Mbrazil Simba aitaka Yanga

KIKOSI cha Simba jana kimeanza mazoezi Dubai kwa ajili ya kambi ya wiki moja kujiandaa na mechi za Ligi Kuu Bara na ile ya kimataifa, huku kocha mkuu mpya, Roberto Oliveira 'Robertinho' akisema anafahamu kila kitu kuhusu Yanga na kutamba hana presha nao kabisa.
Kocha huyo aliyetambulishwa mapema wiki hii kabla ya kuwahishwa Zanzibar kushuhudia Simba ikicheza mechi mbili za michuano ya Kombe la Mapinduzi na kung'olewa mapema pamoja na kulitema taji ilililokuwa ikilishikilia kabla ya kuwataka wachezaji wote kambini ili kuwalisha madini.
Akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya kurejea kutoka Zanzibar, kocha huyo Mbrazili alifichua analijua soka la Tanzania na amekuwa akilifuatilia kwa ukaribu tangu akizinoa Rayon Sports ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya na Vipers ya Uganda, hivyo anajua kila kitu kuhusu wapinzani na wataji wa jadi wa klabu aliyojiunga nayo, yaani Yanga.
Robertinho alisema anafahamu kuna ushindani mkubwa kwa michuano ya ndani ikiwemo upinzani wa timu yake ya sasa Simba dhidi ya Yanga kila zinapokutana na hata upinzani wa timu nyingine na kwamba alishajiandaa mapema kukabiliana nao hata kabla ya kuja kujiunga Msimbazi.
Kocha huyo mwenye falsafa za kujilinda na kushambulia kwa pamoja mwanzo mwisho, alisema kwa  bahati nzuri Yanga anaifahamu hata kabla ya kuja Simba na aliwahi kuifunga mara kadhaa alipokutana nao tangu akiwa  Rayon Sports ya Rwanda na hata msimu huu waliitungua kwenye kilele cha Tamasha la Wiki ya Mwananchi lililofanyika Agosti 6 mwaka jana.
"Naamini kuwepo wangu hapa nchini, unaifanya nitafahamu zaidi vitu vingi mbali ya wapinzani wetu Yanga, kwani imani yangu Simba itakuwa bora zaidi dhidi yao ikiwemo kupata matokeo bora kwa mechi zinakuja na hata kwenye ushindani dhidi ya wapinzani wengine," alisema Robertinho na kuongeza;
"Najua Yanga ina kikosi kizuri, tofauti na kile kilichoshiriki Mapinduzi, lakini bado hainipi shida kwangu kwa kushirikiana na wenzangu niliowakuta (Juma Mgunda na Seleman Matola pamoja na mchambuzi wa mechi, Culvin Mavunga) kila kitu kitaenda sawa na Simba itafanya vizuri zaidi."
Kuhusu ujio wa kocha msaidizi kutoka Tunisia, Oussama Sellami ili ashirikiane pamoja kwa lengo la kuboresha benchi la ufundi kuwa imara zaidi.
"Tumemleta kocha mwingine msaidizi kwani nimewahi kufanya nae kazi namfahamu vizuri uwezo wake naamini atakwenda kuongeza ubora kwa wachezaji," alisema Robertinho aliyefichua juu ya dili lake na Yanga kabla ya kuangukia Simba na kufichua ameitisha kikao cha dharura na mabosi wake ili kuwapa mpango kazi wake na namna atakavyofanya kazi na mastaa aliokutana nao wakiwa Dubai.
"Unajua kabla ya kuja Simba niliwahi kufikia hatua nzuri kimazungumzo na Yanga ila mambo fulani ya msingi hayakwenda sawa, ndio maana nilishindwa kujiunga nao mwanzoni mwa msimu huu.
"Naamini nafasi hii kubwa niliyopata kuifundisha Simba ni fursa ya kuonyesha kwamba timu inakwenda kuwa bora kwenye mashindano ya ndani ili kuchukua mataji pamoja na yale ya kimataifa. Yaliyotokea Mapinduzi sio muda wake sasa, kwani wakati huu kazi kubwa ni kutengeneza Simba imara kwenye benchi la ufundi na wachezaji ili kufikia malengo iliyojiwekea."