za 2019, mchezo wa mwisho wa makundi Tanzania ilicheza dhidi Uganda na ushindi wa mabao 3-0 ulitosha kuivusha Taifa Stars hadi AFCON za 2019.


Metacha Mnata

Mlinda mlango wa Yanga, Metacha Mnata alikuwepo katika kikosi cha timu ya Taifa kilichoitwa kucheza mchezo wa mwisho wa makundi dhidi ya Uganda.

Wakati huo, Metacha alikuwa ndiye kipa namba moja katika kikosi cha Mbao FC ya Mwanza. Metacha ambaye ana miaka 24, baada ya kutoka Mbao, akajiunga na Tanzania Prisons, alipokaa kwa miezi 12 kabla ya kusajiliwa na Yanga.

Agosti 2021, Metacha alijiunga na Polisi Tanzania kabla ya kutimkia Singida Big Stars, Julai mwaka jana na Januari mwaka huu akarejea tena Yanga.


Kennedy Juma

Mlinzi huyo wa kati wa Simba, Kennedy yupo katika rekodi hiyo baada ya kuitwa katika kikosi hicho kilichoivaa Algeria, wiki iliyopita.

Tanzania ilipofuzu 2019, Kennedy alikuwa anakipiga katika kikosi cha Singida Big Stars (kwa sasa Singida Fountain Gate). Kennedy mwenye miaka 29, hana rekodi kubwa katika soka, alianzia kucheza soka la ushindano katika kikosi cha Singida kabla ya kusajiliwa na Simba Julai, 2019.


Jonas Mkude

Kiungo mkabaji wa Yanga, Mkude, ameingia katika rekodi hiyo kutokana na kuwepo katika kikosi kilichoipeleka Tanzania AFCON ya 2019 na mwaka huu.

Taifa Stars ilipofuzu 2019, Mkude alikuwa katika kikosi cha Simba, ambayo alidumu nayo kwa miaka 13, akianzia kucheza katika kikosi cha timu ya vijana. Mkude mwenye miaka 30, pia hana rekodi kubwa katika soka, alianzia Simba tangu 2011 kabla ya Julai mwaka huu kujiunga na Yanga.


Mudathir Yahya

Kiungo mshambuliji wa Yanga, Mudathir, yupo katika rekodi hiyo na 2019 alikuwa anaichezea Azam FC. Nyota huyo mwenye miaka 27, pia anacheza nafasi ya kiungo mkabaji na kiungo wa kati.

Mudathir alianzia kucheza soka katika klabu ya Azam FC 2012, kabla ya kujiunga na Singida Big Stars 2017 na 2018 akarejea Azam FC. Julai mwaka jana akaachana na klabu hiyo na kurejea kwao Zanzibar kabla ya Yanga kumsajili katika dirisha dogo Januari, mwaka huu.


John Bocco

Mshambuli na nahodha wa Simba, Bocco, ameingia katika rekodi hiyo kutokana na kuwepo katika vikosi vyote viwili.

Bocco mwenye miaka 34, hana rekodi kubwa katika soka, amecheza katika klabu mbili tu Tanzania. Nyota huyo alianzia soka lake la ushindani akiwa Azam FC 2007 na alidumu kwa miaka 10, kabla ya 2017 kujiunga na Simba ambayo anaichezea hadi sasa.


Saimon Msuva

Mshambuli anayekipiga katika kikosi cha JS Kabylie ya Algeria, Saimon Msuva, ndiye kinara wa kutupia mabao katika kikosi cha Tanzania kilichofuzu fainali za AFCON mwaka huu.

Msuva naye yupo katika rekodi hiyo, katika fainali za 2019, Msuva alikuwa anakipiga katika kikosi cha Difaa El Jadida ya Morocco. Katika Kundi F, ambalo Tanzania ilipangwa katika kampeni za mwaka huu, Msuva amefunga mabao mawili sawa na nyota wa Niger, Daniel Sosah, wakitanguliwa na raia wa Algeria, Mohammed Amoura ambaye alifunga mabao matatu.

