Mechi za wakubwa zinapigwa huko

Muktasari:
- Botafogo kwa bao 1-0 baada ya muda wa ziada itakutana na Chelsea kwenye robo fainali.
Michuano ya Kombe la Dunia kwa klabu inayoendelea huko Marekani imefikia patamu ambapo sasa zimebakia timu nane zinazopambana kuanzia leo kutafuta tiketi ya kwenda nusu fainali kutoka robo fainali.
Hapa chini kuna uchambuzi, rekodi na mambo muhimu ya kufahamu kwa kila mechi ya robo fainali ya michuano hiyo.
Robo fainali ya kwanza itakuwa kati ya Fluminense na Al-Hilal mchezo ambao utakuwa unazikutanisha timu hizo kwa mara ya kwanza.
Al-Hilal imepata imejizolea sifa tele baada ya kuichapa Manchester City mabao 4-3 katika hatua ya 16 bora licha ya ubora wa timu hiyo.
Hata hivyo, wapinzani wao Fluminense pia walifika hatua hiyo baada ya kuindoa Inter Milan kwa kichapo cha mabao 2-0 kwenye mchezo wa 16 bora.
Timu itakayopiga katika mechi hii itakutana na mshindi kati ya Palmeiras na Chelsea. Mchezo huu utapigwa leo saa 4:00 usiku.
Palmeiras ambayo ilimaliza nafasi ya pili katika Kundi A, ikishinda mechi moja na kutoka sare mbili kisha katika hatua ya 16 bora, iliichapa Botafogo kwa bao 1-0 baada ya muda wa ziada itakutana na Chelsea kwenye robo fainali.
Mchezo huu unaonekana kuwa unaweza kuwa wa kisasi kwa Palmeiras ambao walipoteza katika mchezo wa fainali ya michuano hii mwaka 2022 kwa mabao 2-0.
Licha ya ubora wao, Palmeiras wanakabiliwa na changamoto ya kuwakosa wachezaji wao muhimu wawili ambao ni Kapteni Gustavo Gomez ambaye anatumikia adhabu ya kadi za njano mbili alizoonyeshwa katika mechi tofauti, pia beki wa kushoto Joaquin Piquerez atakosekana kutokana na adhabu.
Wapinzani wao Chelsea, walianza kwa kupoteza 3-1 dhidi ya Flamengo, lakini walijirekebisha kwa kushinda mechi tatu mfululizo, ikiwa ni pamoja na ushindi wa 4-1 katika 16 bora dhidi ya Benfica.
Hata hivyo, matajiri hawa wa London pia watawakosa wachezaji wao muhimu ikiwemo kiungo Moises Caicedo atakayekosekana kutokana na kadi ya njano, lakini itapata ahueni kwa urejeo wa mshambuliaji wao Nicolas Jackson, mchezo huu utapigwa katika dimba la Camping World, huko Orlando.
Upande mwingine vigogo wa Ulaya, wamekutanishwa wenyewe kwa wenyewe, PSG ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya itakutana na mabinga watetezi wa Bundesliga, Bayern Munich kesho kuanzia saa 1:00 usiku.
Mchezo huu ambao utapigwa katika dimba la Mercedes-Benz Stadium, Atlanta mshindi atakutana na mbabe wa mechi kati ya Real Madrid na Borussia Dortmund ambayo pia inasubiriwa kwa hamu kwa sababu itawakutanisha ndugu wawili, Jude na Jobe Bellingham.
Mechi ya Madrid na Dortmund itapigwa katika dimba la MetLife Stadium, New Jersey kuanzia saa 5:00 usiku.