Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MC Alger yaitibulia Yanga kwa Mokwena

Muktasari:

  • Mabingwa wa Algeria MC Alger wamejitokeza katika harakati za kumsajili kocha wa Afrika Kusini, Rulani Mokwena, ambaye kwa muda amekuwa akihusishwa na Yanga.

Algiers, Algeria. Kocha wa zamani wa Wydad Casablanca, Rulani Mokwena, ameripotiwa kuwa kwenye orodha ya makocha wanaowaniwa na klabu ya MC Alger, ambao ndiyo Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Algeria (Ligue 1), likiwa ni pigo kwa Yanga iliyokuwa inamwania.

Hivi karibuni tetesi zilisema kuwa Yanga inamtaka kocha huyo wa zamani wa Wydad ikiwa inaelezwa kuwa mwishoni mwa msimu huu itaachana Miloud Hamdi aliyeipa makombe matatu msimu huu.

Kwa mujibu wa jarida la El Djazaïr El Djadida, MC Alger inayojulikana pia kama The People’s Club iko mbioni kutangaza kocha mpya baada ya kuondoka kwa Khaled Ben Yahia, ambaye mkataba wake wa miezi sita ulifikia tamati mwishoni mwa msimu uliopita.

MC Alger, ambayo imetwaa mataji mawili mfululizo ya Ligi na Kombe la Taifa, inajipanga sasa kwa mashindano ya kimataifa, jambo ambalo limepelekea uongozi wa klabu hiyo kuangalia makocha wa daraja la juu barani Afrika.


Mokwena aingia kwenye orodha

Rulani Mokwena (38), ambaye awali alihusishwa na vilabu vikubwa vya Misri vya Zamalek na Pyramids FC, anatajwa kuwa miongoni mwa makocha watatu waliopo kwenye orodha ya MC Alger. Wengine ni raia wa Ufaransa, Patrice Carteron kocha wa zamani wa TP Mazembe na Al Ahly pamoja na Hubert Velud, ambaye pia ana uzoefu mkubwa barani Afrika.

Licha ya kipindi kigumu kilichomkumba Mokwena akiwa Wydad, ambapo alishindwa kukidhi matarajio ya mabosi wa Casablanca, kocha huyo bado anaheshimika kutokana na mafanikio aliyoyapata akiwa na Mamelodi Sundowns nchini Afrika Kusini, ambapo aliongoza kikosi hicho kutawala soka la ndani na kutikisa Afrika kwa mtindo na uchezaji wa kuvutia.


MC Alger kuandika historia

Uongozi wa MC Alger umedhamiria kuongeza hadhi ya klabu hiyo Kimataifa, hasa baada ya kutwaa mataji ya nyumbani. Wanasaka kocha mwenye maono mapana, uzoefu wa soka la Afrika, na uwezo wa kubeba presha ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa sasa, jina la Mokwena linazidi kushika kasi miongoni mwa mashabiki wa MC Alger, huku baadhi yao wakimtaja kama chaguo sahihi kwa ajili ya kulirejesha jina la klabu hiyo kwenye ramani ya mafanikio ya Kimataifa.


Yanga ilivyotibuliwa

Katika kile kinachoonekana kuwa pigo kwa matajiri wa Jangwani, Yanga SC, kutaka kumnasa kocha huyo, taarifa kutoka Algeria zinaeleza kuwa MC Alger wameanza mazungumzo ya moja kwa moja na kocha huyo na tayari wamemuweka kwenye orodha yao ya juu ya makocha wanaowania nafasi ya ukocha mkuu, hatua inayoweza kuwatibulia kabisa Yanga mipango yao.

Uamuzi wa MC Alger kuingia kwenye mbio hizo unakuja wakati Mokwena akiwa bado hajatangaza rasmi klabu atakayofundisha msimu ujao, huku ikielezwa kuwa ofa ya kifedha na mipango ya klabu hiyo ya Algeria inaweza kumshawishi zaidi ikilinganishwa na pendekezo la Yanga.

Hali hiyo inaiweka Yanga kwenye njiapanda kwani Mokwena alikuwa miongoni mwa majina yaliyokuwa kwenye orodha ya juu ya mabosi wa klabu hiyo, wakimtaja kama kocha mwenye falsafa ya kisasa, uzoefu wa soka la Afrika na uwezo wake wa kimbinu.

Iwapo atajiunga na MC Alger, hii itakuwa klabu yake ya tatu barani Afrika nje ya Afrika Kusini, jambo litakaloendeleza jina lake kama mmoja wa makocha chipukizi wa Kiafrika wanaopaa kwa kasi.