Kabla ya kutua katika kikosi cha JS Kabylie mwezi uliopita, Msuva alipita katika klabu za Moro United, Azam FC, Yanga, Difaa El Jadida, Wydad AC na Al-Qadsiah FC.


Himid Mao

Kiungo mkabaji, Himid Mao, anayekipiga katika kikosi cha Talaea El Gaish ya Misri, wakati Taifa Stars inafuzu AFCON 2019 alikuwa anakipiga katika kikosi cha Project ya Misri.

Mao mwenye miaka 30, alianza kucheza soka la ushindani katika kikosi cha Azam FC mwaka 2009 kabla ya mwaka mwaka 2018 kujiunga na kikosi cha Project. Nyoya huyo hajarejea kucheza Tanzania na ameendelea kukipiga nchini Misri akipita katika klabu za Enppi, Entag El Harby na El Mahalla.


Mbwana Samatta

Nahodha timu ya Taifa, Samatta, ameweka rekodi ya kuwa nahodha wa vikosi viwili ambavyo vimefuzu kushiriki AFCON 2019 na mwaka huu.

Samatta mwenye miaka 30, kwa sasa anaichezea klabu ya Paok FC ya Ugiriki na amekuwa bora tangu 2011 alipokuwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), alipoitwa katika kikosi cha Taifa Stars kwa mara ya kwanza.

Samatta alianzia soka katika kikosi cha African Lyon na amepita Simba, TP Mazembe, KRC Genk na Royal Antwerp za Ubelgiji, Fenerbahce ya Uturuki na Aston Villa ya England.


Kikosi cha Stars cha 2023:

Beno Kakolanya (Singida BS), Metacha Mnata (Yanga), Erick Johora (Geita Gold), Ibrahim Hamad, Bakari Mwamnyeto (Yanga), Mzamiru Yasin (Simba), Sospeter Bajama (Azam), Clement Mzize (Yanga), Kibu Deins(Simba), Himid Mao (Tala’EA Gaish Misri), Mudathir Yahya (Yanga) na Abdul Seleman (Azam).

Wengine ni Abdulmalik Zakaria(Namungo), John Bocco, Kennedy Juma(Simba), Lameck Lawi(Coastal Union), Jonas Mkude (Yanga), Morice Abraham (FK Sportak Subotic, Seribia), Haji Mnoga (Aldershot united, Uingereza), Ben Starkie (Basford United, Uingereza), Saimon Msuva (JS Kabylie, Algeria), Novatus Dismas (Zulte Waregem, Ubelgij), Mbwana Samatta(Paok FC, Ugirik) na Abid Banda (Richard Bay F.C, Afrika Kusini).


Kikosi cha Stars 2019

Aishi Manula (Simba), Feisal Salum (Yanga), Hassan Kessy (Nkana-Zambia), Yahya Zayd (Ismaily-Misri), Gadiel Michael (Yanga), Himid Mao (Petrojet-Misri), Mudathir Yahya (Azam FC), Shaaban Chilunda (Tenerife-Hispania), Kelvin Yondan (Yanga), Shiza Ramadhan (ENPPI-Misri), Andrew Vicent (Yanga), Kennedy Wilson (Singida United) na Aggrey Morris (Azam FC).

Wengine ni Simon Msuva (El Jadida-Morocco), Rashid Mandawa (BDF-Botswana), Jonas Mkude (Simba), Mbwana Samatta (KRC Genk-Belgium), Thomas Ulimwengu(JS Saoura-Algeria), Mechata Mnata (Mbao FC), Aron Kalambo (Tz Prisons), Suleiman Salula (Malindi FC-Zanzibar), Vicent Phillipo (Mbao FC), John Bocco (Simba), Farid Mussa (Tenerife-Hispania)na Ally Mtoni aliyekuwa Lipuli, sasa ni marehemu.