Mgunda anaanza na huyu, ni mkata umeme, wafanya kikao dakika 30

MWENYEKITI wa bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah 'Try Again' wala hatanii na hataki mzaha baada ya kurejea nchini mwisho wa wiki iliyopita akitokea Qatar na kuanza na mipango ya usajili wa kiungo.
Try Again amepata nguvu hiyo ya kukamilisha mipango ya usajili ndani ya Simba baada ya wiki moja nyuma kupokea simu ya mdhamini wao, Mohammed Dewji 'Mo Dewji' aliyemwambia yupo nyuma yake kwa kila kitu tofauti na maneno ya watu.
Mo Dewji ameonekana kukerwa na maneno mengi yaliyokuwa yakisambaa kwenye vijiwe vya soka, mitandao ya kijamii na maeneo mengine mbalimbali kuwa amejiondoa kwenye timu hiyo. Sasa Bilionea huyo kijana amepanga kufanya kweli kwenye usajili wa dirisha dogo.
Mwanaspoti limejiridhisha kuwa Try Again mara baada ya mchezo wa Simba na Geita Gold kumalizika, alimuita kiungo mkabaji, Kelvin Nashon na kufanya mazungumzo naye yenye usiri mkubwa ndani yake.
Katika kuhakikisha hilo linakamilika kwenye kikao hicho kilichochukua zaidi ya dakika 30, Try Again alikuwa pamoja na Nashon 'Mkata Umeme' na kaimu kocha mkuu, Juma Mgunda aliyeonekana kuwa na furaha muda wote.
Mgunda alionekana kuwa na furaha kwenye kikao hicho kwani Mkata Umeme huyo ni miongoni mwa wachezaji wazawa aliowapendekeza kwenye usajili wake wa dirisha dogo ili kuboresha eneo la kiungo.
Kwenye mazungumzo hayo, Try Again na Mgunda inaelezwa walimueleza Nashon, wapo tayari kumpa mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Simba kuanzia sasa.
"Walimueleza Nashon kama atakuwa tayari kabla ya usajili wa dirisha dogo kufungwa watamtumia tiketi ya ndege kutoka alipo hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha usajili wake," alisema mtoa taarifa (jina lake tunalo).
"Nashon ameambiwa akae na watu wake wa karibu ili kukubaliana maslahi ya usajili wake pamoja na mshahara ambao atakuwa anachukua kila mwisho wa mwezi.
"Baada ya kuzungumzia masuala hayo kila mmoja alikubaliana na mwenzake na kama hakutakuwa na mabadiliko yoyote dili hili linaweza kukamilika siku si nyingi kuanzia wakati huu.
"Kuhusu mkataba wake wa miezi sita aliyobaki nao Geita Gold, mabosi wa Simba walimueleza wala haina shida watakutana na uongozi wake kisha kulipa thamani ya muda uliobaki."
Alipotafutwa Nashon alisema: "Jambo hilo la usajili wangu kwenda Simba nadhani ni sahihi zaidi wao wenyewe ndio waeleze kila kitu ila kwa sasa bado nipo na Geita Gold, nguvu na akili ni kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Azam."
Nashon akifanikiwa kutua Simba atatakiwa kuwania namba na Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute ambao wanapata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza.
Wakati huohuo, kwenye nafasi hiyo ya kiungo mkabaji kuna nyota wengine kama, Jonas Mkude, Erasto Nyoni na Victor Akpan ambao wamekuwa hawana uhakika wa kucheza mara kwa mara.
Hata hivyo, kwenye nafasi hiyo ya kiungo mkabaji kuna taarifa kuwa uongozi wa Dodoma Jiji huenda ukatuma maombi ya kumhitaji, Akpan aliyesajiliwa na Simba dirisha kubwa la usajili msimu huu akitokea Coastal Union.
Simba inahitaji huduma na Nashon ili kuongeza nguvu katika eneo la kiungo haswa wa ukabaji huku ikiwa na uhakika wa kukaa na mchezaji huyo muda mrefu kutokana na umri wake kuwa mdogo ndio maana inaelezwa huenda ikamsainisha mkataba wa miaka mitatu.