Mbrazili Simba aanza na straika, kiungo fundi

Muktasari:

  • Taarifa kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa, Robertinho na mabosi zake wamekubaliana kuongeza mashine mbili mpya kiungo mkabaji  na straika mwenye uwezo wa kufunga ili kuja kuongeza makali ya kikosi hicho.

KOCHA wa Simba, Mbrazil Roberto Oliveira 'Robertinho' ameweka bayana kwamba alichokiona Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi na kupitia mafaili ya wachezaji wengine wa kikosi cha kwanza, analazimika kuvuta wachezaji wawili wa kukikiimarisha kikosi hicho.
Robertinho alisimamia mazoezi ya pamoja na wachezaji wa Simba timu hiyo ikiwa Dubai katika kambi ya wiki moja iliyogharamiwa na bilionea na Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohamed  'Mo' Dewji kwa ajili ya kupata muda wa kutosha na utulivu wa kufanya maandalizi.
Taarifa kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa, Robertinho na mabosi zake wamekubaliana kuongeza mashine mbili mpya kiungo mkabaji  na straika mwenye uwezo wa kufunga ili kuja kuongeza makali ya kikosi hicho.
Katika kuhakikisha hilo linakamilika mabosi wa Simba na Robertinho wameingia sokoni kutafuta wachezaji wawili wa kigeni wenye uwezo mkubwa wa kucheza nafasi hizo mbili kabla ya dirisha la usajili lililobakisha siku sita kufungwa wapatikane.
Awali kwenye straika Simba ilikuwa na mpango wa kumleta nchini, Kwame Opoku ila nyota huyo amemua na mawazo yamebadilika na sasa anatafutwa mwingine kwenye kiungo wa ukabaji yupo pia mzawa, Kelvin Nashon aliyetua Singida Big Stars.
Simba inahitaji kiungo wa ukabaji ili kuongeza nguvu eneo hilo ambalo kwa sasa anatumika zaidi Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute ikitokea mmoja wapo amekosekana kumekuwa hakuna utulivu kwenye eneo hilo.
Wakati huo huo Simba inahitaji straika mwenye uwezo wa kufunga ila kuongeza nguvu pamoja na John Bocco mwenye mabao tisa ila kuna wakati amekuwa akikosekana kutokana na sababu mbalimbali na kutumika, Moses Phiri mwenye mabao kumi si straika asili na anamajeraha.
Simba kama itafanikiwa kumpata mchezaji mpya wa kigeni kama malengo yao yalivyo maana yake italazimika kutoa kwa mkopo au kuachana nao waliyopo kikosini kwani sheria ya ligi inahitaji 12 na wapo tayari.
Robertinho alisema ameiona timu kwenye Mapinduzi na atapata muda wa kufanya nayo maandalizi ingawa si wachezaji wote kwani wengine watakosekana kwa sababu mbalimbali ikiwemo za kiafya.
"Wachezaji wote wa Simba nawafahamu niliyokuwa nao kikosini hata wale wasiyokuwepo kwani kabla ya kuja kufanya kazi hapa nilitenga muda wa kutosha kuifuatilia timu na kubaini vitu vingi," alisema Robertinho na kuongeza;
"Kuna vitu vya kiufundi tunakwenda kuvifanyia kazi kuanzia kwenye kambi yetu hii ya Dubai ili timu iweze kufanya vizuri kwenye mashindano yote miongoni mwa mipango yetu kama tutafanikiwa kuna maeneo tutaongeza nguvu kwa kuleta wachezaji wapya."